February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

UFAFANUZI WA KISHERIA KUHUSU ARDHI YA LOLIONDO

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na taarifa zisizo sahii zinazotolewa na baadhi ya viongozi
kwa ushirika na wale wenye kutamani ardhi ya Loliondo kuwa ardhi yote ya Loliondo na
Sehemu ya Tarafa ya Sale ni ardhi ya hifadhi. Wanaodai kuwa kilometa za mraba 4000 za
Tarafa ya Loliondo na Sale sio ardhi ya vjijiji, huenda hawajui wanachosema au wameamua
kutumia nafasi zao kuchukua ardhi ya vijiji kwa nguvu. Naomba ifahamike pia kuwa sio
viongozi wote wanaamini kuwa eneo lote la Loliondo sio ardhi ya vjijiji bali wanaotangaza
kuwa kilometa za mraba 4000 si za ardhi ya vjiji ni wachache kwa maslahi ya wachache.
Natumia nafasi hii kufafanua kisheria kuhusu hadhi ya ardhi ya Loliondo na Sale kisheria ili
kubaini ukweli kuhusu hadhi ya ardhi ya Loliondo kisheria.
Baada ya uhuru, serikali iliendeleza mfumo wa utawala ambapo wilaya na vijiji viliendelea
kuwa sehemu ya utawala wa Serikali za Mitaa ambapo eneo la wilaya ya Ngorongoro ilikuwa
chini ya utawala wa Wilaya ya Maasai. Wilaya ya Maasai ilijumuisha Wilaya za sasa za Kiteto,
Simanjiro, Monduli, Longido na Ngorongoro na makao makuu ya wilaya ikiwa ni Monduli.
Baadae mwaka 1979, Wilaya mpya ya Ngorongoro ilianzishwa ili kurahisisha upatikanaji wa
huduma kwa wananchi. Wilaya ya Ngorongoro ina Tarafa tatu ambazo ni; Tarafa za
Ngorongoro, Loliondo na Sale. Jumla ya kilimeta za Mrabza za Wilaya ni 14,036 ambapo
Tarafa ya Ngorongoro ina kilometa za mraba 8,300, Sale 3,500 na Loliondo 2,200. Manake
kilometa za mraba za lililokuwa Pori Tengefu la Loliondo lilichukua kilometa za mraba zote
2,200 za Loliondo pamoja na kilometa za mraba 1800 za Tarafa ya Sale.
Ikumbukwe kwamba kabla ya uanzishwaji wa Wilaya ya Ngorongoro, wananchi katika tarafa
za Loliondo na Sale walikuwa wakiishi na kumiliki ardhi katika vijiji vyao vilivyosajiliwa
ndani ya iliyokuwa Wilaya ya Maasai. Baadhi ya vijiji katika tarafa vilisajiliwa kabla ya
kuanzishwa kwa Wilaya mpya ya Ngorongoro. Mgogoro uliopo wa sasa ni kuhusu mpango wa
serikali wa kutaka kuchukua ardhi ya vijiji yenye ukubwa wa kilometa za mraba 1500 kuwa
sehemu ya hifadhi pekee na kuwaondoa wananchi pamoja na kuzuia kazi za ufugaji. Mkuu wa
Mkoa wa Arusha pamoja na viongozi wengine tangu mwaka huu uanze wamekuwa
wakisisitiza kuwa ni lazima serikali itenge ardhi hiyo ya vijiji kwa shughuli za uhifadhi pekee.
Wamekuwa wakisisitiza kuwa hilo eneo si la vivjiji bali ni eneo lilikuwa pori tengefu ambapo
serikali inataka kuchukua kilometa za mraba 1500 na kugawia wananchi kilometa za mraba
4000.
Hadhi ya Ardhi ya Loliondo ilikuwaje wakati wa Ukoloni
Matokeo ya majadiliano na mapitio ya nyaraka mbalimbali yanaonyesha kuwa kabla ya ujio
wa wakoloni wa Kijerumani na baadae Waingereza jamii ya kimasai ilikuwa inamiliki na
kutumia ardhi hii kwa taratibu za kimila chini ya usimamizi na uangalizi wa viongozi wa mila
kwa niaba ya jamii.
