February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

WADAU WAICHAMBUA KAULI YA WARIOBA KUHUSU WIZI WA KURA

Siku moja baada ya kauli aliyoitoa Waziri mkuu na Jaji mstaafu wa serikali ya Tanzania Joseph Sinde Warioba kukosoa mapendekezo ya mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya kuanza baada ya uchaguzi mkuu wa 2025, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamesema kuwa hoja hizo zina msingi,zinapaswa kuchukuliwa hatua na mamlaka husika.

Hatua hiyo inakuja wakati huu ambapo chama kikuu cha upinzani, Chadema kuweka wazi ajenda yao kuwa ni upatikanaji wa katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025 kama alivyobainisha mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Kwa sasa kumekuwa na maoni mseto miongoni mwa vyama vya upinzani ambavyo baadhi wamekuwa wakiamini kuwa mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya utachukua muda mrefu hadi kupatikana kwake na kupendekeza kuanza kwa tume huru ya uchaguzi kuelekea kwenye katiba mpya.

Akizungumza katika mkutano wa kitaifa wa haki,amani na maridhiano,Jaji Warioba akishangaa alikosoa mapendekezo ya upatikanaji wa katiba mpya.

Wananchi walikuwa na mambo muhimu kabisa,moja ilikuwa suala la haki za binadamu,mnangoja hilo linangojea mchakato uje baada ya uchaguzi?”,aliuliza Warioba.

Kufuatia kauli hiyo iliyoibua maoni mbalimbali ya watu hususani katika mitandao ya kijamii kama Twitter, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Tanzania wanasema kuwa katiba katika nchi ni muhimu.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa aliyepo jijini Mwanza, Hamdun Malseli anasema kuwa hoja ya katiba mpya aliyoiibua Jaji Warioba inapaswa kuangaliwa kwa kina.

“Bila kung’ata maneno katiba ni muhimu, kwamba inaanzia wapi ndilo jambo la msingi la kujiuliza?” alisema Malseli.

Akizungumzia suala hilo mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Richard Feroozi amesema Jaji Warioba ametoa kauli hiyo kutokana na kuwa ni miongoni mwa watu aliokuwepo kwenye mchakato kupata katiba mpya ambao haukufikiwa mwisho.

“Jaji Warioba anazungumza kitu anachokifahamu, pili ni mtu ambaye amekaa kwenye serikali kwa mda mrefu kwa sababu amewai kuwa waziri mkuu kwahiyo anajua mapungufu ya katiba yako wapi? lakini tatu ni mwanasheria, kwahiyo ni wazi katiba mpya unatakiwa uwepo kabla hata ya uchaguzi” amesema Feroozi.

March 21 mwaka huu kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa walipendekeza mchakato wa kupata katiba mpya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.