March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

UMILIKI WA SILAHA KIHOLELA,UNAATHIRI VIPI HAKI ZA BINADAMU?

 Na Anthony Rwekaza Benedicto

Inawezeka kwa wengi si mara ya kwanza kusikia baadhi ya watuhumiwa wanakamatwa wakiwa na silaha ambazo hazijasajiliwa kisheria, wala sio mara moja kuona uhai wa raia umekatizwa kutokana na silaha za moto, kuna raia wasio na hatia wanaishi na ulemavu utokanao na kutendewa matukio yaliyosababishwa na watu wanaomiliki silaha kiolela.

Umewahi kufikiri na kujiuliza kuwa kumiliki silaha kiolela kuna unaathiri vipi haki za binadamu?

Ili kupambana na matukio hayo ambayo yanahatarisha usalama wa binadamu, Nchini Tanzania Serikali imelipa umakini gani jambo hili?

Mnamo mwaka 2015 Tanzania ilianza kutekeleza Sheria ya usimamizi na udhibiti wa Silaha na Risasi (firearms and Ammunition Control Act 2015).Sheria hiyo inatoa utaratibu na miongozo kwa mtu anayetaka kumiliki Silaha na risasi, miongoni mwa vifungu hivyo ni pamoja na kifungu cha 11 ambacho kinabainisha vigezo muhimu vya mtu kumiliki Silaha na risasi.

Sheria hiyo yenye vifungu 76 vinaeleza kuanzia mchakato wa kununua silaha, usajili na matumizi ya silaha hiyo, michakato hiyo ikiwa inaelezwa kuwa lengo ni kuimalisha usalama wa raia na mali zao.

Je umiliki wa Silaha kiolela upelekea madhara gani kwenye jamii hususani haki za mbinadamu?

Huchochea ongezeko la uhalifu kwenye jamii, mfano silaha zinapomilikiwa kiholela na watu wenye nia ovu mfano vibaka na wezi, wizi na uporaji huogezeka kwenye jamii kwa kuwa wananchi hutishwa na kunyang’anywa mali zao au kuibiwa.

Hupelekea jamii kukosa amani. Pale silaha zinapozagaa mtaani bila kuzingatia utaratibu, maisha ya raia yanakuwa njia panda, kutokana na kuogezeka kwa ujambazi ambao wengi wao utumia silaha za moto kufanikisha malengo.

Huchochea mateso ya kisaikolojia kwa raia. Kwenye masharti ya kupewa kibali cha kumiliki silaha inaelekeza kuwa mtu atakayepewa kibali cha silaha hiyo awe amefuzu mafunzo ya kutumia silaha ikiwa ni pamoja na wapi silaha hiyo inatakiwa kutumika.

Kama ilivyoripotiwa na Jeshi la Polisi Kanda maalumu ya Dar es salaam juu la tukio la watu wawili kupoteza uhai maeneo ya Sinza na matukio mengine yaliyowahi kulipotiwa nyuma, ambayo hudaiwa watu kuonyesha silaha kwenye kumbi za starehe, jambo ambalo Watetezi tv inatilia shaka watu hao kama wameelimika vizuri juu ya matumizi ya silaha hizo.

Katiba ya Jamhuri Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo ndiyo msingi mama unatoa mwongozo kwenye utekelezwaji wa sheria nyingine, inatoa haki kwa kila mtu lakini usioathiri mipaka ikiwa ni pamoja na kuathiri haki zingine.Mfano umiliki wa silaha usikatize haki ya kuishi ya mtu mwingine.

Pale  silaha za moto zinapotolewa hadharani kwenye mazingira ambayo hayakidhi vigezo inakuwa inaathiri uhuru wa raia wengine, jambo ambalo ni kinyume na haki za binadamu, na kwenye sayansi ya akili raia anaweza kuathirika kisaikolojia.

Jamii inaweza kupata hofu au baadhi ya raia wanaweza kupata mashaka pale wanaposikia matokio hovu yanayohusisha silaha za moto. Hofu ikiongezeka amani hupungua, kama raia wamezoea kuona silaha zikiwa zimebebwa na askali siku wanapoona raia wa kawaida ameshikiria silaha!, kuna uwezekano mkubwa kupatwa na hofu.

Nini Kifanyike kutokozemeza matukio hovu yatokanayo na umiliki wa silaha kiolela?

Kuna umuhimu mkubwa kwa Serikali kupitia vyombo vya dola kuthibiti mazingira yoyote yale ambayo yanaweza kuruhusu watu kumiliki silaha kiolela, kuimarisha zaidi na kuogeza umakini kwenye maeneo ya mipakani ili kuthibiti silaha zinazoweza kutoroshwa kwenye Nchi jirani kuingizwa Nchini ili kutumika kufanikisha matukio hovu.

Mamlaka ambazo zimepewa dhamana kisheria kwa utoaji wa leseni za kumiliki silaha ni muhimu kutoa zaidi kipaumbele kwenye elimu ya umiliki silaha kabla ya kutoa vibali, huku pia ikiwekeza umakini wa kufuatilia kwa umakini mwenendo wahusika wanaoitaji silaha kabla ya kutoa kibali kama sheria inavyobainisha.

Watetezi TV inatambua Jamii iliyostaarabika hulinda haki za binadamu kwa kuheshimu utu wa watu, kusitawisha tunu za amani kwenye jamii, kuepuka matumizi ya silaha za moto kinyume na matakwa ya Sheria ya uthibiti na usimamizi wa silaha na risasi 2015.