Ujio wa wakoloni ulileta utaratibu mwingine ambao ulikuwa chini ya sheria za kikoloni hasa
wakati wa Wajerumani na baadae Waingereza walipokuja na sheria ya Ardhi namba 3 ya
mwaka 1923 na kufuatiwa na sheria zingine ikiwemo za Uhifadhi wa Wanyamapori. Umiliki
wa ardhi kimila ulitambuliwa pia na Sheria ya Ardhi ya mwaka 1923 na iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 1928, ili kutambua zaidi haki za wenyeji.
Pamoja na kutungwa kwa sheria mpya ya Ardhi, wakati huo wa utawala wa waingereza ni
wakati huo pia zilitungwa sheria zinazo husiana na usimamizi, ulinzi wa wanyamapori na
uhifadhi. Uwepo wa mapori ya wanyama katika eneo la Sale na Loliondo ulikuwa ni wa muda
mrefu tangu miaka ya wakoloni wa Kijerumani hadi wakoloni wa Kiingereza. Ilipofika miaka
ya 1930, Serikali ya kikoloni ya Waingereza waliona umuhimu wa kuanza kutunga sheria za
kulinda maeneo ya wanyamapori hapa nchini na pia kuweka utaratibu wa kisheria wa kufanya
shuguli za uwindaji. Kwa miaka yote hiyo ya nyuma wakati wa ukoloni maeneo haya ya
Loliondo na Sale yalikuwa katika maeneo ya wananchi yanayomilikiwa kisheria kama
ilivyofafanuliwa hapo juu kwa lengo la kulinda na kuratibu shughuli za Wanyama pekee.
Jitihada za kutaka kuanzisha maeneo ya uhifadhi na mapori tengefu kisheria zilianza rasmi na
Wajerumani mwanzoni mwa karne ya 20. Mikakati yote hii zilijaribu kwa kiasi fulani
kutambua umiliki wa kimila wa ardhi wa jamii asili. Mikakati hii kwa maeneo mengi ya Afrika
Mashariki zilianzisha taratibu za kuweka mazingira ya jamii ya wamaasai kuanza kusumbuliwa
katika maeneo yao. Pamoja na kwamba ardhi ya wamasai Tanzania haikukaliwa na wakoloni,
tishio kubwa lilikuja kuwa baadae ni taratibu za kisheria za uhifadhi wa rasilimali asili na
mbuga za Wanyama kuanza kupewa kipaumbele na serikali za wakoloni na baadae serikali
zetu.
Himaya ya Wajerumani (German East Africa ) ilianza kuweka mikakati ya kumiliki maeneo
kuanzia mwaka 1885 hadi 1914 walipovamiwa na kuondolewa na Waingereza. Mfano
mwanzoni mwa karne ya 20, Wajerumani walianzisha Sheria ya kusimamia Wanyama Pori
iitwayo Game Preservation Ordinance ya mwaka 1908 hadi 1911.Baadae baada ya vita ya
kwanza ya Dunia Waingereza walikuja na kutunga sheria zingine nyingi baada ya vikao huko
Waingereza kuamua kulinda Wanyama na maeneo yao kama ifuatavyo zenye kulenga kwenye
usimamizi wa wanyamapori na uhifadhi
i. Kuanzishwa kwa Idara ya Wanyamapori (Tanganyika Game Department in 1919)
ii. Sheria ya Wanyamapori (The Game Preservation Ordinance 1921) iliyoanzisha pia Pori
la Akiba la Serengeti kwa wakati huo wa 1929.
iii. Sheria ya Ardhi ( Land Ordinance 1923 )
iv. Sheria mpya ya wanyamapori ( New Game Ordinance ya 1948), Sheria hii ndiyo
iliokuja na utaratibu wa kuanzishwa Hifadhi ya Serengeti (Serengeti National Park).
