March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

WAAFRIKA WAELEZA KUWEPO KWA UBAGUZI UKRAINE

Wakati Urusi ikiendeleza mashambulizi ya kivita nchini Ukraine ,waafrika wanaotaka kuondoka nchini humo wamedai kukumbana na ubaguzi dhidi yao unaofanywa na wanajeshi wa Ukraine na maafisa waliopo mipakani.

Mwanafunzi mmoja anayesomea udaktari nchini humo amelieleza shirika la habari la CNN kuwa yeye pamoja na waafrika wengine walishushwa kutoka katika basi waliloabiri katika kituo cha ukaguzi kilichopo katika mpaka wa Ukraine na Poland.

Anasema waliambiwa wasimame pembeni wakati basi hilo likiondoka likiwa na raia wa Ukraine pekee.

“Mabasi zaidi ya 10 yalikuja tukawa tunaangalia wote wakiondoka,tulidhani baada ya kuwachukua raia wa Ukraine watatuchukua na sisi lakoni walituambia hakuna mabasi mengine hivyo tutembee,” alisema mwanafunzi huyo.

“Mwili wangu ulikufa ganzi kutokana na baridi kali na haujalala kwa siku nne sasa,raia wa Ukraine wamekuwa wakipewa kipaumbele kuliko waafrika hatutaki kujua kwanini tunajua sababu,ninataka tu kurudi nyumbani,” ameongeza

Kutokana na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine,raia wa Ukraine hasa wanawake na watoto wanakimbilia mataifa ya jirani kupata uhifadhi,na hii sio mara ya kwanza kuwepo kwa madai ya kuwepo kwa ubaguzi dhidi ya waafrika ambao wengi wapo masomoni wanaotaka kukimbilia nchi jirani kupata uhifadhi.