December 4, 2022

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

WALIOUAWA MAPIGANO YA ISRAEL NA PALESTINA WAFIKIA 225

Na Leonard Mapuli.

Raia nchini Palestina wameungana  na kufanya  maandamano kupinga mashambulio ya anga yanayoendelea katika ukanda wa Gaza chini majeshi ya Israel.

Mapema hii leo (Jumanne) Rais wa Marekani Joe Bideni amempigia simu Waziri Mkuu wa Israel, Benjamini Natanyahu na kumsihi kukomesha mapigano kati ya vikosi vya majeshi vya Israel na wapiganaji wa Hamas ,ikiwa ni simu yake ya tatu kuwasiliana na Netanyahu  tangu kuzuka kwa mzozo huo Mei 10 mwaka huu.

Wakati huo huo maoni yaliyotolewa kwa njia ya video katika mkutano wa mawaziri 27 wa mambo ya kigeni toka nchi 27 za umoja wa Ulaya,Ujerumani imeitaka Israel kuacha mashambulizi mara moja na kwamba ipo tayari kutoa misaada ya kibinadamu kwa Palestina.

“Kusitisha mzozo inapaswa kuwa kipaumbele chetu”,amesema Heiko Maas,waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani akiahidi kupeleka kiasi cha Euro milioni 40 kugharamia misaada ya kibinadamu katika eneo la Gaza.

Mamia ya waandamanaji kutoka Palestina wameandama hadi kwenye geti la mji wa Damascus linalotenganisha mji huo na jiji kongwe la Jerusalem.katika maandamano hayo,watu watatu wamekamatwa na polisi walitumia pia risasi za mpira,magrunedi,na maji ya kuwasha kuwatawanya waandamanaji hao.

Maandamano mengine yameshuhudiwa katika mji wa Bethlehem ambapo pia polisi waliwatawanya kwa maji ya kuwasha Wapalestina waliokuwa wakiandamana  kupinga mashambulizi yanayofanywa na Israel.Katika maandamano hayo,watu saba wamejeruhiwa.

Mzozo wa Israel na Gaza umeingia juma la pili ambapo hadi sasa Wapalestina 213 miongoni mwao wakiwa watoto 61 wameuawa huko Gaza na wengine 1500 wakibaki majeruhi,huku watu wengine 12 miongoni mwao watoto wakiwa wawili wameuawa nchini Israel na wengine 300 wakiuguza majeraha.