February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

VITA YA URUSI,UKRAINE:TANZANIA YAJIHAMI YAONGEZA BAJETI KUFIKIA TZS 41 TRILIONI

Serikali ya Tanzania, imepanga kukusanya na kutumia Sh. 41 trilioni katika bajeti ya 2022/2023, ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.1 ya bajeti ya Sh. 37.98 trilioni, iliyopangwa 2021/2022.

Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, akiwasilisha mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2022/23 na Mfumo wa Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka huo, jijini Dodoma.

“ Kwa kuzingatia sera, misingi, vigezo na vihatarishi vya bajeti, jumla ya Sh. 41,063.9 bilioni (Sh. 41 trilioni), zinatarajiwa kukusanywa na kutumika. Sawa na ongezeko la asilimia 8.1, ikilinganishwa na makadirio ya 2021/22 ya Sh. 37,980.6 bilioni,” imesema taarifa ya Dk. Mwigulu.

Taarifa ya Dk. Mwigulu imesema, mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa ya Sh. 28.698 trilioni, sawa na asilimia 69.9 ya bajeti yote, huku misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo inatarajiwa kuwa Sh. 4.154 trilioni.

Kupitia taarifa hiyo, Dk. Mwigulu amesema ongezeko hilo limezingatia sera, misingi na vihatarishi vya bajeti, ikiwemo vita kati ya Urusi na Ukraine, ambayo inatabiriwa kuongeza bei ya nishati duniani na kuchangia ongezeko la bei za bidhaa.

“Aidha, kutokana na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa kwa nchi ya Urusi, athari kubwa zaidi zinaweza kujitokeza kama vita hiyo itachukua muda mrefu. Maeneo ya moja kwa moja ambayo yanaweza kuathirika ni pamoja na nishati ya gesi ambapo Urusi ni msambazaji mkubwa wa nishati hiyo, kwa takribani asilimia 40” imesema taarifa ya Dk. Mwigulu na kuongeza:

“Kwa kuwa nchi za Ulaya ambazo zimekuwa zikipata nishati hiyo kutoka Urusi, zitahamia kwenye nchi nyingine, nishati hiyo inatarajiwa kupanda bei na hivyo Tanzania nayo itaathirika na ongezeko hilo. Vilevile, maeneo mengine yatakayoathirika ni, riba na bei za hatifungani katika masoko ya kimataifa, bei ya mazao ya kilimo na dhahabu.”