February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

WANACHAMA THRDC WAKABIDHI MSAADA WA MAGODORO 100 KWA VYUO VYA MAFUNZO (MAGEREZA) VISIWANI ZANZIBAR

Na Loveness Muhagazi

Mapema leo Septemba 17, 2021 Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Wanachama wa Mtandao kanda ya Zanzibar wamekabidhi msaada wa Magodoro 100 kwa wafungwa walio katika vyuo cha mafunzo (Magereza) visiwani humo, msaada huo ni mchango wa wanachama wa THRDC Tanzania walioenea Tanzania nzima, Bara na Visiwani.

Akizungumza wakati wa kukabidhi Msaada huo Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini Tanzania Onesmo Olengurumwa ameutambulisha mtandao na kueleza kuwa mtandao unafanya kazi kuhakikisha kuwa unatetea haki za binadamu, lakini Zaidi wanachama wa mtandao huo Tanzania Bara na visiwani wamekuwa wakifanya kazi kuhakikisha makundi yote yanapata haki zao bila kujali maeneo walipo.

“Tumaahidi Kuwa Mtandao utaendelea kuhakikisha unafanya kazi kwa ukaribu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, punde Mtandao umwkusudia kuw ana tawi dogo visiwani humo Ili kuendelea kukuza mahusiano baina ya wnaachama wa Mtandao bara na visiwani Pamoja na Serikali zake.

Olengurumwa ameeleza kuwa Mchango huo wa Magodoro 100 utasaidia kuwatengenezea wanafunzi walio katika vyuo vya mafunzo mazingira salama ya kuishi wakati wa mafunzo kwani kwa hali ya wanafunzi (wafungwa) pindi wawapo ndani ni vigumu kujipatia mahitaji muhimu kama hayo lakini wadau wanapojitokeza na kuonyesha kujali kwa kuchangia michango mbali mbali, huwasaidia wanafunzi hao kupata haki saw ana binadamu wengine.

Mratibu amepongeza jina linalotumika kwa magereza visiwani humo linalotambua magereza kama “VYUO VYA MAFUNZO” kwani jina hilo linatengeneza saikolojia ya wafungwa na kuona kuwa wapo katika eneo hilo kwa ajili ya kujifunza, kubadilika na kurudi kuwa watu wema tena kwenye jamii.

“Binadamu huwa tunakosea lakini kuna nafasi ya kujirekebisha kwa hiyo tunaamini, Kisaikolojia unapolipa gereza jina hilo inamaanisha unamuandaa mfungwa (Mwanafunzi) Kisaikolojia kuona kwamba hajaja hapa kufungwa bali amekuja kujifunza namna gani anaweza kuishi na wana jamii wengine bila kufanya makosa, lakini pia ni jambo ambalo tungependa na kule bara baadae ikiwezekana majina ya taasisi zetu tuweze kuyaboresha ikiwezekana kwa kusikia tu jina inaweza kumsaidia na kumjenga mtu” Onesmo Olengurumwa

Naye Mrajisi wa NGO visiwani Zanzibar Ahmed Khalid Abdulla Ametoa shukrani za dhati kwa mtandao na wanachama wake kwa kuweza kufanikisha upatikanaji wa magodoro hayo ambayo yatatumika kuboresha mazingira ya vyuo vya mafunzo.

“Niwashukuru wanachama wa THRDC kwa kuguswa na jambo hili, na kuweza kukabidhi vifaa hivi ambavyo vina manufaa sana kwa matumizi ya magereza haya, naendelea kuwakaribisha wengine wenye uwezo wa kutoa chochote wakaribie ili kuweza kufanikisha upatikanaji wa vifaa muhimu kwa amhitaji ya chou hiki” Ahmed Khalid Mrajisi wa NGO Zanzibar

Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo kwa niaba wa Waziri wa nchi Afisi ya Rais, Tawala za mikoa na Idara maalum za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Kamishina wa vyuo vya Mafunzo Zanzibar Khamis Bakar Khamis amezipongeza Asasi za Kiraia kwa kujitokeza kutoa msaada huo kwani wamejitokeza wakati sahihi ambapo vyuo hivyo vimehitaji msaada.

“Msaada huu umelenga kwenye kuleta utu wa mtu, Yule mwanafunzi kwa maana ya mfungwa yupo ndani, uhuru wake kidogo umepungua, hana uwezo wa kutoka madukani kwenda kununua godoro lakini analihitaji atalipata wapi msaada huu umekuja kwa lengo la kuonyesha utu, ubinadamu, lakini pia heshima, kwa hiyo tunashukuru sana, kuna msemo wa utani unasema gereza ni ‘second street’ hatuombei kwenda kule lakini hatukatai unaweza ikatokea siku moja ukajikuta umeteleza ukajikuta huko , tusiwe na tabia ya kusema wakome, kama tuna chochote cha kuweza kusaidia tusaidie ni kwa sababu ya utu tu” Kamishina wa vyuo vya Mafunzo Zanzibar Khamis Bakar Khamis

Tukio Hilo la ukabidhiwaji wa magodoro limehudhuriwa na wanachama wa Mtandao THRDC Tawi la Zanzibar kutoka visiwa vya Unguja na Pemba, wengine ni Mratibu wa THRDC Zanzibar Bw. Abdallah Abied kutoka Shirika la ZAFAYCO, Mkurugenzi wa ANGOZA na mjumbe wa bodi ya THRDC Mzee Hassan Khamis, Mussa Kombo Mratibu wa THRDC Kanda ya Pemba, wanadishi wa Habari na Maaskari wa Vyuo vya Mafunzo akiwemo naibu Kamishna wa chuo Cha Mafunzo visiwani Zanzibar.

Mwisho, wadau, Mashirika na wanachama wa mtandao THRDC wametakiwa kuendelea kushirikiana na serikali kutatua changamoto mbali mbali za wananchi zikiwemo maeneo ya haki za binadamu, huduma mbali mbali za kijamii, Serikali pia iendelee kushirikisha mashirika na wadau kuendelea kushiriki katika michakato mbali mbali katika maeneo ambayo serikali haiwezi kufika watetezi wa haki za binadamu wasaidie kufanikisha maendeleo Zaidi kwa jamii.

MWISHO