February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

WANAWAKE NGORONGORO WAMPA UJUMBE RAIS SAMIA; WAMTAKA AINGILIE KATI MGOGORO NGORONGORO

Na Antony Rwekaza

Baadhi ya Wanawake wanaoishi Ngorongoro wamelalamikia Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA) kwa kuwafanyia vitendo vya ukatili na ukiukwaji wa haki, hali ambayo imekuwa ikiwapelekea kushindwa kufikia dunia yenye usawa kwa watu wote.

Hayo yameelezwa kwenye risala maalumu waliyoiandaa katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani hapo jana Machi 8, 2022 iliyobebwa na kauli mbiu isemayo “USAWA WA JINSIA LEO KWA MAENDELEO YA KESHO”.

Katika Risala hiyo iliyoelekezwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan,wanawake hao wa jamii ya kimaasai wamedai kuwa pamoja na mchango wao kwenye uhifadhi na nia yao ya kulinda maliasili lakini wamedai wamekuwa wakikumbana na changamoto ambazo ni kandamizi kwao kama wanawake.

“Ndugu Mheshimiwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pamoja na mchango wetu wanawake kwenye uhifadhi na nia yetu katika kulinda maliasili, sisi wanawake wa Ngorongoro tunashindwa kufikia dunia yenye Usawa kwa wote kwa sababu ya changamoto mbalimbali za Uhifadhi ambayo ni kandamizi kwetu wanawake wa Ngorongoro” imesema taarifa hiyo.

Kati ya changamoto hizo ambazo wameziorodhesha ni pamoja na kupata vitisho, upokonywaji wa ardhi waliodai kuwa unafanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia kwa kamishna wa uhifadhi NCAA ,Dr. Fredy Manongi, huku wakidai kuwa kumekuwepo na uhasama na Wanawake hao kufanyiwa vitendo vinavyotokana na chuki za wazi kutoka kwa  kwa Mamlaka ya uhifadhi.

Wanawake wa Jamii ya kimasai wakiwa wameshikilia bango la kumuomba Rais Samia kuingilia Kati mgogoro wa Ngorongoro

Pia wamelalamikia kuletewa dawa na chumvi ambazo zimekwisha muda wake na kueleza kuwa wamekuwa wakifanyiwa hivyo kwa malengo maovu ikiwemo kuwafifisha kiuchumi, pamoja na kuchochea udumavu.

“Vitisho na upokonywaji wa ardhi unaofanywa na wizara ya maliasili na utalii kupitia kwa kamishina wa uhifadhi wa NCAA Dr. Fredy Manongi.Uhasama na chuki za wazi kutoka NCAA kwa wenyeji kwa kufanya vitendo tofauti tofauti mfano wamekuwa wakileta Chumvi na dawa zilizokwisha muda wake kwa lengo la kudumaza na kuua uchumi wetu” Risala hiyo imeeleza

Pia Wamesema mchango wa wenyeji hao umekuwa hautambuliki katika suala zima la uhifadhi hasa ikizingatiwa kuwa wamekuwa wanahifadhi Wanyama kwa kipindi cha karne nne zilizopita.

Aidha Wameongeza kuwa Mhifadhi na Menejimenti ya NCAA wameshindwa kutekeleza jukumu la tatu la uanzishwaji wa mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ambalo linawataka kulinda na kuendeleza jamii ya watu waishio ndani ya hifadhi ya Ngorongoro,Lakini pia Wanawake hao wamelalamikia upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya watu kuipitia vyombo vya habari na watu binafsi,wakidai kuwa wamekuwa wakitoa taarifa za uongo na upotoshwaji kuhusu yanayofanyika kwenye hifadhi hiyi.

“Upotoshwaji unaofanywa na kamshina wa uhifadhi kupitia baadhi ya vyombo vya habari na watu binafsi ambao wamekuwa wakihusika kutoa Taarifa za uongo na upotoshwaji juu ya Yale yanayofanyika ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.” imeongeza taarifa hiyo

Aidha wametuma ujumbe kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Jamii ya Wanawake hao wameonesha uwezo mkubwa katika uongozi, pamoja na kusimama na dunia katika harakati kupinga ndoa za utotoni kwa watoto wa kike huku pia wakieleza kuwa wanapinga ukeketaji kwa watoto wa kike ambao umekuwa hauna manufaa kwa afya ya msichana na jamii kiujumla.

Kutokana na kauli mbiu ya ”USAWA WA JINSIA LEO KWA MAENDELEO YA KESHO” ikiwa ni kutambua mchango wa wanawake na wasichana duniani kote katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi, mtazamo wao ni kuwa ili kuendana na mabadiliko ya tabia ya nchi wanasimama kulinda utamaduni wao wa asili ambao wamedai unasaidia kwa kiasi kikubwa kulinda maliasili na kuindeleza utalii kwa maendeleo endelevu kwa manufa ya Taifa.

Wameongeza kuwa wanayo imani kuwa utamaduni weo utalinda mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kuwa umekuwa rafiki kwa Misitu, Vyanzo vya Maji, Wanyama na Mazingira. Lakini wamesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa siku hiyo wanaungana na wanawake wenzao wa Tanzania na Dunia nzima kujenga jamii iliyo na Usawa na yenye kujali haki za binadamu, ambapo wamedai kuwa wanaamini kwamba mwanamke ni kiongozi namba moja kwenye familia na jamii nzima.

Pia wanawake hao wa jamii ya kimaasai wamempongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya tangu aingie madarakani akiwa kama kiongozi mwanamke huku pia wakiwapongeza viongozi wengine wa kike akiwemo Spika wa Bunge Dkt.Tulia Akson.

Vilevile risala hiyo licha ya kuonesha changamoto ambazo wamedai kukabiliana nazo Wanawake hao, wamesema wanayo imani na Rais Samia na wanaamini anaweza kuwafanya kuwa na furaha kwa kuepuka kadhia na uvunjifu wa haki za binadamu kwao kama walivyodai, wamependekeza baadhi ya mambo kwa Rais Samia, na kati ya mambo hayo ni kuwa Wanaomba kusitishwa kwa vitisho na mipango yeyote yenye lengo la kuwaondoa wenyeji katika ardhi yao ya asili ambayo wamekuwepo kwa muda wa Karne zilizopita.

Lakini pia wamependekeza kuwa wanaomba Rais umuondoe Mhifadhi Mkuu aliyepo sasa Dr. Fredy Manongi, ambapo wamedai kuwa ameshindwa kutekeleza jukumu la tatu la kuendeleza wenyeji wanaoishi kwenye mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ambao wapo kisheria, pia wameiomba kwenye risala hiyo Serikali kusitisha mipango ya kutaka kubadilisha sheria ya uendeshaji wa NCAA kwani siyo shirikishi, huku wakimuomba Rais Samia Suluhu kutembelea Wananchi hao wanaoishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kubaini changamoto zinazowakabili hususani kwa Wanawake, ambapo wameomba afanye hivyo wakiamini kuwa anaweza kuwa suluhisho la changamoto hizo.

Itakumbukuwa hivi karibuni kumekuwepo na sintofahamu iliyoibuka kufuatia Serikali kutaka kuondoa baadhi ya kaya zinazoishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro, lakini Sirikali kumekuwepo na kauli kindhani juu ya jambo hilo hali ambayo imeibua mjadala mpana.