February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

YAFAHAMU MAMBO MATANO MUHIMU BAADA YA SPIKA NDUGAI KUJIZULU

Na: Anthony Rwekaza

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo siku ya Alhamisi ya January 6, 2021 akidai maamuzi hayo ameyafanya kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa lake.

Akieleza dhamira yake kwenye barua alioiandika kuelekea kwenye ofisi ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwenye barua hiyo ametoa shukrani kwa Wabunge huku akisema uamuzi alioufanya ni binafsi na wa hiari.

Barua hiyo haijaonesha na kuweka bayana moja kwa moja sababu iliyomplekea Spika Ndugai kufanya uamuzi huo, lakini baadhi ya wadau hasa kwenye mitandao ya kijamii wamekuqa mitazamo yao kwa kuhusianisha uamuzi huo na sakata ambalo limekuwa gumzo Nchini Tanzania.

SABUBU IPI INATAJWA KUPELEKEA UAMUZI HUO?

Itakumbukuwa kilienea kipande cha video kwenye mitandao ya kijamii, ikiwa ni muda mchache baada Spika Ndugai kumaliza kutoa hotuba yake Desemba 26, 2021 alipoalikwa kwenye tukio la makumbusho ya ya kabila la Wagogo, baadhi ya wananchi wakiwemo viongozi na Wanachama wa ngazi mbalimbali wa CCM waliibuka na kutoa maoni yao juu ya sakata hilo, baadhi yao walionekana kumpinga.

Baadhi ya kauli aliyonukuliwa akiitoa Ndugai ni “Juzi mama ameenda kukopa 1.3 trilioni. hivi ipi bora. Sisi Watanzania wa miaka 60 ya uhuru kuzidi kukopa na madeni au tubanane banane hapa hapa, tujenge wenyewe bila madeni haya makubwa makubwa haya yasiyoeleweka. Ni lini sisi tutafanya wenyewe ‘and how’ (na kwa vipi),” alisema Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania, Job Ndugai

Kufuatia sakata hilo kuonekana kuwa gumzo mnamo January 3, 2022 Spika Ndugai alijitokeza na kufanya mkutano na vyombo vya habari kwenye Ofisi za Spika Bungeni Jijini Dodoma ambapo aliomba radhi kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania wote kufuatia kipande hicho cha video(clip), lakini Ndugai alienda mbali zaidi na kusema kauli zake zilitafsiriwa kinyume na makusudio yake huku akidai teknolojia imetumika kukata kipande hicho na kukikuza na hali iliyopelekea sintofahamu.

Lakini Rais Samia Suluhu Hassan January 5, 2022 wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa dola, kupitia kauli zake alionekana kuwashangaa wanaokosoa mikopo inayokopwa na Serikali anayoiongoza tokea alipoingia madarakani ikiwemo mkopo wa trillion 1.3 ambao ulitajwa pia kwenye kipande cha video ya hotuba ya Ndugai.

Rais Samia alidai kuwa mkopo huo ni mzuri hata kuliko baadhi ya mikopo mingine iliyowai kukopwa awali kwenye Serikali zilizopita, lakini aliongeza kuwa wapo baadhi ya watendaji wakiwemo baadhi Mawaziri wameanza kuonyesha hali ya kuwania Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2025, alidai kuwa atafanya mabadiliko ili wenye dhamira hiyo wakae nje ya mifumo ya kiutendaji ili wajipange vizuri na uchaguzi, kuliko kubaki kukwamisha shughuli muhimu za wananchi.

Sakata hilo linafanya wengi kuamini kuwa hiyo ndiyo sabubu iliyopelekea Spika Ndugai kutangaza kuachia nafasi hiyo, hasa kiini cha mtazamo huo kinatokana na hasa pale Ndugai alipojitokeza kuomba radhi.

NDUGAI ALIVYOUPATA USPIKA WA BUNGE

Job Ndugai ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa ambalo Mkoani Dodoma, mnamo tarehe 10 Novemba 2020, alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge la 12 baada ya kupata kura 344 kati ya kura 345 zilizopigwa sawa na asilimia 99.7. Ndugai alifanikiwa kutetea kiti hicho ambapo alikuwa Spika wa Bunge la 11 tokea 2015 – 2020.

