February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

“UKAMATAJI MIFUGO HIFADHINI NI UKATILI MKUBWA”-JOB NDUGAI

Job Ndugai-Spika wa Bunge la Tanzania.

Leonard Mapuli.

Spika wa Bunge Job Ndugai ameshanga mwendelezo wa vitendo vya ukamataji wa mifugo inayoingia katika maeneo ya  hifadhi na kudai kuwa kitendo hicho hakikubaliki.

Kwa muda sasa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa jamii za wafugaji juu kukamatiwa mifugo yao na kutaifishwa jambo Job amesema ni kinyume cha sheria na kwamba kama bunge ndilo lilipitisha sheria hiyo,bali litakuwa bunge la ajabu na huenda siku hiyo hakuwemo bungeni.

“Mheshimiwa waziri wa mifugo hii mingongano ya wafugaji na hifadhi ambapo ile sheria sijui ilipitaga wapi,sijui tulikuwa tumelala au ilikuwaje,ile kwamba ng’ombe wakiingia kwenye hifadhi wanataifishwa wote??Hapana hapana”Amekataa spika Ndugai na kuiita sheria hiyo kuwa dhulumati kwa vile ngo’ombe hawana utashi wa kuamua waende kupata malisho wapi wala kung’amua mipaka ya hifadhi.

“Na siku hizi ukitazama wanaochunga mifugo ni vijana wadogo,wanaweza kuwa wanacheza mpira ukakuta ng’ombe zimeshaingia kwenye hifadhi wanakamatwa,wanauzwa” ameongeza Ndugai na kusema kitendo hicho ni ukatili mkubwa dhidi ya wafugaji.

Ndugai ameendelea kushangaa kukamatwa kwa mifugo waingiapo hifadhini na kutaifishwa huku wanyamapori kama tembo na wengineo wakiripotiwa kuingia katika maeneo ya watu na kufanya uharibifu ukiwemo wa mazao bila wizara kuchukuliwa hatua yoyote,na amemtaka waziri mwenye dhamana kulitazama hilo ili kuwe na usawa.

“Tembo nae akiingia kwenye shamba la mtu basi iwe mali yake”amesema Ndugai na kushangiliwa na wabunge kwa makofi.

Ndugai pia amepinga takwimu za mifugo zilizotolewa na wizara hiyo akiziita kuwa ni  za kupika baada wizara kusema Tanzania ina ng’ombe milioni 33.6 na kuagiza kufanyika kwa upya kwa sensa ya mifugo ambayo kuna uwezekano mkubwa idadi kupungua sana nchini Tanzania.

Bunge linaendelea na mjadala wa makadilio ya mapato na matumizi ya wizara ya mifugo na uvuvi kwa mwaka wa fedha 2021/2022  ambapo wizara hiyo imeliomba bunge kupitisha jumla ya shilingi bilioni 169.19,kati fedha hizo,shilingi bilioni 47.84 zitakwenda zitatumika na sekta ya mifugo,huku bilioni 121 zikitengwa kwa ajili ya sekta ya Uvuvi.