Hii ndiyo sheria ya kwanza iliyoanza kuleta maumivu makubwa hasa kwa ardhi za
Wamaasai waliokuwa wanaishi Serengeti, Ngorongoro na Loliondo. Mwaka 1959
Kutokana na sheria hii, Wamaasai wakaondolewa maeneo ya Serengeti Mwaka 1959
na kuhamishiwa maeneo ya Ngorongoro na Loliondo na kuungana na ndugu zao
wengine.
v. Sheria ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ya mwaka 1959- Sheria hii ilianzishwa
na watawala wa kikoloni ili kuhifadhi eneo la Ngorongoro na pia kuwalinda na
kuendeleza jamii ya wamaasai waliokuwepo na waliohamishiwa eneo la Ngorongoro
kupisha uanzishwaji wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Sheria mpya ya wanyamapori (New Game Ordinance ya 1948), ndiyo iliyokuja na utaratibu
wa kuanzisha Hifadhi ya Serengeti (Serengeti National Park). Hii ndiyo sheria ya kwanza
iliyoanza kuleta maumivu makubwa hasa kwa ardhi za Wamasai waliokuwa wanaishi
Serengeti, Ngorongoro na Loliondo. Mwaka 1959 Kutokana na sheria hii Wamasai
wakaondolewa maeneo ya Serengeti Mwaka 1959 na kuhamishiwa maeneo ya Ngorongoro na
Loliondo na kuungana na ndugu zao wengine. Sheria ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
ya mwaka 1959 ilitungwa na watawala wa kikoloni ili kuhifadhi eneo la Ngorongoro na pia
kuwalinda na kuendeleza jamii ya wamaasai walikuwepo na waliohamishiwa eneo la
Ngorongoro kupisha uanzishwaji wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Hadhi ya Ardhi ya Loliondo Baada ya Uhuru
Baada ya uhuru, serikali ya Tanzania ilitunga sheria ya Uhifadhi wa wanyamapori ya mwaka
1974 na kuanzisha mapori tengefu ambapo Loliondo na Sale yalitangazwa kwenye Gazeti la
Serikali Na. 269 la mwaka 1974. Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 1974, imechambuliwa
zaidi kwa lengo la kubainisha uhusiano na uwepo wa sheria hii na ardhi za vijiji. Uchambuzi
wa sheria hii unaonyesha jinsi mapori tengefu na mapori ya akiba yalivyoanzishwa kwa lengo
la kusimamia rasilimali za wanyama pori kipindi cha nyuma bila kuathiri milki za kimila za
ardhi katika ardhi za Vijiji wakati wa ukoloni na baada ya Uhuru. Kabla ya sheria hii ya
wanyamapori kutungwa baada ya uhuru, kulikuwa na sheria ya Ukoloni iliyoitwa Fauna Game
Ordinance, iliyoanzisha pori la akiba la Loliondo katika ardhi ya vijiji ambayo ilikuwa
inatumika kwa taratibu za kimila na tamaduni zao kama ilivyokuwa nchi nzima kabla ya
ukoloni. Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 1974 ilitambua aina tatu za mfumo wa ulinzi.
Mapori tengefu pekee ndiyo yalianzishwa katika maeneo ya Vijiji ambapo hayakuwa na
mgogoro kwa kuwa hayakugusa milki ya ardhi ya Vijiji.
Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1923 katika kifungu cha 9, ilitoa mamlaka kwa
Mkurugenzi wa Huduma za Maendeleo ya Ardhi kutoa hati za kumiliki ardhi za Vijiji. Baada
ya mabadiliko ya sheria za Ardhi za Tanzania hasa mwaka 1999, Sheria Mpya ya Ardhi ya
Vijiji Na.5 ya mwaka 1999 illibainisha kuwa, kutakuwa na Vyeti vya ardhi vya Vijiji tofauti
na hati za kumiliki ardhi zilizotolewa kwa Vijiji kwa mujibu wa Sheria ya ardhi ya mwaka
1923.Vilevile Sheria hizo mpya za ardhi zimeendelea kutambua hati hizo ambazo zilitolewa
kwa Mujibu wa Sheria zingine kabla ya kutungwa kwa Sheria hiyo.
