March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

“UHURU WA ASASI ZA KIRAIA UNAREJEA”-OLENGURUMWA

MRATIBU WA THRDC ONESMO OLENGURUMWA AKIFUNGUA MKUTANO WA CSOs-Mei 28,2021.

Na Leonard Mapuli

Mratibu wa kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania na wakili wa Mahakama kuu Onesmo Olengurumwa amesema kuna matumaini makubwa kurejea kwa uhuru wa asasi za kiraia   pamoja na nafasi ya ushiriki wa watu katika masuala mbalimbali kwa uhuru katika utawala wa awamu ya sita.

Olengurumwa amebainisha hayo wakati akifungua mkutano wa kikosi kazi cha asasi za kiraia kilichokutana kujadili masuala mtambuka yanayohusu hali ya uhuru wa  kujieleza nchini Tanzania kilichofanyika leo (Mei 28) jijini Dar es Salaam .

“Uwepo wa mama Samia unatupa moyo sana sisi asasi za kiraia, tunaona ushiriki wa wananchi sasa unarejea,kila kitu kimefunguka,lakini kabla yake hali ilikuwa mbaya,nafasi ya ushiriki wa wananchi (Civic Space) ilipotezwa”-amesema Olengurumwa na kuwataka wadau wote wa asasi za kiraia kujitokeza kwa wingi kupaza sauti maana mazingira sasa ni rafiki.

Moja kati ya nafasi ya iliyokuwa ikipigiwa kelele ni uhuru wa watu kukusanyika ama kufanya mihadhara ya siasa ,utetezi wa haki za binadamu, kwa kutaja baadhi,ambapo mamlaka za serikali zilizuia mikusanyiko ya aina hii ambayo kisheria kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kiusalama.

Tangu mwaka 2015 kumekuwepo na kilio cha kukosekana kwa ushiriki wa wananchi katika kujieleza,kukusanyika na kujumuika baada serikali kuzuia baadhi ya shughuli,kuweka masharti magumu ya kisheria kwa watu kujieleza.

“Ilikuwa inashangaza vyama vya siasa vinanyimwa kukusanyika,Asasi zinazuiwa kufanya mikutano kwa sababu za kiintelijensia,wakati Diamond anafanya matamasha anakusanya watu na anaruhusiwa,Simba na Yanga wanacheza na watu wanakusanyika uwanja wa taifa,marathoni watu wanakimbia hadi polisi wenyewe,hawakuzuiwa,lakini vyama vya  upinzani wakiomba kibali kukusanyika wanazuiliwa kwa sababu za usalama”,amehoji Wakili Fulgence Massawe kutoka kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania,LHRC.

Baadhi ya sheria zinazotajwa kuathiri uhuru wa kujieleza ikiwemo habari pamoja na kunyima asasi  za kiraia kutimiza majukumu yake ni  sheria ya huduma ya vyombo vya Habari,Sheria ya upatikanaji taarifa,Sheria ya NGO’s, na Maboresho ya Sheria ya vyama vya siasa,kwa kutaja baadhi,na zote hizi zilitungwa ndani ya miaka mitano kuanzia 2015 kwa lengo kudhibiti ushiriki asasi,utoaji elimu,uhuru wa kujieleza,pamoja na uhuru wa habari kwa ujumla.

“Dhima ya vyombo vya habari ni kuelimisha,kuburudisha,kuhabarisha,na kukosoa,ila hii ya kukosoa ilikufa kabisa,ya kuelimisha ikawekewa mipaka,  tukabakiza kuburudisha na kuhabarisha kuhusu maendeleo”,amesema Edwin Soko,Mwenyekiti wa Chama cha Wandishi wa habari mkoa wa Mwanza.

Sheria ya BRADEA ilifanyiwa marekebisho mwaka 2020, ambapo kifungu cha 4 kilibadilishwa na kuweka takwa la kisheria kwamba; kesi ya mtu itakubaliwa na Mahakama Kuu endapo tu mtu huyo anayefungua kesi ameambatanisha kiapo kinachoonyesha kuwa ni kwa kiasi gani mtu ameathirika yeye binafsi. Marekebisho hayo yaliondoa haki ya watu au mashirika kufungua kesi zenye maslahi kwa umma,na kuyafanya kukosa fedha za ufadhili toka kwa wahisani.

“Wafadhili walikimbia,waliogopa kuweka pesa maana zisingekuwa na kazi”,ameongeza Charles Odero,Mkurugenzi wa Shirika la CLAO.

 Mkutano wa kikosi kazi cha nafasi ya Asasi za kiraia kujadili masuala mtambuka kuhusu hali ya uhuru wa kujieleza nchini Tanzaniwa kimeandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za binadamu Tanzania (THRDC) pamoja na American Bar Association umehudhuriwa na wadau kutoka asasi mbalimbali pamoja wandishi wa habari.