March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

UZINDUZI WA MWONGOZO WA KODI KWA ASASI ZA KIRAIA

Na Loveness Muhagazi

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Taasisi ya Wajibu Institute, KPMG kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hii leo wamezindua mwongozo waw Kodi kwa Asasi za Kiraia (CSO Tax Tool-Kit).

Akizungumza katika uzinduzi huo uliohudhuriwa na viongozi kutoka TRA Pamoja na watetezi wa Haki za binadamu kutoka taasisi ya Wajibu Institute Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania THRDC Onesmo Olengurumwa ameeleza kuwa Mwongozo huo uliozinduliwa ni nyenzo muhimu katika kukuza uelewa na utekelezaji wa sera na sheria za kodi kwa asasi za kiraia.

“Mchango wa Asasi za Kiraia (AZAKI) katika pato la taifa, umekua ni mkubwa sana, AZAKI mbalimbali kutoka kote nchini zimekuwa zikichangia pato la taifa kupitia kodi mbalimbali kama vile Kodi ya Mapato (PAYE), Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Withholding Tax (Kodi ya Zuio) , Kodi ya Mhuri (Stamp Duty) na kodi zingine nyingi” Mratibu Onesmo Olengurumwa wakati wa Uzinduzi.

Hata hivyo Olengurumwa alipata wasaha wa kuelezea namna mwongozo huo utaweza kuzisaidia Asasi za Kiraia katika maswala ya ulipaji Kodi ambayo awali yalikuwa yakifanyika kwa usumbufu mkubwa kutokana na Asasi za Kiraia kutokuwa na uelewa mpana wa mahitaji yaliyotakiwa na Mamlaka ili kutimiza wajibu wao.

“Kwa kifupi, mwongozo huu unaelezea namna ya kujisajiri kama mlipa kodi, matakwa ya sera, sheria na miongozo mbalimbali kuhusu haki na wajibu katika kulipa kodi. Vilevile, mwongozo unaelezea dhana tofauti kuhusu aina tofauti za kodi ikiwa ni pamoja na ushuru na kodi mbalimbali. Pia, mwongozo umeelezea ni kwa namna gani taasis inaweza kuwa Taasis ya Kihisani (Charitable organization) na namna taasis za kihisani zinatozwa kodi. Kiujumla, mwongozo huu umejikita katika kuelezea maeneo ambayo yana changamoto katika ulipaji wa kodi kutoka Asasi a Kiraia ili kukuza uelewa na utekelezaji wa sera na sheria za kodi” Olengurumwa

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Naibu Kamishina wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Bi Feliciana Nkane amefurahi kushiriki katika tukio la Uzinduzi wa Mwongozo huo na kuzipongeza Asasi zote zilizoshiriki katika mchakato wa kuandaa mwongozo wa kodi kwaajili ya asasi za kiraia na kueleza kuwa AZAKI zimekuwa na mchango mkubwa kwa mapato ambayo yamekuwa yakitumika katika uwezeshaji wa shughuli mbali mbali za kijamiii.

“Mmekuwa na mchango mkubwa kwa pato la taifa (GDP). Kulingana na ripoti ya 2015 ya Wizara ya Afya juu ya mchango wa Mashirika yasivo ya Kiserikali nchini, takwimu zinaonvesha kwamba katika mwaka huo, asilimia 78 ya mapato ya NGOs yalikuwa yametumika moja kwa moja kufadhili shughuli za maendeleo ya watu kama vile kilimo, afya, elimu, maji, na huduma zingine za kijami. Asilimia 22 tu ndio zilitumika kukidhi gharama za uendeshaji wa mashirika hayo” Feliciana Mkane, Naibu Kamishina TRA

Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Imeahidi kuhakikisha inashirikiana vyema na Asasi za Kiraia kuhakikisha Mwongozo huu unasambaa kote nchini katika kila wilaya ili kuhakikisha AZAKI zote nchini zinapata Uelelewa wa maswala ya ulipaji kodi kama yalivyoelekezwa katika Mwongozo huo.

“Sisi kama TRA tutasambaza nakala za mwongozo huu katika ofisi zetu zote za wilaya ili ninyi AZAKI muweze kupata nakala bure pasi na malipo yoyote. Hii ni kusudi asasi nyingi zaidi zifaidike na taarifa zilizomo katika mwongozo huu ikiwemo taratibu za namna ya kuomba kibali cha hadhi va kutolipa kodi (Charitable status). Nitoe wito kwa wadau wote katika sekta ya Asasi za Kiraia kupata nakala za muongozo huu, kutilia maanani yaliyomo, na pia kuwashirikisha na wengine katika maeneo yao. Lengo ni kuhakikisha asasi za kiraia kote nchini zinapata uelewa wa ulipaji kodi kama ilivyoainishwa katika mwongozo huu. Tunaamini hili litapunguza kwa kiasi kkikubwa changamoto za ulipaji kodi kwa asasi za kiraia” Feliciana Mkane, Naibu Kamishina TRA

Hata hivyo Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Imeupongeza Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Accountability Tanzania, na WAJIBU-Institute of Public Accountability kwa kwa kuwa mstari wa mbele kushirikiana na sisi TRA katika kuhakikisha mwongozo huu unakamilika na leo kuzinduliwa.

MWISHO