Na Evarist Mapesa
Jamii imeonywa kuachana na tabia za kujisaidia vichakani na badala yake watumie vyoo safi na salama ili kuepuka magonjwa ya matumbo yanayoweza kuyapata.
Wito huo umetolewa ikiwa ni siku moja tangu serikali ya Tanzania kupitia wizara ya afya kutoa takwimu zinazoonesha idadi ya watanzania wanaojisaidia vichakani kupungua kutoka asilimia 5.7 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 1.4 December 2021.
Daktari kutoka Shirika la WACAP lililopo jijini Mwanza Ayoub Msalilwa, amesema kuwa kujisaidia kwa vichakani kunaweza kuleta madhara hata kwa watu wengine kuugua magonjwa ya matumbo.
“Baadhi ya watu wameendelea kubaki katika kundi la watu wasiotumia vyoo na wanaweza kusababisha madhara kwa watu wengine kwa mfano mtu atakapokuwa ameenda kujisaidia nje ya choo yaani kwenye kichaka au majani,kile choo chake kama kina vijimelea vya wadudu,basi hivyo vimelea vinaweza kusababisha madhara kwa watu wengine”,alisema Msalilwa.
“Tafiti zinaonesha kuwa vimelea Zaidi ya 106 vinaweza kubebwa ndani ya kile choo au mkojo wa mtu yule ambaye hajatumia choo iwe ni kujisaidia katika maeneo ya vichakani au ya wazi,vijimelea hivyo vinaweza kusababisha magonjwa ya kuambukiza kama vile magonjwa ya matumbo ikiwa ni pamoja na typhoid, kuhara, kichocho”,aliongeza Msalilwa.
Kwa sasa mashirika mbalimbali kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania yamekuwa yakianzisha kampaini mbalimbali ya kuhamasisha ujenzi wa vyoo bora ili kusaidia kuepuka maradhi ikiwemo ya mlipuko kama kipindupindu.
Kwa mujibu wa Waziri wa afya nchini Tanzania Ummy Mwalimu,wamefikia Zaidi ya asilimia 72 za kaya za kitanzania zenye vyoo bora.
Licha ya mafanikio hayo lakini watu wanaojisaidia katika maeneo ya vichakani wanachagizwa kwa kiasi Fulani na kutokuwa na vyoo safi na salama katika maeneo yao,jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.
“Inaweza kusababisha magonjwa ya virusi mbalimbali na hata pia kusababisha magonjwa ya macho kama trachoma, endapo nzi atatua katika kile kinyesi na baadae kusambaza vile vijimelea vya wadudu na kuweza kuwapatia watu wengine”,alisema Msalilwa.
“Magonjwa kama vile kichocho hutokea iwapo mayai yakibebwa kutoka katika kile kinyesi,na mvua zianpokuwa zimenyesha mabaki ya kile choo yatakapokwenda kwenye maji,yanaweza kusababisha magonjwa kama kichocho”,aliongeza Msalilwa.
Malengo ya serikali ya Tanzania ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2025 kila kaya ziwe na vyoo bora ili kusaidia kupunguza magonjwa yakiwemo ya kuhara pindi milipuko ya aina hiyo inapotokea.
Habari Zaidi
UFAFANUZI WA KISHERIA KUHUSU ARDHI YA LOLIONDO
“NILIGOMBEA URAIS CHADEMA KWA BAHATI MBAYA”DKT SLAA
MONGELA AIBUA TENA SAKATA LA MGOGORO WA ARDHI LOLIONDO