Jina la Ndugai lilipendekezwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) ili kupigiwa kura ya siri na Wabunge na alifanikiwa kupitishwa kwa vipindi viwili tofauti licha ya kung’atuka kabla ya muda. Ambapo alikuwa na mamlaka ya kisheria ya kuendelea kuwa Spika mpaka 2025 isipokuwa ikitokea sababu za kisheria ikiwemo pale Bunge lingevinjwa au Spika kama ingetokea ameshindwa kukidhi matakwa ya sheria, taratibu na kanuni zinazoongoza Bunge.

Imeripotiwa kuwa Katibu wa Bunge Nenelwa Mwihambi tayari amepokea nakala ya kujiuzulu kwa Spika Job Ndugai, aliyopelekewa na Katibu Mkuu wa CCM Bw.Daniel Chongolo, ambapo akibainisha kuwa upande wa chama kimeridhia kujiuzulu kwake.

BAADA YA SPIKA KUJIUDHURU HALI INAKUWAJE, BUNGE LITAENDELEA BILA SPIKA?

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 imelizungumzia Bunge kuwa ni muhimili kati ya mihimili mitatu kwenye Nchi, ambayo mingine ni Mahakama, Utawala (Serikali), hivyo shughuli zake uendeshwa kwa misingi ya sheria na taratibu.

Kwahiyo Katiba hiyo Mama ambayo ni msingi wa sheria nyingine mbalimbali kwenye Nchi, inaeleza kuwa ili shughuli za Bunge kuendelea inatakiwa kiti cha Spika wa Bunge kiwe kimejazwa.

Hivyo kutokana ya taratibu za kisheria, inatarajiwa mchakato wa kumpata Spika kufanyika kabla ya shughuli hizo kuanza, ambapo kwa mujibu wa melezo ya Job Ndugai kabla ya kujiudhulu kwake, akisema January 3, 2022 kuwa shughuli za Bunge zinatarajiwa kuanza rasmi January 17, 2022.

Inategemea Ofisi ya Katibu wa Bunge kwa kuzingatia miongozo ya kisheria kuweka bayana mchakato wa uchaguzi wa Spika, ambapo Chama kinachokidhi sifa ya kupendekeza jina la Spika kitawasilisha jina kwenye ofisi hiyo ili kupigiwa kura ya siri, kumpata Spika wa Bunge mpya ambaye atakuwa Mkuu wa muhimili wa Bunge kama ilivyoelezwa kwenye Katiba.

MATUKIO GANI YANAWEZA KUKUMBUKWA KIPINDI NDUGAI AKIWA SPIKA?

Yapo matukio mbalimbali ambayo yalijitokeza katika kipindi ambacho Spika Ndugai alikuwa kwenye kiti hicho, matukio hayo hayahusiani na yeye binafsi moja kwa moja isipokuwa yanaweza kuihusianisha na kipindi ambacho amekuwa kiongozi wa muhimili ambao umekuwa na jukumu la kutunga sheria na kupitisha Bajeti ya Serikali na kuisimamia Serikali.

Tukio la kumvua Ubunge Tundu Lissu; ilikuwa ni kipindi cha Bunge la 11 ambapo aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alivuliwa Ubunge rasmi kwa madai ya kukosa sifa za kisheria za kuendelea kuwa Mbunge baada ya kuelezwa kuwa kutoonekana bungeni bila Spika kuwa na taarifa ya maandishi na kutojaza fomu ya tamko la mali na madeni. Hali hiyo ilipelekea Bunge hilo lililoongozwa na Job Ndugai kuifamisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kutangaza Jimbo la Singida Mashariki kuwa lipo wazi.

Itakumbukwa baada ya hapo NEC ilitangaza rasmi uchaguzi mdogo kwenye Jimbo la Singida Mashariki na michakato ilifanyika na iliwezesha kumpata Mbunge mpya kupitia tiketi ya CCM lakini Chadema hawakusimamisha mgombea kwenye uchaguzi huo. Baada ya hapo Tundu Lissu alianza mchakato wa kudai mafao yake, huku akidai kukutana na kisiki kizito kwenye mchakato huo, hali hiyo ilipelekea mabishano ya hoja na Ndugai.

Sakata hilo zima lilikuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii na iligonga vichwa mbalimbali vya magazeti Nchini Tanzania hata kwenye vyombo mbalimbali vya kimataifa, huku wengine wakikosoa uamuzi wa kumvua Ubunge Tundu Lissu lakini hawakukosa wale wenye mawazo mseto ambao walitete uamuzi huo.

