February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

“WANANCHI MSIDANGANYWE KUHUSU CHANJO YA UVIKO-19”-IGP SIRRO

IGP Simon Sirro-Mkuu wa Polisi.(Picha:Jeshi la Polisi).

 Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro, amewataka Wananchi na Watanzania kwa ujumla wasidanganywe na watu wa chache au kikundi cha watu wanaowahamasisha kwa njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii kuto kuchanjwa chanjo ya Uviko-19 ambapo zoezi la uchanjwaji wa chanjo hiyo lilizinduliwa jana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Ikulu Dar es salaam.

Kamanda Sirro ni miongoni mwa waliopatiwa chanjo ya Corona katika siku ya uzinduzi wa chanjo hiyo.

“Nilikubali kuchanjwa kwa sababu Mheshimishiwa Rais na Amiri Jeshi  Mkuu ameonesha njia” amesema Sirro na kuipa kongole wizara ya afya kwa kutimiza majukumu yake na kwamba amekuwa na imani na wizara hiyo tangu akiwa mdogo.

“Nawaomba watanzania waamini maelezo tunayopewa na waziri wetu wa Afya”,ameongeza Sirro wakati akizungumza katika kwenye hafla ya kuandikishiana hati ya makubaliano kati ya Shirika la Bima la Taifa na Jeshi la Polisi kupitia Shirika lake la Uzalishajimali ambapo shirika hilo litaweza kuwa wakala wa bima za maisha na ajali kwa watendaji wa Jeshi hilo la Polisi pamoja na familia zao huku Jeshi hilo likitoa ahadi ya kutanua wigo ili bima hiyo ya maisha iweze kuwafikia hata waendesha pikipiki maarufu bodaboda.

Aidha kamanda Sirro ameonesha kusikitishwa na watu wanaopotosha ukweli kuhusu chanjo,kwa kuwaaminisha watu vitu vya uongo ili hali wao si wanataaluma ya sayansi wala tiba nakuwataka watanzania kusikiliza wataalamu na si wanaoendekeza porojo kwenye taaluma isiyowahusu.

“Ni kama vile sisi wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi,na hasa jeshi la polisi tuliopewa jukumu la suala la ulinzina usalama wa nchi,halafu ukakuta mtu anazungumzia suala la polisi utadhani yeye ni polisi ofisa,na wakati siyo,ni jambo la aibu sana”,amesema Kamanda Sirro na kuamba mambo yote ya Afya iachiwe wizara husika iliyopea majukumu hayo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Taifa Dkt. Elirehema Joshua amesema kuwa licha ya kuwepo kwa idadi ndogo ya wananchi wenye ufahamu wa masuala ya bima za maisha, ajali na mali ambapo kupitia shirika la uzalishajimali la Jeshi la Polisi litakuwa na wigo mpana wa kuwafikia wananchi pamoja na kuwezesha Watanzania wote kupata elimu na huduma zote za bima zinazopatikana nchini.