February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

ZIARA YA MRATIBU THRDC SHIRIKA LA AACP MKOANI SHINYANGA

Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) amelitembelea Shirika la Agape Aids Control Program (AACP) lililopo mkoani Shinyanga kwa lengo lwa kubaini fursa na chnagmoto wanazopitia katika utekelezaji wa majukumu yao ya utetezi wa haki za binadamu.

Shirika hili linajihusisha na masuala ya haki za binadamu na Maendeleo ya jamii likiwa na malengo ya kuwezesha wanawake,kulinda watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia, kutoa elimu ya afya ya uzazi na kuona jamii ikipata haki.

Shirika hili limejikita zaidi katika kutoa msaada wa kisheria na kusaidia watoto wa kike ambao wapo katika mazingira hatarishi na wale waliopotia unyanyasaji wa kijinsia na wamefanikiwa kuanzisha nyumba salama kwa ajili ya watoto hao pamoja na shule.

Katika ziara hiyo THRDC imebaini changamoto mbalimbali zinazoikumba shirjka la AACP ikiwemo Changamoto ya fedha ikitajwa kuwa ni kikwazo kikubwa cha utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo.

“Tumekuwa na upungufu wa fedha,jamii inatufahamu vizuri na tumekuwa tukifanya vizuri hata ile gari ya wahitaji hasa watoto wanaokuja kusaidiwa inaongezeka na watu wengi wakija wanataka msaada wanategemea kusaidiwa sasa wakati mwingine ukosefu wa fedha unatuwekea mazingira magumu katika utekelezaji,” amesema Afisa Programu wa AGAPE.

Kwa upande mwingine kutokana na kuwepo kwa changamoto hiyo kumepelekea shirika hilo kushindwa kuajiri walinzi katika ofisi hizo ambako kuna nyumba salama za kukaa wasichana waliookolewa kutoka katika mazingira hatarishi na shule ambayo inasomesha watoto hao hali ambayo inawaweka hatarini.

Pia Changamoto nyingine inayoikumba shirika hilo ni kukithiri kwa vitendo vya rushwa pale ambapo kesi hizi za unyanyasaji wa kijinsia zinafikiswa katika vyombo vya sheria na kifungu cha sheria ya ndoa kinachoruhusu mtoto wa miaka 13 kuozwa na wazazi kikitumika kama mwanya wa kuendeleza vitendo hivyo.

“Ukiwa mahakamani hakimu anakwambia unaifahamu sheria ya ndoa? ulienda ukakuta mtoto anaolewa huoni mzazi ametumia sheria hiyo,ukiangalia mtoto ana miaka 15 na ni mwanafunzi lakini kasimamia hicho kijipengele tu,nimeulizwa si chini ya mara mbili tatu na mahakimu wanaangalia kipengele hicho tu hawaangalii sheria zingine,” John Myola,Mkurugenzi shirika la AACP.

Aidha Watendaji wa Shirika hilo wameeleza kuwa wanakutana na vikwazo mbalimbali ikiwemo kupata vitisho pale ambapo wanatekeleza majukumu yao kuiomba THRDC kuwawezesha kupata mawakili ambao watasimamia kesi wanazozifungua mahakamani

“Tuna shida sana ya wakili kuna kesi ambazo zinahitaji mtu asimame atusaidie kutusemea na kutuelekeza,watoto hawa wanatendewa vitendo vibaya sana ambavyo hatuwezi kufikiria,Tunahitaji wakili wa kusimamia kesi hizo,”John Myola,Mkurugenzi AACP

Pia Mratibu wa THRDC ,Olengurumwa amepata fursa ya kutembelea Shule ya Sekondari ambayo inamilikiwa na shirika hilo na kuona changamoto mbalimbali ikiwemo ufinyu wa madarasa na miundombinu ya elimu pamoja na kutokuwepo kwa walinzi ambao wanalinda eneo hilo huku Changamoto ya mabweni,madarasa kutokuwepo kwa uzio kuzunguka shule hivyo watoto hao wanaomba wadau wajitolee kuboresha kituo hicho cha usalama.

“Tupo hapa kutimiza ndoto zetu,tunaomba kusaidiwa vifaa kama madarasa,kompyuta pamoja na ulinzi kwasababu bado kule tulipotoroka unyanyasaji wanaendelea kutufuatilia,”amesema mmoja wa wahanga wa ndoa za utotoni anayesoma katika shule hiyo.

Shule hiyo kwa sasa ina wanafunzi 40 na wote wakiwa ni wasichana ambao wameokolewa kutoka katika ndoa na mimba za utotoni.

Kwa mujibu wa AACP wanasema kuwa matukio ya ubakaji,ndoa na mimba za utotoni yamekithiri kwa kiasi kikubwa katika mkoa huo na wasichana wadogo wamekuwa wakiachishwa shule na kuozwa kwa watu waliowazidi umri na kuhusu matukio ya ubakaji mengi yanafanywa na ndugu wa karibu wakiwemo wazazi na walezi wa watoto hao.Na ili kutatua changamoto hiyo shirika limekuwa likifungua kesi mbalimbali mahakamani lakini kutokana na kukosa mawakili wamekuwa wakishinda kesi chache kati ya nyingi wanazozifungua.

Baada ya kusikia changamoto pamoja na kazi zinazofanywa na shirika hilo Mratibu Olengurumwa amelipongeza shirika hilo kwa kazi nzuri wanayofanya na kutoa wito wa kuendelea kufanya kazi zao katika mazingira salama huku akiahidi kutafuta njia ya kuwezesha kupatikana kwa mawakili watakaosimamia kesi.

“Tunaahidi kusaidia kufanya fund raising kwa ajili ya kituo hiki salama na shule ili iweze kupata majengo ya madarasa,uzio,walinzi pamoja na matron wakudumu” ameeleza Mratibu THRDC.

Aidha Afisa Dawati la Wanachama THRDC,Lisa Kagaruki ameiasa AGAPE kutosita kuripoti kuhusu matukio ya kiusalama hasa pale wanapopata vitisho na kuwataka kuendelea kusaidiana kwa ukaribu na Kituo cha Watetezi TV katika kuibua changamoto mbalimbali za uvunjifu wa haki za binadamu.