February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

WANANCHI KIGOMA WANYWA MAJI YA MTARONI,WAILILIA SERIKALI

Wakazi wa Kijiji cha Mkwanga-Kigoma wakichota maji Mtaroni kwa matumizi ya nyumbani.

Na Mwandishi Wetu-Kigoma

Wakazi wa kijiji cha Mkwanga halmashauri ya wilaya ya Kigoma, wanakabiliwa na hatari za kiafya kutokana na kulazimika kutumia maji machafu yanayopita katika mtaro unaopeleka maji katika mto Kaseke wilayani humo,na hivyo wameiomba serikali kuwasaidia kutatua changamoto hiyo.

Wakielezea kuhusiana na maji wanayotumia, wakazi wa kijiji hicho wamesema licha ya kuona takataka kwenye maji hayo lakini bado wamekuwa wakilazimika kuyatumia tu kutokana na kutokuwa na mbadala.

Maji yanayotumiwa na wakazi wa kijiji cha Mkwanga-Picha na Pendo Thomas

Amina Bahita ni mkazi wa kijiji cha Mkwanga ameeleza kuwa hali hiyo imekuwa ikiwaathiri kiafya ikiwemo kuwa sababishia kuugua matumbo na kichocho

“Haya maji hayana usalama kabisa yana safirisha takataka kutoka maeneo mengine halafu tunachangia na mifugo kama ng’ombe na mbwa hii sio sawa “Amesema Bahita

Naye mwenyekiti wa kijiji cha Mkwanga Paulo Ntibalio ameeleza kero hiyo inapaswa kupatiwa ufumbuzi wa haraka hatua itakayo saidia usalama wa wananchi katika eneo hilo na kuepukana na madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi ya maji yasiyo salama.

Mkazi wa Mkwanga akiwa amebeba maji yanayolalamikiwa-Picha na Pendo Thomas

Alieleza wamekuwa wakijitahidi kuzuia shughuli za kibinadamu zinazo chafua mto huo ikiwemo viwanda vya Mawese vinavyo mwaga taka katika mto huo lakini wameshindwa kudhibiti uchafuzi huo.

Kituo hiki kimemtafuta meneja wa RUWASA wilaya ya Kigoma Respicious Mombeki kufahamu juu ya suala hilo ambapo ameeleza eneo hilo lilipaswa wananchi waanze kutumia maji safi na salama tangu mwezi wa tano mwaka jana

Alieleza kinacho kwamisha hadi sasa ni mkandarasi anae tekeleza mradi huo Serengeti limited Company kushindwa kukamilisha kwa wakati huku akiwa ameshaongezewa muda kwa awamu tatu bila mafanikio.

“Inawezekana mkandarasi hana uwezo au ana miradi mingi sisi kama RUWASA tunapambana kuhakikisha ananyang’anywa huo mradi ili tuumalizie na wananchi wapate maji” Amesema Mombeki

Alieleza kinacho sababisha washindwe kuchukua hatua za haraka dhidi ya mkandarasi huyo ni kuwa aliingia mkataba na mfadhili wa mradi huo shirika la ENABEL na sio wao .