Kipindi hiki itakumbukwa kutokana na jitihada za mageuzi makubwa ya upimaji wa Vijiji vya
wafugaji katika Tarafa za Loliondo na Sale kwa kupitia viongozi wa Vijiji, Kata, Wilaya na
mashirika ya kiraia ambapo vijiji mbalimbali vilipimwa na kupata Hati za kumiliki ardhi katika
Vijiji vyao kama ilivyoelezwa katika Taarifa ya Jamii kuhusu mgogoro huu. Mchakato wa
upimaji na hatimaye kutolewa kwa hati za kumiliki ardhi hizi, ulisimamiwa na Halimashauri
ya wilaya ya Ngorongoro kwa msaada wa mashirika ya KIPOC na ADDO.
Jumla ya ardhi ya vijiji vyenye ukubwa wa Hekta 346,672 za tarafa ya Loliondo zilipimwa na
kupatiwa hati za umiliki wa ardhi. Baadhi ya vijiji vilivyoweza kupata hati hizo ni pamoja na
Arash, Loosoito/Maaloni, Olorien/ Magaidur, Oloipiri, Soitsambu na Ololosokwan, kwa
mujibu wa sheria ya ardhi ya mwaka 1923. Jitihada zote hizi zinabainisha kuwa eneo la
kilometa za mraba 4000 za Loliondo na Sale ni ardhi halali za vijjiji zilizokuwa zinatumika pia
kama pori tengefu.
Usajili wa Vjijiji Loliondo na Sale
Kifungu cha 7 (12) cha sheria ya Ardhi ya Vijiji kinatambua hati zote za milki ya ardhi ya Vijiji
vilivyotolewa kwa mujibu wa sheria zingine kabla ya kutungwa kwa sheria hiyo. Hivyo kwa
mujibu wa sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999, Vijiji vyote vya tarafa za Loliondo na
Sale vilivyosajiliwa kwa Mujibu wa Sheria ya Serikali za mitaa [Mamlaka za wilaya] Na. 7 ya
1982 na kupata hati za kumiliki ardhi ni halali na vinaendelea kutambulika kisheria. Aidha ni
dhahiri kuwa hatua ya Serikali ya kutaka kumega ardhi ya Vijiji kiasi cha kilomita za mraba
1,500 inavunja Ibara ya 24 ya katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria za ardhi
ambazo zinatoa haki ya msingi ya kumiliki mali ambapo ni pamoja na ardhi kama rasilimali
kuu.
Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 1974, ilianzisha mapori tengefu ambapo
Loliondo na Sale ilitangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 269 la mwaka 1974. Kabla ya
sheria hii ya wanyamapori kutungwa baada ya uhuru, kulikuwa na sheria ya Ukoloni iliyoitwa
Fauna Game Ordinance iliyoanzisha pori la akiba la Loliondo katika ardhi ya vijiji ambayo
ilikuwa ikitumika kwa taratibu za mila na tamaduni zao kama ilivyokuwa nchi nzima kabla ya
ukoloni ambapo haikuwa na madhara katika milki ya ardhi ya Vijiji kwa kuwa ilitumika
kulinda na kuratibu shughuli za wanyamapori. Baada ya miaka kadhaa baadae baada ya uhuru,
mwaka 1974, Sheria hiyo ikafutwa baada ya kutungwa sheria mpya tajwa hapo juu ya
wanayamapori. Sheria hii pia ilitangaza maeneo ya mapori tengefu katika maeneo ya Vijiji na
haikuondoa haki ya milki ya ardhi ya wananchi katika ardhi ya Vijiji.
Ikumbukwe pia kwamba eneo hili la Loliondo ndilo ambalo wakoloni walionyesha kuwa
makazi ya wenyeji baada ya uanzishwaji wa Hifadhi ya Serengeti. Lakini wakati wa ukoloni
dhana ya mapori ya akiba yalianzishwa kwa lengo la kusimamia wanyamapori bila kuathiri
matumizi na mila za usimamizi wa ardhi za wenyeji. Hata hivyo, changamoto za kimaslahi kati
ya vijiji vya wafugaji na makampuni binafsi ya kitalii na kiuwindaji zilianza pale Tanzania
ilipoingia katika sera za mfumo wa soko huria na kuanza kubinafsisha hadi mashirika
yaliyokuwa yanaratibu maswala ya rasilimali asili hapa nchini. Serikali iliruhusu hadi
makampuni binafsi kuanza kusimamia shughuli za uwindaji.
