February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

WANAFUNZI 293 SHULE YA BILIONEA LAIZER : WALIMU WAWILI TU

Bilionea Saniniu Laizer ameiomba Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuongeza walimu katika shule ya Saniniu Laizer aliyoijenga huko Naepo Kata ya Naisinyai  wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Akizungumza na waandishi wa Habari Bilionea Laizer ameonyesha kufurahishwa na muitikio wa jamii ya kimaasai wa kupeleka Watoto shule na kupelekea idaidi ya Watoto katika shule hiyo kufikia 293 mpaka sasa.

Shule hiyo inayofundisha kwa lugha ya Kingereza inatajwa kuwa na walimu wawili tu jambo linalopelekea walimu hao kushindwa kuwafikia wanafunzi wote ipasavyo ambao kwa uwiano ni 1: 147 yaani mwalimu mmoja anatakiwa kufundisha wanafunzi 147, kinyume na taratibu za wizara ya Elimu unaomtaka mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi wasiozidi 46.

Changamoto tuliyonayo kwa sasa ni uhaba wa walimu, walimu waliopo ni wawili tu na wanafunzi waliopo ni 293, hivyo tunaiomba Serikali yetu kuangalia namna ya kutusaidia kuongeza walimu ili kufundisha watoto hawa.

Billionea Laizer

Pamoja na changamoto ya waalimu Billionea Laizer ameiomba serikali kusaidia katika ujenzi wa Bweni litakalowezesha wanafunzi kupata malazi katika shule hiyo.

Billionea Laizer ameeleza kuwa uwepo wa shule hiyo umefungua wigo kwa watu wazima wa jamii ya Kimasai kupata elimu ya watuwazima kwa muda wa masaa matatu kwa siku.

Tumeona ni vema kutoa elimu kwa watu wazima ambao huko nyuma walikosa elimu lakini kwa kutambua umuhimu wake na baada ya kujenga shule hii wameamua kuja kuifuata hapa.”

Billionea Laizer

Mpaka sasa shule ya saniniu lazier ina wanafunzi 293 ambao wote wanajifunza kwa kutumia lugha ya Kiswahili na kingereza, jambo ambalo hapo awali lilikuwa gumu kutokana na utumiaji wa lugha ya asili ya kabila hilo.