February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

UFARANSA YAIOMBA RWANDA MSAMAHA MAUAJI YA KIMBARI

Rais Paul Kagame wa Rwanda na Emmanuel Macron wa Ufaransa

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliyeanza ziara yake ya kihistoria nchini Rwanda ameiomba radhi nchi hiyo kufuatia mauji ya kimbari ya mwaka 1994 kwa kuwa Ufaransa ilikuwa na wajibu mkubwa na wa kihistoria kuwajibikaji dhidi ya mauaji ya kimbari nchini  Rwanda.

“Nimesimama hapa mbele yenu leo kwa unyenyekevu na heshima kubwa,nimetambua uwajibikaji wa Ufaransa ulikuwa muhimu” amesema Rais Macron mwanzoni mwa hotuba yake aliyoitoa eneo la makumbusho ya mauaji ya Kimbari,yalipohifadhiwa mabaki ya watu 250,000 waliouawa katika mapigano ya kikabila miaka 27 iliyopita.

Macron amekuwa rais wa kwanza wa Ufaransa kuitembelea Rwanda baada ya miaka kumi ya kigugumizi kwa Ufaransa dhidi ya mauji ya maelfu ya Wanyarwanda,wengi wao wakiwa jamii ya Watutsi.

Rais Macron amewasili kwa ziara ya kihistoria, kurejesha uhusiano baina ya nchi hizo mbili zilizokuwa na uhusiano wa kihistoria uliokuwa umepotea kwa mwaka 27,na amekaribishwa vyema na mwenyeji wake Paul Kagame ambae amempongeza kwa kutambua  umuhimu wa Ufaransa na uwajibikaji kufuatia mauaji ya Kimbari.

“Maneno yake yamekuwa ya thamani kuliko  hata msamaha wenyewe,na ni yakweli”,amesema Rais Kagame alipozungumza na wanahabari mara baada ya mazungumzo yake na Rais Macron mjini Kigali.

Kiongozi mkuu wa chama  cha manusura wa mauaji ya kimbari (IBUKA) Egide Nkuranga amesema hotuba ya Macron haikuwa na matumaini makubwa na ni ya kukatisha tamaa maana hajaomba msamaha wa kueleweka  kwa niaba ya Ufaransa wala hajaomba kusamehewa.

“Amejaribu tu kuelezea mauaji na wajibu wa Ufaransa,na hii ni sawa maana anaonesha dhahiri kuwa anajua ukweli”,amesema Nkuranga alipokosoa hotuba ya Macron.

Ufaransa ilihusikaje na mauaji ya kimbari?

Matokeo ya ripoti mbili zilizotolewa  mwezi March na April mwaka huu kuhusu jukumu la Ufaransa  kwa Rwanda zilibainisha uwezekano  wa Ufaransa kuhusika katika mauaji yale.Ripoti hizo mbili zilizokabidiwa kwa rais Macron ziliishtumu Ufaransa kuhusika katika umwagaji damu nchini Rwanda kwa namna moja ama nyingine.

Matokeo ya ripoti hizo,yaliyokubaliwa na Serikali ya Ufaransa,  yanaituhumu Ufaransa kuhusika katika mauaji hayo  kwa kuwa ilikuwa karibu zaidi utawala uliokuwa madarakani wa kabila la Wahutu.Hata hivyo hapakuwa na ushahidi wa moja kwa moja juu Ufaransa kuhusika katika umwagaji damu japo wengi wa waliouawa walikuwa ni kabila hasimu la Watutsi.