February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MWANZA : WANAWAKE WANAPIGWA,KUBAKWA,KUTUKANWA NA KULAZIMISHWA KUTOA RUSHWA YA NGONO

Na Evarist Mapesa
Imeelezwa kuwa wanawake wanaoenda kufanya biashara katika Mwalo wa Mswahili uliopo jijini Mwanza wanakumbana na matukio ya ukatili wa kimwili, kingono na kisaikolojia.
Akiwasilisha taarifa kwa wadau na Viongozi wa serikali Katibu Chawata Mkoa wa Mwanza Getrudes Pesatatu amesema wanawake wanapigwa, wanabakwa, wanatukanwa, wanatukanwa matusi ya nguoni na wanalazimika kutoa rushwa ya ngono.
“Kuna uzingativu hafifu wa muongozo wa kudhibiti watu wanaoshabikia vitendo vya unyanyasaji. Uwezo mdogo wa kipato miongoni mwa wanawake wachuuzi ,hali hii inashawishi wachuuzi kutoa rushwa ya ngono,” amesema Pesatatu.
Akichangia hoja Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu (SHINYAWATA) Alfredy Kapole amesema watu wenye ulemavu wamekuwa wakishindwa kupata bidhaa kutokana na ugumu wa kushindwa kuingia majini sehemu bidhaa ilipo.
” Baadhi ya akina mama huingia majini kwenda kununua lakini watu wenye ulemavu wakifika pale wao hushindwa kwenda kuchukua mzigo mpaka wabembeleze, kwahiyo mpaka waonewe huruma ndipo aweze kununua samaki, pia watu wenye uarubino wamekuwa wakinyanyapaliwa pindi wakifika eneo hilo kwa ajili ya kununua,” amesema Kapole.
Ameongeza kuwa wafanyabiara na wavuvi wameomba Mwalo wa Mswahili uwe na eneo la kuanikia na kuuzia dagaa ili watu wote waweze kupata huduma hiyo.
Hata hivyo nae Diwani wa kata ya Mkuyuni Donata Yusuph amesema serikali imekuja na mkakati ya kuhakikisha Mwalo huo unakuwa wa kisasa ambapo ujenzi wake utaanza mwezi wa Agosti Mwaka huu na kwenda kutatua changamoto zote zilizopo katika eneo hilo.