February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

WANAWAKE NGORONGORO WAKANUSHA MADAI YA KUPEWA HONGO WAGOME KUONDOKA HIFADHINI

Baadhi  ya Wanawake kutoka Tarafa ya Ngorongoro, wamelaani propaganda zinazoendeshwa na baadhi ya watu mitandaoni, kwamba wanapewa hongo ili wakatae pendekezo la Serikali la kuhama katika hifadhi ya Ngorongoro, kwa ajili ya kusuluhisha mgogoro wa ardhi.

Wito huo umetolewa tarehe 7 Aprili 2022 , mkoani Arusha na Wanawake wa Jamii ya Kifugaji Waishio Tarafa ya Ngorongoro.

“Tunawataka wale wote wanaoendesha Kampeni za kutuchafua na kuchochea mgogoro huu, kuacha mara moja na wahame bila kutuchafua sisi ambao hatuna nia ya kuondoka katika ardhi yetu ya asili,” limesema tamko la wanawake hao.

Wanawake hao wamesema, hakuna mtu na au shirika lolote lisilo la kiserikali (NGO’s), anayewashawishi wakatae pendekezo la Serikali la kuhama katika hifadhi hiyo, kwenda kwenye eneo walilotengewa wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga.

“Kumeibuka kundi dogo sana la watu wanaotumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kwamba, wanahama Ngorongoro na kukashifu wale wanaobaki ikiwemo sisi wanawake wakidai tunazuiwa na kutishwa tusihame Ngorongoro, jambo ambalo siyo kweli,” limesema tamko la wanawake hao.

Tamko hilo limesema “kelele za kwamba kuna NGO zinazotuhonga sukari na fedha, eti tusikubali kuhama Ngorongoro siyo kweli. Bali ni kampeni za chuki na uongo mtupu, unaotungwa na baadhi ya watu wanaoendelea kuhamasisha sisi kutolewa kinguvu katika ardhi ya urithi wetu.”

Wanawake hao wamesema hawana mpango wa kuondoka katika maeneo yao kwa kuwa ni ardhi yao ya asili.

“Sisi wanawake tupo tayari kutoa ushirikiano wowote utakaohitaji katika kumaliza mgogoro huu, Kwa njia sahihi itakayo tumia hekima na busara lakini sio kujadiliana na yeyote namna ya kuhama nakuacha ardhi yetu ya asili,” limesema tamko hilo.