February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

ZIARA YA MRATIBU KITAIFA THRDC MKOA WA SHINYANGA

Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Wakili Onesmo Olengurumwa akiambatana na Afisa Ushawishi na Uanachama, Bi. Lisa Kagaruki, wametembelea Shirika la Rafiki Social Development Organization (Rafiki SDO), Shinyanga mjini.

Rafiki SDO ni taasisi inayojihusisha na maendeleo na utetezi wa haki za binadamu kwa jamii, linalofanya kazi na makundi mbalimbali ikiwemo watoto, vijana, na makundi maalum.

Shirika hili limejikita kufanya kazi nchi nzima huku makao makuu yakiwa Shinyanga mjini. Rafiki SDO inaendesha miradi mbalimbali kwa jamii kwa lengo la kubadili perspective ya jamii na kupunguza uvunjifu wa haki za watoto, hasa watoto wa kike.

Picha : Mkurugenzi wa Shirika la SDO,Gerald Ng’ong’a akiwa ofisini kwake hii leo wakati alipotembelewa na Mratibu wa THRDC mapema hii leo.

Pamoja na Kazi ambazo zimekuwa zikifanywa na Rafiki SDO, bado kumekuwa na changamoto mbali mbali ambazo shirika hili limekuwa likikitana nazo ambazo ni pamoja na;

Ujuzi mdogo kwa maafisa wa habari juu ya kazi zinazofanywa na AZAKI. Mara nyingi habari zinazotolewa juu ya kazi zao hupotosha umma na mara nyingine kuwasababishia matatizo na mamlaka husika pia Ofisi haina mwanasheria ingawa imeweza kufuata taratibu zote za kisheria zilizowekwa na mamlaka huku Jamii huficha uvunjifu wa haki za binadamu zinazotokea katika maeneo yao.

Utofauti wa mila na desturi umekuwa ukizuia sana uwezekano rahisi wa kuzifikia baadhi ya jamii zenye tamaduni na misimamo mikali katika maswala ya haki za watoto, hasa katika kuwapatia elimu juu ya maswala ya ukatili wa kijinsia, na elimu ya uzazi.Hatahivyo, Rafiki SDO inafanya kazi kwa ukaribu sana na serikali za ngazi zote ikiwemo serikali za mitaa na vijiji katika kuwafikia walengwa.

Pamoja na Changamoto hizo kumekuwa na faida ambazo ni pamoja na kuwepo kwa Mahusiano mazuri na serikali za ngazi zote. Hii imeweza kusaidia kwa namna kubwa sana utekelezaji kamili wa miradi ya shirika.

Rafiki SDO wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali kwa vijundi vya vijana. Hivi sasa wapo mbioni kutoa baiskeli zaidi ya 100 kwa vijana kama njia ya usafiri ili kutimiza majukumu yao ya ujasiriamali.

Baada ya kusikiliza changamoto na fursa za taasisi ya Rafiki SDO, Mratibu wa mtandao wa Watetezi wa haki za binadamu Tanzania, THRDC, Onesmo Olengurumwa ameipongeza sana na ameiasa taasisi hiyo kuendeleza mahusiano hayo mazuri na serikali ili kuendelea kuifikia jamii kwa upana na kuwawezesha wananchi kupata elimu mbalimbali na kuendelea kuwashika mkono vijana wa kike.

Afisa dawati la wanachama THRDC Lisa Kagaruki ameishauri Rafiki SDO kutumia ipasavyo kituo cha televisheni cha Watetezi TV, kuibua baadhi ya changamoto zinazowakumba Watetezi wa Haki za Binadamu mkoani humo ili kufanikisha utatuzi wa haraka pamoja na kuionyesha jamii kazi ambazo zimekuwa zikifanywa na Watetezi hao kwa upana zaidi.