Na Leonard Mapuli.
Polisi nchini Haiti wamewaua washukiwa wanne wa mauaji ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo,Jovenel Moise aliyeuawa jana Jumatano, katika makazi yake binafsi,mjini Port-au-Prince, na mkewe kujeruhiwa..
Taaarifa iliyotolewa kwa vyombo habari inasema, washukiwa wengine wawili wapo kizuzini na bado msako wa kuwasaka wote waliouhusika umepamba moto.
“Watakamatwa au watauawa tu” amenukuliwa mkuu wa Polisi nchini humo, Leon Charles.
Mapema Jumatano watu waliojihami kwa silaha walivamia makazi ya rais na kumuua kwa risasi.Mke wa Moise amehamishiwa katika hospitali moja mjini Florida nchini Marekani ambako anapatiwa matibabu.Taarifa zinaeleza kuwa hali yake inaimarika lakini yupo chini ya uangalizi maalumu.

Katika tukio hilo pia,waliotekeleza mauaji hayo ya rais,waliwateka pia askari polisi wawili na kutokomea nao kusikojulikana,lakini kwa mujibu wa mkuu wa polisi,tayari askari hao wamekombolewa na wako salama.
Akizungumza baada ya mauaji hayo.Waziri Mkuu wa mpito Claude Joseph,amewataka wananchi kuwa watulivu,na ametangaza hali ya hatari nchini humo,ambapo kwa kipindi kisichojulikana,kutakuwa na zuio la mikusanyiko yoyote,pia jeshi la nchi hiyo litafanya kazi zote za kipolisi badala ya polisi wenyewe.
Balozi wa Hait nchini Marekani Bocchit Edmond amewatuhumu wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya wa Marekani kuhusika na mauaji hayo, na kwamba lilifanywa na wabobezi .Akizungumza na shirika la habari la The Reuters,amesema wauaji walijifanya wafanyabiashara wa dawa za kulevya wakati wakiingia katika nyumba ya rais huyo.
Rais wa Marekani Joe Biden ametuma salamau za rambirambi kwa watu wa Haiti,huku waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson akiyaita mauaji hayo kuwa ni ya “kuchukiza” na amewataka raia kuwa watulivu.
Baraza la usalama la umoja wa mataifa linataraji kufanya kikao kuhusu mauaji hayo leo Alhamisi, na limewataka wanasiasa nchini Haiti kutotumia mauji hayo kuleta vurugu ama uchochezi wa aina yeyote.
Rais Moise aliyeingia madarakani mwaka 2017,hivi karibuni amekuwa na wakati mgumu wa kiutawala kufuatia maandamano ya raia kumtaka ajiuzulu.
Bunge la nchi hiyo lilipaswa kumchagua rais mwezi Octoba 2019, lakini mabishano yamekuwa yakifanya uchaguzi uendelee kuahirishwa,na mpaka umauti,Rais Moise alikuwa akitawala kwa amri yake mwenyewe.
Maisha yamekuwa magumu sana katika nchi ya Haiti,yenye wakazi milioni 11,kati yao asilimia 60 wakiishi katika umaskini wa hali ya juu.
Habari Zaidi
ETHIOPIA: AJIUNGA CHUO KIKUU AKIWA NA MIAKA 69
MWANDAAJI MISS RWANDA KUFUNGULIWA MASHITAKA YA UHALIFU WA KINGONO
KENYA: ODINGA AMTEUA MARTHA KARUA KUWA MGOMBEA MWENZA WA URAIS