February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

WAMILIKI WA MABASI ,DALADALA WAPENDEKEZA NAULI ZIONGEZWE

Wadau  wa usafirishaji nchini Tanzania, wamependekeza nauli za mabasi yaendayo mikoani na ruti fupi zipande, ili kukabiliana na athari za ongezeko wa gharama za uzalishaji, zilizosababishwa na kupanda kwa bei  ya mafuta.

Mapendekezo hayo yametolewa leo Jumatano, katika kikao cha wadau cha kujadili bei za nauli kilichoitishwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA).

Katibu wa Umoja wa Usafirishaji Abiria Mkoa wa Dar es Dalaam (UWADAR), Selemani Kimomwe, amesema umoja huo unapendekeza bei ya nauli ipande kwa Sh. 400.

“Kwa maoni yetu UWADAR tunaomba ongezeko la Sh. 400 la nauli kutoka kila nauli, mfano nauli ya Sh. 500 iongezeke kutoka Sh. 500 kuja Sh. 900, kwa ruti tu. Tunaamini maombi yetu yatafanyiwa kazi,” amesema Kimomwe.

Naye Mwakilishi wa Kampuni ya Usafirishaji ya Happy Nation, Ally Siddy Urasa, amesema wanapendekeza nauli ipande hadi kufikia Sh. 72 kwa kilomita, na kwamba bei ya kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza iwe Sh  83,861.

Kwa upande wake,  Mkurugenzi wa Kampuni ya ABC Uper Class, Severine Ngallo, amesema wanapendekeza nauli ipande kutoka Sh. 53.22 kwa kilomita moja, hadi kufikia Sh. 86.31.

Hata hivyo,mapendekezo hayo yalipingwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri LATRA, Leo Ngowi, ambaye ametaka  mapendekezo yaliyotolewa na  UWADAR, ya ongezeko la nauli la Sh. 400 akitaka yapitiwe upya kwa kuwa vigezo vilivyotumika kuipanga kutokuwa na uhalisia.

“Baraza limeazimia mamlaka isipokee maombi (ongezeko la Sh. 400 nauli ya daladala Dar es Salaam), mpaka yafanyiwe maboresho, wayarudishe tena ili tuangalie gharama zinazotozwa. Nauli za sasa ziendelee kutumika,” amesema Ngowi.

Pia, Ngowi, ameshauri  nauli za mabasi yaendayo mikoani zisipandishwe badala yake vitumike viwango vya nauli vilivyopangwa 2013, kwa sababu wahusika hawajafikia viwango hivyo.

“Nauli ya Mwanza ni Sh. 61,400,  lakini nauli inayotozwa 45,000 mpaka 50,000,  kuna tofauti ya Sh. 6,400 ambayo msafirishaji hajafikia viwango. Kigoma nauli 78,400, nauli inayotozwa ni kati ya 50,000 mpaka 60,000 ikiwa tofauti ya 18,400. Kwa hali iliyopo sasa pamoja na kampuni bado hawajaanza kutoza nauli zilizioanishwa na mamlaka mpaka leo hii,” amesema Ngowi na kuongeza:

“Maombi kwa mamlaka tumeleta matatu, kwanza isipokee maombi haya badala yake watoa huduma waelekezwe kutumia nauli zilizohimili  ambazo hazinatumiwa.Kwa mikoa nauli zilizoidhinishwa bado haijzajaongezeka,  zishushwe kuendana na nauli zilizopita kama Kigoma, Bukoba na hili ni ombi letu kwa malamka .

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji LATRA Gillard Ngewe, amesema mamlaka hiyo itaendelea kuchukua maoni juu viwango vipya vya bei, hadi tarehe 20 Aprili 2022, kwa njia ya maandishi, kisha watatoa bei elekezi.