Jambo lingine ni la aliyekuwa Mthibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ( CAG), Prof. Musa Assad kutoa kauli iliyokuwa kuwa Bunge ni dhaifu, baada ya kauli hiyo kuenea Ndugai alijitokeza na kumkabili, hali hiyo ilipelekea majibizano ya hoja mpaka pale CAG huyo alipotenguliwa na kuteuliwa CAG mwingine. Jambo hilo pia liligonga vyombo vya habari na kufanywa mjadala kwenye mitandao wa kijamii.

Ndugai pia katika kipindi chake cha uspika imeshudiwa baadhi ya Wabunge wakiwajibishwa na Kamati ya nidhamu kutokana kudaiwa kufanya vitendo vyenye viashira vya utovu wa nidhamu, baadhi yao walionywa na wengine kusimamishwa kutoshiriki vikao kwa muda akiwemo Mbunge wa Jimbo la Kawe, Josephat Gwajima na Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Jerry Slaa.

Mbunge Josephat Gwajima alidaiwa kutoa taarifa za uzushi zinazokiuka maelekezo na msimamo wa Serikali kuhusiana na sakata la chanjo ya Corona huku Jerry Slaa akisimamishwa kutokana na kutoa kauli iliyodaiwa kuitoa kwamba Wabunge hawakatwi Kodi, ikidaiwa kuwa sio kweli bali inachonganisha.

Kati ya mambo ambayo hayawezi kuachwa nyuma, ambayo yalichukua nafasi hasa kipindi cha Bunge la 11, 2015/2020, Ndugai akiwa Spika ni mabadiliko ya sheria mbalimbali yaliyofanywa, ikiwemo mabadiliko ya Sheria ya vyama vya siasa, pia kupanua wigo wa kinga ya kisheria aliyokuwanayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tu, hadi kinga hiyo kuwafikia Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Spika wa Bunge…

Sakata lingine ni kuwatambua Wabunge wa viti maalumu 19 ambao wanadaiwa kutokana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Ikumbukwe baada ya uchaguzi Mkuu 2020 Chadema walitakiwa kuwasilisha mjina ya Wabunge wao wa viti maalumu ambao ni Wanawake kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi inavyoelekeza baada ya Chama hicho kukidhi sifa.

Hata hivyo Chadema kupitia Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chama hicho pamoja na Baadhi ya viongozi wengine ambao ni wajumbe wa Kamati kuu walidai kugomea kupeleka majina ya Wabunge wa viti maalumu kwa madai mbalimbali ikiwemo kulalamikia mchakato ya Uchaguzi Mkuu 2020 ulivyoendeshwa, lakini mjina ya Wabunge hao 19, waliapishwa Bungeni huku licha ya Chadema kudai kuandika barua kutaka mamlaka za kibunge wasiwatambue kama wamepewa ridhaa na chama.(barua hiyo Ndugai aliifananisha na kipeperushi, kwa madai kuwa haikuzingatia taratibu)

Hali hiyo iliibua sintofahamu baina ya Chadema na Bunge, huku Ndugai akihaidi kulinda haki za Wabunge hao jambo ambalo liliendelea kuwa gumzo hasa pale ambapo Kamati Kuu ya Chadema ilivyoweka bayana kuwavua nyadhifa zote ndani ya Chama na uanachama wao.

WANANCHI WAMEPOKEAJE UAMUZI WA NDUGAI, KUN’GOKA?

Hipo mitazamo tofauti juu ya uamuzi uliofanywa na Job Ndugai, yapo makundi ambayo yanadai kuwa uamuzi huo utalinda heshima yake kwa kuwa naye amekuwa mstari wa mbele kuwajibisha wale ambao utoa kauli ambazo zinaweza kuleta taharuki au kuzorotesha juhudi za Serikali, huku wengine wakienda mbali zaidi kuwa ameonyesha ukomavu wa kisiasa.

Licha ya mtazamo huo, lakini wengine kwenye mitandao ya kijamii wanadai kuwa Ndugai alijikaanga kwa kauli zake mwenyewe hivyo kinachotokea kilitegemewa, lakini hoja ya Katiba Mpya imekuwa sehemu ya mitazamo ya wadau wengine ikiwemo kwenye mitandao ya kijamii wakidai mazingira yaliyopelekea Ndugai kun’goka ni kutoka na changamoto za kikatiba, wanaenda mbali zaidi na kudai kuwa katiba mpya itaongeza zaidi uhuru na utendaji wa mihimili na mipaka yake, ikiwemo Bunge.