February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

ZIARA YA MRATIBU THRDC KATIKA SHIRIKA LA ACTION FOR DEMOCRACY AND LOCAL GOVERNMENT ADLG

Na Loveness Muhagazi

Mratibu kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Nchini Tanzania THRDC Onesmo Olengurumwa hii leo anetembelea taasisi ya Action for Decmocracy and Local Government – ADLG, ADLG ni taasisi inayojishughulisha na masuala ya Uwajibikaji kidemokrasia na katika ngazi ya serikali za mitaa.

“Taasisi yetu inafanya kazi Zaidi na jamii tunaamini pale jamii inapojengewa uwezo wa kujitambua hapo jamii hiyo inakuwa na uwezo wa kuweza kujua inataka nini na nini haitaki na jamii hiyo inaweza kudai uwajibikaji katika eneo wanaloona ni sawa zaidi, tunaamini kuwa mabadiliko yoyote kwa jamii lazima yaanzie kwa Jamii yenyewe kwanza” Jimmy Luhende Mkurugenzi wa Taasisi ya ADLG.

Taasisi ya ADLG imekuwa ikifanya kazi na jamii tatu, jamii ya wakulima wadogo wadogo kwa mikoa ya Shinyanga, Geita na Simiyu, jamii ya wachimbaji wadogo wa madini, Pamoja na jamii ya Wavuvi ambao wamekuwa wakikumbana na changamoto mbali mbali katika shuguli zao. Ili kuhakikisha jamii hizo zinasaidika, taasisi ya ADLG imekuwa ikishirikiana na taasisi zingine za utetezi wa haki za Binadamu kama taasisi ya Haki Rasilimali na ANSAF ili kuhakikisha jamii inahudumiwa vyema.

Pamoja na kufanya kazi na hayo makundi ADLG ilifanya utafiti na kugundua vijana na wanawake wanakumbana na changamoto mbali mbali na vitendo vinavyohatarisha amani na usalama wao , hasa katika chaguzi jambo lililopelekea taasisi ya ADLG kuangalia namna ya kutoa usaidizi kwa upande huo na kupunguza wahanga. Hivyobasi, ADLG iko mbioni kuanza programu ya Vijana na Amani na Usalama, na Hadi sasa, mashirika takribani 20 yanategemea kutekeleza program hii.

“Katika kuhakikisha kunakuwepo na uwajibikaji tunafanya kazi na jamii, tunatamani kuona Asasi za kiraia zinafanya kazi na Serikali kuhakikisha kunakuwepo na uwajibikaji, lakini pia kushirikiana na baadhi ya sekta serikalini katika masuala yanayohusu ufuatiliaji kwa mfano wizara kama TAMISEMI” anaongeza Jimmy Luhende.

Taasisi ya ADLG inakumbana na Changamoto mbali mbali katika utekelezaji wa kazi zake ikiwemo kuwepo kwa mashirika machache yanayojikita katika eneo la Uwajibikaji, Sekta ya AZAKi inafanya kazi katika ngazi ya jamii na vijiji, ambapo suala la ufuatiliaji wa uwajibikaji wa mamlaka ingewekwa katika majukumu yao. Mashirika mengi hayajikiti humu kwasababu eneo hili ni hatarishi. Hata hivyo, changamoto ya uwajibikaji ipo katika ngazi ya mtu mmoja mmoja katika taasisi, na sio taasisi nzima ya serikali.

Bw Luhende ashauri kuwa ni muhimu kwa wanachama wa mtandao wanaofanya kazi za utoaji huduma kuwa na kipengele cha kudai uwajibikaji wa mamlaka katika ngazi zao za utekelezaji.

“Kwa kuongezea, ADLG ilifanya mradi wa kupinga rushwa, Anti-corruption project, ambapo mradi huu ulikua wa miaka 3, iliyoshirikiana na TAKUKURU, Mradi huu uliwafikia mikoa saba. ADLG imekua ikitafakari namna ya kurudia kufanya mradi huu kwa kuungana na mashirika 10 ili kuutekeleza kwa Pamoja kwani mradi huu umekua moja ya miradi yenye mafanikio makubwa” Jimmy Luhende

Mratibu THRDC ameipongeza taasisi hii ya ADLG kwa kufanya kazi za uwajibikaji na kutekeleza majukumu katika ngazi ya Kijiji. Pia mratibu alikabidhi makabrasha kutoka THRDC, ikiwemo majarida ya compliance, mpango wa utekeleza wa AZAKi wa FYNDP, Pamoja na mengine mengi ya Mtandao. Mratibu awasihi wanachama wa Mwanza kutekeleza miradi yao, na kuiainisha na mpango kazi wa kitaifa ili kuchochea nafasi ya mashirika yasiyo ya kiserikali katika maendeleo ya taifa.

MWISHO