February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

WACHINA WA KIWANDA CHA YI SEN MAFINGA WAPUUZA AGIZO LA RC IRINGA,WAENDELEA KUNYANYASA WAFANYAKAZI.

Lin Xin Zong-Msimamizi wa Kiwanda cha YI SEN

Na Leonard Mapuli.

Wawekezaji wa kiwanda cha uchakataji bidhaa zitokanazo na misitu cha YI SEN  International Investment Co. Ltd, kinachofanya uzalishaji wake katika eneo la Luganga Halmashauri ya Mafinga,wilayani Mufindi Mkoani Iringa,wameonekana kutofanyia kazi agizo lililotolewa na Mkuu wa Mkoa huo, Queen Sendiga aliyeagiza kutatuliwa kwa changamoto mbalimbali za Wafanyakazi ikiwemo uboreshaji maslahi,kuacha unyanyasaji,pamoja na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.

Mwanzoni mwa mwezi Septemba,Mkuu huyo wa Mkoa akiambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo,alifika kiwandani hapo kufuatia taarifa  juu ya ukiukwaji mkubwa wa sheria na haki za wafanyakazi, ambapo aliagiza kiwanda hicho kutatua kero zote za wafanyakazi ndani ya siku 30.

Watetezi media imefika katika kiwanda hicho zikiwa zimepita takribani siku ishirini tangu agizo la Mkuu huyo wa mkoa litolewe, na kushuhudia hali ikiwa ni vilevile bila hata changamoto moja kutatuliwa.

Queen Sendiga-Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Baadhi ya wafanyakazi waliiambia Watetezi mediakuwa ,hakuna kilichobadilika na zaidi kumeongezeka unyanyasaji mpya kwa wafanyakazi, unaofanywa na viongozi wazawa wanaotoa adhabu mbalimbali ikiwemo kusimamisha ama kufukuza kazi wale wote wanaolalamikia ukiukwaji wa haki za wafanyakazi.

“Kwa sasa,viongozi wanaotusimamia sisi (Wafanyakazi),ndio wanaotunyanyasa hata kuliko wachina,ukiongea kitu chochote cha halali,wanakuadhibu kwa sababu umeongea,lakini ni Watanzania kama sisi’’,amesema Jackson Kavimbi,ambae ni mfanyakazi wa kiwanda hicho na kwenda mbali zaidi kuwatuhumu mabosi wazawa kujineemesha kwa mishahara minono inayotokana na kuwanyonya wafanyakazi wa chini.

Katika hatua nyingine ya kushangaza,Watetezi media ilishuhudia ulipwaji wa mishahara kinyume na maelekezo ya Mkuu wa Mkoa,ambapo Septemba 18 (Jumamos), kampuni hiyo ililipa wafanyakazi ujira wa wiki mbili,kwa njia ya kienyeji (Dirishani),licha ya kutakiwa kuanza utekelezaji wa kulipa mishahara kwa kufuata taratibu zinazokubalika kisheria,kwa ajili ya maslahi ya wafanyakazi, na upatikanaji wa kodi ya serikali.Hali hii iliashiria kuwa, maagizo ya Mkuu wa mkoa yalikuwa but una hayajaanza kutekelezwa.

Wafanyakazi hao walilipwa fedha kati ya Shilingi 77,000 hadi 84,000,ikiwa ni malipo ya majuma mawili yaliyopita,licha ya kuwepo kwa maelekezo ya serikali kuachana na kiasi hicho cha malipo pamoja na namna hiyo ya ulipaji.

“Nimekerwa sana na vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na kampuni hii,nimeshatoa taratibu,naomba zifanyike na hili lisijirudie tena’’, ni maneno ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Queen Sendiga,aliyoueleza uongozi wa kiwanda hicho alipofika kiwandani hapo mapema mwezi huu (Septemba),na kuagiza utaratibu wa awali kuachwa mara moja, ikiwemo suala la mishahara,hali ambayo bado imeendelea.

Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho pia walijaribu kumkingia kifua muwekezaji, na kuwatuhumu wanaolalamika kuwa hawaridhiki,lakini baada ya uchunguzi,tulibaini kuwa wote waliozungumza na kuwatetea wawekezaji,ni wale ambao wana nafasi mbalimbali za uongozi katika kiwanda hicho.

“Sisi inabidi tunufaike kupia wao,na wao wanufaike kupitia sisi,ila wote wanaolalamika wana “Base” sana kwetu,sasa ikifika wao (Wachina) wakaona wanakandamizwa sana,sijui kama wataendelea na uzalishaji na sijui tutaenda wapi”,alisema mmoja wa wafanyakazi ambae hakutaka jina lake litajwe,huku baadhi ya wafanyakazi wenzake wakizungumza na mwandishi pembeni na kumwambia “Huyo ni kiongozi”.

Wafanyakazi hao pia wamelalamikia kuendelea kufanya kazi bila mikataba,na kufanyishwa kazi muda wa ziada, ambapo waajiri huahidi kulipa muda huo, lakini hakuna hata mfanyakazi mmoja alishawahi kulipwa malipo hayo licha ya karibu wafanyakazi wote kufanyishwa kazi kwa masaa mengi.

“Kwenye makubaliano yetu ni kwamba lazima tutoke saa kumi na nusu (Kwa wanaoingia asubuhi),lakini hapa tunatoka hadi saa moja na nusu,na hela ndio ilele,haiongezeki wala nini”,Mfanyakazi wa kiwanda hicho Peter Punda aliimbia Watetezi Media,ambayo Septemba 19,ililazimika kwenda kiwandani hapo majira ya jioni na kushuhudia wafanyakazi wa kiwanda hicho wakitoka kwa makundi kuanzia saa 12:43 hadi saa 1.40 jioni, huku wengine wakiwa wamepakiwa katika malori ya wazi yaliyokuwa yakishua magogo kiwandani humo, kuelekea makwao.

Juhudi za kumpata msemaji wa kiwanda hicho ziligonga mwamba,baada ya msimamizi wa kiwanda hicho mwenye asili ya China, kukataa kuzungumza nasi,kwa madai kuwa hajui Kiswahili wala Kiingereza,na kwamba yeye si msemaji wa kampuni,maelezo aliyoyatoa kwa lugha ya  kichina, na kutafsiriwa kwa Kiswahili na mkalimani wa kampuni hiyo.

Hadi sasa kiwanda hicho kikubwa cha uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na misitu,kina wafanyakazi zaidi ya 300, ambao huingia kwa zamu asubuhi na usiku,huku uzalishaji wake ukionekana mkubwa lakini usio na tija kwa wafanyakazi,kwa kudaiwa kutozingatia sheria za kazi,haki za wafanyakazi,na usalama mahali pa kazi.