February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

VIONGOZI WAPYA TLS,WAJENGEWA UWEZO KUHUSU NAMNA YA KUENDESHA MASHAURI YA KIMKAKATI

Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania,Onesmo olengurumwa amesema kuwa uelewa mdogo kuhusu mashauri yenye maslahi ya umma miongoni mwa mawakili nchini ndiyo changamoto kubwa inayozuia kufungua mashauri hayo kwani wengi wamejikita zaidi katika kesi zenye maslahi binafsi.

“Wengi wanaamini kuwa ukiwa wakili katika masuala ya haki za binadamu unaweza ukawa masikini, hakuna malipo hakuna fedha na ndio changamoto ambayo sasa wengi wameona hakuna umuhimu wa kufanya mashauri ya kimkakati,” ameeleza Olengurumwa wakati akizungumza na waandishi wa habari punde baada ya kuwasilisha mada katika semina elekezi kwa viongozi wapya wa Kanda wa Chama cha Wanasheria Tanganyika mapema hii leo.

Aidha Olengurumwa ameongeza kuwa njia pekee ya mawakili kuweza kuisaidia jamii ni kupitia mashauri ya kimkakati na kuwataka viongozi hao kuwa chachu kwa mawakili wengine pamoja na kuwashawishi kufungua kesi za kimkakati huku THRDC ikiahidi kuwa nao bega kwa bega na kuwapa sapoti.

“pia changamoto ya kiusalama, tumeona baadhi ya mawakili makampuni yao yakifungiwa sasa vyote hivi vimeweka mazingira magumu sana ya kuwa na mawakili wengi nchi nzima wanaojishughulisha na mashauri mbalimbali ya kimkakati,” ameongeza Olengurumwa na kuongeza kuwa wataendelea kushirikiana na TLS na pale itakapowezekana watawakusanya mawakili kutoka katika kila kanda na kuwajengea uwezo kuhusu kufungua na kuendesha mashauri ya Kimkakati.

Kwa upande wake Jaji Mstaafu, Robert Makaramba ameeleza kuwa ni lazima mawakili watumie nguvu ya ziada katika kujielimisha kuhusu mashauri ya kimkakati na wakati wa kuendesha mashauri hayo hawana budi kutafuta maoni ya wadau wengine kama watu wa haki za binadamu.

“Wahusishe na  watu wengine kuhusu hiyo kesi  usifanye kuiatamia…hata ikitokea umeshindwa mahakamani endelea kufanya uchechemuzi endelevu suala ambalo mawakili wengi hawalifanyi”ameeleza Makaramba.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS),Kaleb Gamaya amesema mafunzo hayo yamelenga kuwapitisha viongozi wapya kuhusu majukumu yao na kuwapa uelewa kuhusu nini cha kufanya katika kanda zao huku akiishukuru THRDC kwa kushirikiana nao katika kuandaa na kutoa mafunzo kwa viongozi hao.

“Hawa wadau wamejikita katika eneo la haki za bindamu na wanalisimamia vizuri sana,sasa badala ya sisi kuhangaika huku na kule kwenye eno hili tunaona tu ni vizuri tufanye kazi na wadau wenzetu kuliko kushika kila kitu,”ameeleza Kaleb.

Kwa upande wao washiriki wa warsha hiyo wameahidi kutendea kazi kile walichojifunza kuhusu kesi za kimkakati ili kuweza kuisaidia jamii.

“Kutokama na mafunzo haya kwanza nimepata hamasa kubwa sana na haitaishia hapa itaendelea mpaka kwa mawakili ambao nawawakilisha,”amesema Faudhia Mustafa mmoja wa viongozi wa Kanda TLS.