February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

UGANDA:MTOTO,DEREVA WA GEN. KATUMBA WATHIBITIKA KUUAWA KWA RISASI.

Gari la Gen. Katumba baada ya kushambuliwa kwa risasi

Mtoto wa Generali Katumba Wamala anayefahamika kwa majina ya Brenda Wamala Pamoja na dereva  wa generali huyo mstaafu wa jeshi la Uganda,wamepoteza Maisha katika shambulio la risasi lililofanywa na watu waliojihami kwa silaha mapema hii leo (June 1).

“Brenda (Binti wa Gen. Katumba aliyeuawa) ndio kwanza alikuwa amerejea nchini baada ya kuhitimu masomo yake nchini Marekani,sijui serikali itasemaje maana Katumba hakustahili kutendewa kitendo kile,inaumiza”,amesema Joyce Sentongo,ndugu wa karibu wa Gen. Katumba.

Wahalifu waliliminia risasi gari la waziri huyo lilikouwa kwenye mwendo na kusababisha mauaji ya wawili hao huku Generali Katumba akinusurika lakini akisalia na jeraha la risasi iliyompata sehemu ya bega.

Taarifa iliyotolewa na msemaji mkuu wa jeshi la Uganda Brigadia Flavia Byekwaso imefafanua kuwa,shambulio hilo ambalo bado lengo lake hasa halijafahamika lilifanywa na watu wanne waliokuwa katika pikipiki ambao walilishambulia kwa risasi gari alilokuwemo generali Katumba,bintiye,na dereva.

Duru za siasa za Uganda zinadai kuwa upo uwezekano mkubwa kuwa tukio lile lilikuwa na shabaha ya kuumua generali Katumba,hata hivyo taarifa hizo hazijathibitishwa na mamlaka za usalama za nchini Uganda.

“Haya ni matukio yenye malengo ya kuzusha taharuki kwa jamii,serikali ya Uganda itayashughulikia kikamilifu,tuwape mamlaka muda wa kuchunguza na watuambie kilichotokea haswa ni nini”,amesema Chris Baryomunsi,waziri wa nchi anaeshughulikia nyumba na maendeleo ya makazi katika serikali ya Uganda.

Spika wa bunge la Uganda Jacob Oulanyah na makamu wake wamemjulia hali Generali Katumba anayeendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Kimataifa ya Madpal mjini Kampala.

Generali Katumba amepata kuwa mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama nchini Uganda kati ya mwaka 2013 hadi 2019 kabla ya kuzigeukia medani na siasa.Hili ni tukio la pili kushambuliwa kwa risasi kwa wanasiasa nchini Uganda ndani ya miaka miwili ambapo June 8 mwaka 2018 mbunge wa jimbo la Arua,Ibrahim Ibiriga aliuawa kwa kushambuliwa kwa risasi akiwa eneo la Kawanda,Jirani san ana makazi yake.