March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

“WANDISHI WENGI WA HABARI HAWAJIELEWI”-JAJI MAKARAMBA

Na Leonard Mapuli.
Jaji mstaafu wa Mahakama kuu ya Tanzania Robert Makaramba amesema moja kati ya mambo yanayofanya waandishi wengi wa habari wa Tanzania kupata matatizo yanayojirudia mara kwa mara ni kutojitambua.

Jaji Makaramba ameongeza kuwa wandishi wengi wa Habari wapo mstari wa mbele kutafuta matukio yenye faida kwa watu ama makundi mengine lakini hawawezi kujisemea matatizo yao wenyewe ambayo ni mengi pia.

“Ni rahisi kwa wandishi wa habari nchi hii kutafuta ukweli wa taarifa za mauaji ama mateso ya watu wengine kuliko ya kwao”,amesema jaji Makaramba na kurejea taarifa za kukamatwa,kupigwa, kupotea ,na kuuawa kwa baadhi ya wandishi wa habari nchini Tanzania kwa nyakati tofauti.

Kwa mujibu wa wasilisho la Jaji Makaramba katika mafunzo ya Wandishi Habari za mitandao chini ya uratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za binadamu Tanzania (THRDC) na ICNL ni kwamba taarifa nyingi za madhira yanayowakumba wandishi wa Habari hasa barani Afrika hazifiki katika taasisi za kuandaa takwimu kimataifa kwa sababu wandishi wenyewe hawawezi kujiandika.

Kwa mujibu wa Takwimu za UNESCO,jumla ya wandishi wa habari 273 wamefungwa katika magereza mbalimbali duniani na wengine 66 hawajulikani walipo kwa mwaka 2020,huku wandishi wa Habari watano wakiripotiwa kuuawa tangu kuanza kwa mwaka huu 2021 katika sehemu mbalimbali dunia.

Jaji Makaramba ameonesho hofu kubwa kuwa huenda takwimu hizi ni ndogo kwa kuwa wandishi wenyewe hawawezi kuwa mstari wa mbele kutafuta na kutoa taarifa zinazowahusu katika kazi zao za kila siku na kushauri wandishi wa habari kuwa na umoja ili kuwa na sauti moja kubwa inayoweza kusikika duniani.

“Sauti moja ni muhimu katika kujipambania,anzeni ninyi (Wandishi wa habari mitandaoni) kuwa na umoja wenu ili kuwa na taarifa zenu pamoja na kulinda haki zenu”,ameongeza Jaji Makaramba kwa kurejea matatizo mengi yanayowakumba wandishi na kupiganiwa na wadau wengine nje ya tasnia habari.

Kwa muda mrefu wandishi wa habari wamekuwa wakiripoti taarifa za magumu wanayopitia hasa kiusalama na kimaslahi katika mawasilisho pekee pale wanapoalikwa kwenye matukio mbalimbali nchini Tanzania lakini si kwenye vyombo vya habari.