February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

WAZIRI, NCHEMBA: SERIKARI TAYARI IMEKUSANYA BILION 48 KWENYE TOZO MPYA ZA MIAMALA YA SIMU

Na Anthony Rwekaza

Waziri wa Fedha na Mipango, Mwingulu Nchemba amesema tokea Serikali ianze kutekeleza mpango wa kutoza kodi ya uzalendo kwenye miamala ya simu tayari imekusanya zaidi ya Bilioni 48 kwa muda wa wiki nne.

Akizungumza na umma kupitia waandishi wa habari ametoa mrejesho juu ya hatua mbalimbali kuhusu Kodi za miamala, kati ya mambo hayo amesema tangu makato hayo yaanze kukusanywa kimekusanywa kiasi Cha zaidi ya Bilion 48, na kati ya fedha hizo nyinge tayari Serikali imeshaanza kuzisambaza kwenye shughuli za maendeleo zilizokusudiwa.

“Tangu makato ya tozo yaanze kwa hizi Wiki 4 hadi leo tumekusanya zaidi ya Bilioni 48, zaidi ya Bil 22 tulishapeleka kwenye maeneo ambayo hayana vituo vya afya (zaidi ya vituo 90), leo tumepeleka zaidi ya Bil 15 kwenye eneo hilohilo na kufanya vituo kuwa zaidi ya 150” Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba

Pia Waziri, Nchemba amesema kwenye Bilioni 48 hizo walizokusanya zaidi Bilion saba zipelekwa kujenga madarasa ya wanafunzi huku kiasi kingine kikipelekwa kwenye vituo vya afya, amedai kuwa madarasa hayo yanasaidia watoto wa wananchi.

“Kati ya hizi zaidi ya Tsh.Bil 48 tulizokusanya kwenye makato ya tozo kwa hizi Wiki nne, zaidi ya Bil 7 zimepelekwa kwenye madarasa, mtaona wenyewe tumepeleka fedha zijenge vituo 150 ambavyo vinaokoa maisha yetu, pia madarasa zaidi ya 500, ni Watoto wetu wanasoma” Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba

Aidha Waziri Nchemba amesema kwa upande wa Zanzibar Serikali tayari imekusanya zaidi ya Bilioni 1.66, jambo hilo amelitafsiri kuwa ni mafanikio makubwa kwenye mpango huo waliokusudia kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Lakini kutokana kuwepo mijadala tofauti kuhusu tozo hizo, Waziri Mwigulu Nchemba amewaomba Watanzania na kuwasihi kuwa jambo tozo za miamala lina tija kwao kwa kuwa pesa hizo wanazokatwa ni zakwao bali kupitia kwenye maendeleo.

“Ombi langu moja tu kwa Watanzania wote, ni kwamba hili jambo(tozo ya miamala) ni letu sisi sote wala si la serikali, yaani kila Mtanzania pale ulipo kitu kimoja ambacho ukitambue ni kwamba nchi hii ni yako wewe hapo ulipo, na pesa ni yako wewe hapo ulipo” Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba

Ikumbukwe makato hayo tokea yapitishwe kwenye Bajeti ya Serikali 2021/2022 mijadala mingi ilianza kwenye mitandao ya kijamii hata mitaani na kwenye vyombo vya habari, hali hiyo ilimsukuma Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Samia Suluhu Hassan kuagiza Waziri Mkuu, Waziri Nchemba na watendaji wengine kulitathimini kwa mapana.

Mijadala haikuishia tu mitaani ilipelekea Mwanaharakati Mtetezi wa Haki za Binadamu Charles Odero kufungua kesi kwenye Mahakama kuu Dar es salaam, dhidi ya Waziri wa Fedha na Mipango na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akipinga suala la tozo mpya iliyowekwa kwenye miamala ya simu, tayari kesi hiyo ilianza kusikilizwa Mahakamani tarehe, 12, Augosti 2021.