February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

ZIARA YA MENEJA PROGRAMU WA THRDC KATIKA SHIRIKA LA KAYD

Meneja Programu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania Bw. Remmy Lema akiambatana na Mkuu wa Dawati la wanachama la Mtandao, Lisa Kagaruki pamoja na Mratibu wa Kanda ya Magharibi, Bw. Alex Luoga wametembelea shirika mwanachama Kasulu Youth Development (KAYD) lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

KAYD inajihusisha na haki za vijana, huku ikijikita katika kuzisaidia kaya na vijiji vya pembezoni kiuchumi na kijamii, hasa katika upatikanaji wa chakula na lishe (WASH) kupitia kilimo endelevu, elimu, Afya, mafunzo ya ufundi stadi, amani, maswala ya jinsia, demokrasia na Utawala Bora, pamoja na Haki za Binadamu.

Taasisi inaendesha karakana inayowawezesha vijana kupata mafunzo ya ufundi stadi, na mbinu za ujasiriamali unaowasaidia kuepukana na shughuli za utumikishwaji katika ajira mbali mbali.

KAYD imefanikiwa kuigusa jamii katika maeneo mbali mbali ikiwemo;
• Utoaji msaada wa madawati 30 kwa shule pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa. Hii ni kupitia chuo cha mafunzo kilichopo chini ya shirika hilo.

• KAYD imekuwa ikijenga uwezo wa wafanyakazi Ili kuweza kufanya kazi kwa weledi, pamoja na kupata wadau wa kimkakati wanaoweza kusaidia katika uendeshaji wa programu za taasisi.

• Kuwajengea uwezo wabadili tabia 50 ambao wameweza kuhamasisha jamii kubadili mitazamo ya wanaume hasa katika namna ya kuwasaidia wake zao Kazi na kutowaona kama vyombo vya starehe, lakini pia kuwajengea uwezo wanawake hasa katika maswala ya umiliki ardhi.

• Zaidi ya wanufaika 200,000 wejengewa uwezo na kuiwezesha jamii kutambua umuhimu wa kusomesha watoto na kusaidia wanawake katika umiliki wa rasilimali.
• Ajira zimeongezeka miongoni mwa vijana na kupunguza utumikishwaji.

Pamoja na kazi kubwa inayofanywa na KAYD, bado inabaini uwepo wa changamoto kadhaa ikiwemo;

1) Mila na desturi zinazochangia ukandamizaji hasa kwa wanawake.

2) Rushwa inayopelekea kushindwa kukomeshwa kwa vitendo vya ukatili ambapo mara nyingine mamlaka huingilia Haki za Binadamu kupitia ukamatwaji wa Watetezi.

3) Ufinyu wa rasilimali fedha unaosababisha taasisi kushindwa kufikia watu wengi, pamoja na umaskini, ambao hupelekea watu kushindwa kufuatilia michakato ya upataji haki na kuishia njiani.

4) Umasikini uliokithiri unaowapelekea wazazi kushiriki katika kubuni mbinu
za kuwazuia watoto kusoma Ili kufanya kazi za kuingiza kipato katika familia.

5) Matukio ya kupotezwa kwa watu wakiwemo watetezi wa haki za binadamu na kupelekwa kusikojulikana.

Pamoja na majadiliano hayo, KAYD imeshuhudia kurekodi kisa cha mtetezi wa haki za binadamu wilayani humo, aliyepotea kwa muda wa miaka miwili sasa. KAYD imeiomba THRDC kusaidia katika kufuatilia swala la Mtetezi huyo aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha miaka miwili (2) iliyopita mara baada ya kukamatwa na Polisi.

Meneja Programu ameeleza kuwa Mtandao THRDC umepokea taarifa za kupotea kwa Mtetezi huyo na kulifanyia ufuatiliaji kama moja ya majukumu ya Mtandao.

Pia amepongeza taasisi kwa kufanya kazi kwa weledi na kufanikiwa kuifikia jamii kwa kiasi kikubwa katika kutatua baadhi ya changamoto zinazoikumba jamii.

Ameishauri taasisi kuwa na mpango mkakati (Strategic plan) Pamoja na kuandaa Mpango kazi ambao unaweza kurahisisha utekelezaji wa mpango mkakati huo.

Pia ameikumbusha taasisi kuwasilisha ripoti ndani ya muda Ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza kwa kushindwa kufanya hivyo.

Mkuu wa Dawati la Wanachama, Bi. Lisa Kagaruki, ameipongeza taasisi ya KAYD kwa kuwa na utaratibu wa kutunza Taarifa za shughuli zinazotekelezwa na taasisi ambazo hutoa mwanga na kuonyesha ufanisi wa taasisi.

Pia ameishauri taasisi kuendelea kutumia Watetezi TV katika kuripoti matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaotokea katika maeneo yao, na hata shughuli zinazoendeshwa na Taasisi.