March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

WAFUGAJI NGORONGORO WALIA NA SERIKALI,WAOMBA ISITISHE ZOEZI LA KUWAONDOA HIFADHINI

Viongozi wa jamii ya kifugaji wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wameitaka serikali kumuondoa madarakani mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wakidai hazingatii maslahi ya jamii na kuongozwa na siasa chafu pamoja na ukandamizaji wa haki za wafugaji mkoani humo.

Kauli hiyo imetolewa mnamo Agosti, 27 mwaka huu na kutiliwa saini na wenyeviti wa vijiji 18 wilayani humo kwa niaba ya jamii ya wafugaji.

“Serikali isitishe mpango wa Wizara ya maliasili na utalii wa kuhamisha wafugaji kutoka Ngorongoro kwani ni ardhi yao ya urithi na hawajaiharibu kwa karne nyingi na hawataiharibu,”imeeleza taarifa hiyo.

Aidha wameeleza kuwa kutokana na serikali kukataza kilimo katika ardhi ya Ngorongoro imepelekea baada la njaa na utapiamlo katika eneo hilo ambalo wamelitaja kuwa ndilo linaloongoza kwa utalii na kuiomba serikali kuchukua hatua kwa kushirikiana na jamii hiyo ya kifugaji kutatua baa la njaa.

“Mifugo imepigwa marufuku katika maeneo mengi mazuri kwa malisho,hii imesababisha ufukara uliopindukia katika tarafa ya Ngorongoro.Kudumaza maendeleo kwa kudhibiti ujenzi,biashara na kukataza kilimo,”imeongeza taarifa hiyo.

Pia viongozi hao wametaka kuanzishwa kwa Tume ya kimahakama ili kuchunguza dhuluma na ukatili unaofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Hifadhi ya Ngorongoro kwa Zaidi ya miongo sita ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

“Serikali ianzishe baraza la wafugaji ambalo lilikuwa ni jukwaa pekee la kutetea haki za wafugaji wanaoishi katika vijiji 25 vilivyopo katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro”

Kwa upande mwingine wameiomba serikali iridhie kuanzisha mjadala shirikishi wa hatma ya hifadhi hiyo, mjadala ambao utaangalia kwa undani changamoto za kimazingira,watu na utalii katika eneo hilo.

Pia wameitaka serikali na Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro kuachana na mpango wa kuwahamisha wafugaji kutoka katika eneo hilo kwa madai kuwa wafugaji hao wamebakiwa na ekari 8,292 baada ya mwaka 1958 kutoa ekari Zaidi ya 14,000 ili kupisha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“wanyamapori wamekuwa wakiua ama  kujeruhi wafugaji na kuharibu mali zao.Mfano hivi karibuni Simba waliua watoto watatu na kumjeruhi mmoja kijiji cha Ngoile,”