March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

WAZIRI AZITAKA NGO’s KUMTUMIA RAIS SAMIA UIMARISHWAJI HAKI ZA BINADAMU

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, amezishauri Asasi za Kiraia na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s), kutumia kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kuibua hoja zitakazoimarisha haki za binadamu nchini.

Dk. Ndumbaro ametoa ushauri huo leo Alhamisi, akifungua kikao kazi cha kupitisha mpango mkakati wa Asasi za Kiraia kuhusu utekelezaji wa mapendekezo 167 yaliyokubaliwa na Tanzania kwenye duru la tatu la Mchakato wa Tathimini ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (UPR).

“Taasisi zinazoshughulika na haki za binadamu ni tatu, zikiwemo asasi zisizo za kiserikali ambazo ninyi mpo na tufanye hima hasa kipindi ambacho Tanzania imebahatika kupata Rais mwanamke. Hakuna watu wanajua ukiukwaji wa haki za binadamu kama wanawake na hakuna watu wanajua kutetea haki za binadamu kama mwanamke,” amesema Dk. Ndumbaro.

Dk. Ndumbaro amesema “na mimi nikiangalia wazi utawala wa Awamu ya Sita utafuja moaka 2030 na sisi Watetezi wa Haki za Binadamu tunatakiwa kuutumia sababu Rais Samia ni mwenzetu lazima tutumie fursa hii kuweka hoja zetu ili zisikike sana na tumuunge mkono.”

Katika hatua nyingine, Dk. Ndumbaro amesema Rais Samia ameziagiza asasi za kiraia kufanya utetezi wa haki za binadamu kwa kuzingatia mksingi ya katiba, sheria, mkla na tamaduni za nchi.

“Rais Samia naye amenipa ujumbe niwafikishie kwa siku ya leo, Rais ameagiza niwaleze kwamba Serikali yake itaendelea kushirikiana na sasi zote zinazohusiana na masuala ya haki za binadamu. Ameniagiza niwapongeze kwa kazi nzuri mnayofanya ya kuendelea kusimamia kutetea haki za binadamu,” amesema Dk. Ndumbaro na kuongeza:

“Rais ameniomba muendelee kumsaidia yeye na Serikali katika kulinda na kuendeleza haki za binadamu kwa kuzingatia na kuimarisha amani na utulivu, anasisitiza sana Utanzania wetu sababu haki za binadanu lazima ziwe kwenye katiba na sheria zetu.”