February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

WITO WA MAHAKAMA KUMUITA NDUGAI WAGONGA MWAMBA, ASHINDWA TENA KUFIKA MAHAKAMANI

Shauri namba 2/2022 linaendelea kusikilizwa kwenye Mahakama Kuu Dar es salaam, ambapo kwa mara ya pili Job Ndugai ambaye anatakiwa kujibu maombi yaliyowasilishwa kwenye shauri hilo ambapo Mwenyekiti wa NCCR, Mageuzi James Mbatia akiwa na jopo la Mawakili wanapinga utaratibu uliotumiwa na Ndugai kujiudhulu nafasi ya uspika.

Awali upande wa waleta maombi Januari 24, 2022 ulielekezwa na Mahakama kufanya tena mchakato wa kumpelekea nyaraka ya wito Job Ndugai baada ya kutojulikana kama nyaraka ya kwanza waliyompelekea ilimfikia, licha ya waleta maombi kueleza Mahakama kuwa baada ya utaratibu wote waliojaribu kuutumia ili wito huo kumfikia Ndugai kushindikana, waliamua kumtumia wito huo kwa njia ya barua pepe (Email).

Mawakili wa upande waleta maombi wamesema walifuata maelekezo ya Mahakama kutaka wafanye mchakato wa kumfikishia wito Job Ndugai, lakini wameeleza Mahakama mbele ya jopo la Majaji watatu kuwa walitumia mtendaji wa majukumu ya Mahakama ambaye alienda kwenye makazi yake ya kibunge Jijini Dodoma lakini hakufanikiwa kumkuta na wamesema kuwa alipojaribu kuwaachia walinzi walikataa kupokea nyaraka hiyo.

Wameongeza kuwa baada ya hapo walienda kwenye Ofisi za Katibu wa Bunge iliyopo Dodoma lakini hawakuwa tayari kupokea nyaraka hiyo hisipokuwa waliwapa namba ya simu ambayo wanadai waliipiga bila kupokelewa, hivyo wameeleza kwa juhudi za kumpata zilishindikana.