February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

WALIOBAMBIKWA SILAHA LOLIONDO WAACHIWA HURU

Na Mwandishi Wetu.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha,leo Septemba 20,imewaachia huru Lein Mbirika na mwenzie Muresi Mbeyo, wote wakazi wa Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, waliokuwa wakikabiliwa na kosa la kukutwa na silaha kinyume na sheria.

Lein Mbirika,alikamatwa na kikosi kazi kilichokuwa kimeundwa na serikali 2017 kwa ajili ya kusaka silaha zilizokuwa zikitumika kutekeleza matukio ya ujangili wilayani Ngorongoro ,ambapo baadhi ya watu wanadai kukamatwa na kikosi kazi hicho, akiwemo Lein na kupelekwa porini kwa nguvu kutafuta silaha zilizokuwa zimefichwa kwa kuchimbiwa chini ama kwenye vichaka ,na zilipopatikana wanadai walilazimishwa kukiri kuwa ni za kwao.

Lain anadai baada kukamatwa na kikosi kazi,aliambiwa akiri kumiliki silaha kwa vitisho vya askari,ambapo alilazimika kufanya hivyo na akawekwa rumande kwa karibu miaka mitatu kabla ya kuachiwa huru mwaka 2019,na kukamatwa tena muda mchache baada ya kuachiwa na ndipo alipounganishwa na mtuhumiwa Muresi Mbeyo na kuwekwa tena rumande jijini Arusha.

Kubambikiwa silaha na askari kwa wakazi waishio Loliondo na maeneo mengine yanayopakana na Mamlaka ya Hifadhi  ya Ngorongoro inatajwa kama  moja ya kero waliyoipata wakazi wa eneo hilo katika opareshesheni zilizoendeshwa kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu,chini ya waziri mwenye dhamana (Maliasili na Utalii) Hamis Kigwangalla.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania,Onesmo Olengurumwa aliwasaidia kwenye masuala ya kisheria akisaidiana na Wakili Symon  Mbwambo na wenzake kuhakikisha watuhumiwa hao wanawakilishwa vyema mahakakamani wakati wote ili wapate haki yao, ambapo leo,wameachiwa huru baada ya mahakama kuthibitisha kuwa hawakuwa wakimiliki silaha kwa  shughuli yoyote licha ya kusoteshwa rumande muda mrefu,na pia kuingizwa gharama za “Nenda Rudi” kutoka Loliondo hadi Arusha kila kesi yao ilipotajwa.

Baada ya kuachiwa huru,wakazi hao wamemshukuru Onesmo Olengurumwa na kumuomba  aendelee na moyo wa kusaidia wananchi wanaopata shida za kisheria Wilayani Ngorongoro na kukosa usaidizi wa kisheria na kesi nyingi kuchukua muda mrefu huku zikiendeshwa nje ya wilaya hiyo.