February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

ZIARA YA MRATIBU KITAIFA WA MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU TANZANIA KAHAMA

Kahama, Shinyanga.

Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Wakili Onesmo Olengurumwa akiambatana na Afisa Ushawishi na Wanachama, Lisa Kagaruki, wamehitimisha ziara kwa mkoa wa Shinyanga kwa kutembelea Shirika la The Foundation of Human Health and Social Development (HUHESO), Kahama.

HUHESO ni taasisi inayojihusisha na utetezi wa haki za wanawake na wasichana hasa katika upande wa afya. HUHESO imejikita katika sehemu kuu tatu;


•HUHESO FM
•HUHESO Institute
•HUHESO foundation


Ambapo sehemu zote ni njia mbalimbali za kuendelea kutetea haki za binadamu na Kwasassa, HUHESO Foundation ina miradi miwili (EPIC program na Mwanamke Amka). Miradi hii yote ni kwa ajili ya wasichana balehe, na wanawake pamoja na makundi maalum yaliyo katika hatarishi ya kupata maambukizi ya VVU, na magonjwa ya zinaa.

HUHESO FM (104.5 FM)


Hii ni radio iliyo chini ya usimamizi wa HUHESO ambapo ina vipindi mbalimbali vyenye kuibua ukatili wa kijinsia katika ngazi za wilaya na vijiji. Radio hii ilianza 2018 ambapo tangu huo mwaka, wameweza kushirikiana na wananchi, watetezi wa haki za binadamu, mashirika mbalimbali na hata mamlaka za kiserikali katika kupaza sauti kwa ajili ya haki za msichana na mwanamke.

HUHESO Institute


Hiki ni chuo kinachofuata mtaala wa VETA na NACTE katika kuwajengea uwezo vijana kwa upande wa ujasiriamali, uandishi wa habari, pamoja na maendeleo ya jamii. Kimeanzishwa mwaka huu 2021 ambapo tayari kina wanafunzi zaidi ya 25. Hii ni njia moja wapo ambayo HUHESO wanaitumia ili kuwapa msingi wa maisha vijana wa Kahama, Shinyanga na kuipa jamii ujuzi na maarifa ya kujitegemea.

Changamoto zinazowakabili HUHESO ni nyingi ikiwemo;Uelewa wa jamii juu ya kazi za HUHESO Foundation kwa upande wa haki ya afya kwa makundi maalumu bado ni mdogo sana,Elimu ya kiusalama waliyonayo ni ndogo katika kukabili changamoto zinazowapata pindi wakitekeleza majukumu yao,Changamoto ya kifedha na Masuala ya utekelezaji wa matakwa ya kisheria kupitia njia ya kidigitali imekua ni changamoto kwa HUHESO. Ingawa changamoto hii imelazimika kukabiliwa kutokana na kuhofia faini na adhabu kutoka mamlaka husika.

Hata hivyo, HUHESO imeonekana kuwa na mashirikiano mazuri na serikali, wanachi wa Kahama, mashirika mengine kama vile SHIHABI, na vyombo vya kiusalama.Ulinzi wa Ofisi za HUHESO upo vizuri, jengo lina gate pamoja na uwepo na mlinzi ni jambo la kusifika. HUHESO ipo njiani kufunga camera za ulinzi ili kuendelea kuimarisha usalama wao.

Mkurugenzi wa HUHESO foundatio, Bw. Mwesigwa Mohamed ameishukuru sana THRDC kwa kuendelea kushirikiana nao katikao utetezi wa haki za binadamu, hasa katika utoaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo. Vivyohivyo, ameushukuru mtandao kwa vitabu na vipeperushi vilivyokua vikitolewa kama muongozo wa utetezi wa Haki za Binadamu.


Kwa upande wake Mratibu Kitaifa ameipongeza sana HUHESO na amelishauri shirika hilo kuendelea na mashirikiano mema na serikali pia kuwepo na mshikamano kati ya wanachama wa Mtandao, hasahasa wanaotetea haki ya aina moja, kuendelea kufata sheria na taratibu zote zilizowekwa na mamlaka husika pamoja na kuendelea kutumia vizuri rasilimali zao, na kufanya kazi wa uwazi na weledi katika jamii.


Mratibu ameshauri watetezi wa haki za binadamu watumie HUHESO Fm kutoa elimu kuhusu haki za mtoto wa kike, na ukatili wa kijinsia kwa jamii ya watu wa mkoa wa Shinyanga ambapo bado kuna changamoto kubwa sana juu ya upatikanaji wa haki za mtoto, hasa mtoto wa kike na wanawake kwa ujumla.

Afisa dawati ameishauri HUHESO FM kuwa mabalozi wazuri wa Watetezi TV katika kuhabarisha umma juu ya uvunjifu wa haki za binadamu nchini.