February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

WADAU MWANZA WAJADILI VITENDO VYA UKATILI KATIKA MAENEO YA BIASHARA

Na Evarist Mapesa

Wadau na viongozi kutoka Taasisi mbalimbali Jijini Mwanza leo wamekutana kujadiliana njia za kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia ambao umekuwa katika maeneo ya kibiashara.

Katika kikao hicho cha wadau wa maendeleo Mwanza (AZAKI), watumishi, na viongozi wa Serikali kilicho andaliwa na Shirika la kutetea Haki za Watoto Wafanyakazi wa Nyumbani (Wotesawa), kujadili changamoto, fursa na vikwazo vya maendeleo ya vijana, wanawake,na watu wenye ulemavu vinavyopatikana katika Mwalo wa Mswahili uliopo Mkuyuni Jijini Mwanza kaskazini Magharibi mwa Tanzania.

Kwa pamoja wadau hao Wamekubaliana kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na Ulinzi shirikishi , elimu inayohusiana na ukatili wa kijinsia kwa wanawake, watoto na watu wenye ulemavu.

Programu Meneja wa Shirika la Wotesawa Elisha David, alisema wamekuwa wakiendelea kufuatilia changamoto mbalimbali ambazo zinalikumba soko hilo ikiwa ni pamoja na ufinyu wa Mwalo, changamoto za kimazingira hususani wamama wanaolazimika kuingia kwenye maji yenye kina kirefu, usafi wa mazingira, ukatili na unyanyasaji wa wanawake, ajila kwa watoto pamoja na unyanyasaji.

Hata hivyo amesema wamekubaliana kupanua Mwalo huo, kuboresha kamati za Mtakua ambazo zinajikita kutoa elimu kwa jamii juu ya ukatili, jeshi la polisi kuweka Ulinzi shirikishi na kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya ukatili wa kijinsia kwa jamii.

Kikao hiki ni utekelezaji wa Taarifa iliyotolewa na kamati ya Mtakua kwenye kikao cha wadau wa maendeleo juu ya Mwalo wa Mswahili iliyofanyika ndani ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa lengo la kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia ambapo walibaini vitendo hivyo katika soko hilo.

Shirika la Wote Sawa ni miongoni mwa mashirika wanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania.