February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

VIKUNDI AMBAVYO HAVIJAREJESHA KWA WAKATI MIKOPO 10% YA HALMASHAURI KUFIKISHWA MAHAKAMANI

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Yahaya Nawanda amemuagiza Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa,Simon Berege kuvifikisha mahakamani vikundi vyote vya vilivyoshindwa kurejesha mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani.
Imeelezwa kuwa vikundi hivyo vinahusisha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambavyo inadaiwa kuwa vimeshindwa kurejesha mikopo kwa wakati muafaka waliokubalina na Serikali.
Elekezo hilo amelitoa Agosti 17, 2022 akiwa mjini Maswa wakati akizungumza na watumishi wa serikali na mashirika ya umma kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo huku akiongeza kuwa ni lazima vikundi vilivyopatiwa mikopo ya fedha virejeshe ili vikundi vingine viweze kukopa huku akimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuvifikisha mahakamani ambavyo havijaresha fedha.
“Ndani ya mwezi mmoja watu wote waliochukia fedha za asilimia kumi lazima tuwapeleke mahakamani na waanze kurudisha fedha hizo kuanzia kesho mkurugenzi fedha zote za asilimia kumi ambazo zilichukuliwa na wananchi wakakopa aidha kwa vijana, watu wenye ulemavu na wanawake lazima zirudishwe “Dkt Nawanda.
Akizungumza kuhusu agizo hilo, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Simon Berege amesema kuanzia Agosti 18, 2022 kwa kushirikiana na wanasheria wa halmashauri hiyo wataanza kuwafikisha mahakamani wadaiwa sugu huku akiongeza kuwa kuna vikundi vipatavyo 31 ambavyo havijarejesha mikopo ya zaidi ya Sh. Milioni 200 na mikopo hiyo ni ile iliyotolewa kuanzia mwaka 2013.
“Agizo hili tumelipokea na tunahakikisha wale wote amabao walichukua fedha za asilimia kumi ya mapato ya ndani kuanzia kesho tunawafikisha mahakamani ili itakapo fika siku ya ijumaa tuweze kutoa taarifa ya watu waliofikishwa mahakamani “amesema Mkurugezi wa Halmashauri ya Maswa, Simon Berege
Itakumbukwa Mikopo inayotolewa na Halmashauri za Wilaya uongozwa na Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa sura 290, ambapo Mwongozo huo unaelezea kuwa kanuni zilizowekwa chini ya kifungu cha 37 ambazo zinajulikana kama kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu za mwaka 2019 zinatumika katika Mamlaka zote za Serikali za Mitaa Tanzania Bara.