February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

ZANZIBAR:THRDC KUWAKUTANISHA MAJAJI,MAHAKIMU MARA MBILI KWA MWAKA.

Salma Ali Hassan-DPP-Zaanzibar

Na Leonard Mapuli-Zanzibar

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wa Zanzibar,Salma Ali Hassan,amewataka Majaji na Mahakimu wote wanaotekeleza majukumu yao visiwani humo,kutochoka kusoma sheria mbalimbali,zitakazowasadia kurahisisha utoaji wa maamuzi ya mashauri mbalimbali katika majukumu yao.

Bi. Salma ameyasema hayo wakati wa kufunga mafunzo ya siku mbili kwa Majaji,Mahakimu,na taasisi mbalimbali zinazohusiana na utoaji haki,yaliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),tawi la Zanzibar,yaliyofanyika katika eneo la Kiembe Samaki,na kufunguliwa na kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar, Hamis Ramadhan.

“Niwashauri Majaji na Mahakimu wote mliopo hapa,msichoke kusoma zaidi na Zaidi masuala ya sheria ili tuweze kufanya maamuzi kwa usahihi”amesema Jaji huyo na kuishukuru taasisi hiyo kwa kuandaa mafunzo hayo,kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa Haki za binadamu visiwani humo ambao ni haki ya kila mtu.

“Tuliyojifunza hapa tuyachukue,maana yanatugusa wote,uwe Jaji,Hakimu,Polisi,mwandishi,fikilia jambo unaloliona mbele yako lingekuwa linakuja kwako ungefanyaje”ameongeza DPP Salma.

Abdallah Abeid-Mratibu,THRDC-Zanzibar

Awali,Mratibu wa Mtandao huo visiwani Zanzibar,Abdallah Abeid,amesema mafunzo hayo yameimarisha nguvu ya pamoja baina ya wadau wa upatikanaji wa haki visiwani humo.

“Ukweli ni kwamba,kuna kazi nyingi nimejikuta nazigundua kupitia mafunzo haya ambazo ni lazima zifanyike hapa Zanzibar katika masuala mazima ya Haki”,amesema Abdallah.

Onesmo Olengurumwa-Mratibu wa Kitaifa wa THRDC

Mratibu waKitaifa wa  Mtandao,Wakili Onesmo Olengurumwa,amehitimisha kwa kuwashukuru wote walioitikia wito katika mafunzo hayo,na kuiomba Mahakama iendelee kushirikiana na Mtandao huo, si tu katika eneo la Haki za binadamu,bali mambo yote,maana hakuna jambo lisilo na haki ndani yake na kwamba taasisi ya THRDC kwa kuanza,itakuwa ikiwakutanisha Majaji,mahakimu,na taasisi zingine za usimamizi wa Haki za Binadamu angalau mara mbili kuanzia mwaka 2022.

“Uzuri wa Zanzibar  ni eneo dogo,na Rais wetu ni msikivu,tuendelee na utaratibu huu wa mafunzo,ili baada ya miaka miwili au mitatu,Zanzibar iwe ni sehemu ya watu kuja kujifunza masuala ya Haki za Binadamu”,amesema Olengurumwa,wakati akitoa neno la mwisho kwa washiriki wa mafunzo hayo,ambao ni Majaji,na Mahakimu kutoka Unguja na Pemba.

Prof.Chris Maina-Moja ya wawezeshaji wa mafunzo.

Watoa mada katika mafunzo hayo walikuwa Jaji Mstaafu, Joaquine De Mello,Jaji Mstaafu Awadh Bawazir, Profesa Chris Maina Peter,na Dr. Clement Mashamba na yamehitimishwa leo,Novemba 28.