Miaka hiyo kabla ya ubinafsishaji mfano kazi za uwindaji zilikuwa chini ya Tanzania Wildlife
Company (TAWICO) lakini baada ya miaka 1990 makampuni binafsi yalishamiri katika utalii
wa uwindaji na ndio ujio wa Kampuni ya Kiarabu ya Kiwindaji ya Ottero Business (OBC)
katika eneo la Loliondo mwaka 1992, na kupewa eneo lote la kilometa za mraba 4000 la Vijiji
vya Loliondo na sale. Ujio wa Kampuni hii ya Kiarabu ulianzisha changamoto ya wananchi
kutumia maeneo yao ya vijiji kinyume na sheria za ardhi na pia sheria hii ya Wanyamapori ya
mwaka 1974. Migogoro mingi ilianza kuzuka baina ya kampuni hii na wananchi na pia baina
ya kampuni hii ya OBC na watumiaji wengine wa ardhi ya vijiji kama makampuni mengine
yanayofanya kazi za kitalii eneo hili.
Lililokuwa Pori Tengefu (GCA) la Loliondo lilifutwa na Sheria ya Wanyamapori ya
mwaka 2009
Mwaka 2009, Sheria mpya ya wanyamapori ilitungwa ambapo pia ilifuta Sheria ya Uhifadhi
wa Wanyamapori ya mwaka 1974. Mabadiliko ya Sheria ya Wanyamapori yalibadili hadhi ya
mapori tengefu na kuondoa shughuli zote za kibinadamu kama ilivyokuwa awali. Sheria hii
kwa kutambua kuwa maeneo mengi yaliyokuwa na mapori tengefu ni ardhi halali za vijiji
iliweka utaratibu katika kifungu cha 16 (4) na 16 (5) kwa Waziri mwenye dhamana (Maliasili
na Utalii) kufanya mapitio upya na kuondoa mapori tengefu katika ardhi za Vijiji ndani ya
mwaka mmoja baada ya Sheria hiyo kuanza kutumika (“ For the purpose of sub-section 4 ,
The Minister shall ensure that no land falling under the village land is included under the game
controlled areas’ Section 16).
Sheria hii imepiga marufuku shughuli zote za kibinadamu katika maeneo ya mapori tengefu
ambayo kimsingi yalikuwa yamepachikwa katika ardhi za Vijiji kwa kuwa lengo lake lilikuwa
ni kusimamia rasilimali za wanyamapori na sio milki ya ardhi. Tafsiri yake ni kuwa, kwa
kutambua kuwa maeneo mengi karibu asilimia 60 ya mapori tengefu hapa nchini yalikuwa
katika ardhi za vijiji, Bunge ambalo ni muhimili wa kutunga Sheria liliona umuhimu wa
kuondoa mapori tengefu katika maeneo ambayo ni ardhi za vijiji kama ilivyokuwa kilometa za
mraba 4000 za pori tengefu la Loliondo. Bahati mbaya zoezi hili kwa upande wa Loliondo
halikufanyika kama sheria ilivyoagiza, badala yake kumekuwemo na maneno mengi kuwa
bado Loliondo nzima ni pori tengefu kinyume na utaratibu wa sasa wa kisheria ambao
hauruhusu pori tengefu kuchangamana na shughuli za kibadamu.
Matokeo yake ni kwamba kwa mujibu wa sheria ya Wanyamapori ya sasa Loliondo hakuna
tena pori tengefu linalotambulika kisheria. Kwa uchambuzi huu ni wazi kuwa eneo lote la
kilometa za mraba 4000 za Loliondo na Sale ni ardhi halali ya vijiji.
Pamoja na uwepo wa mgogoro wa ardhi ya Vijiji katika Tarafa za Loliondo na Sale kuanzia
miaka ya 1992, mabadiliko hayo ya kisheria yamechochea kasi ya mgogoro baada ya
kutekelezwa kwa jaribio la kutenga eneo halali la Vijiji lenye ukubwa wa kilomita za mraba
1500, kupitia Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya wilaya ambayo ilifadhiliwa na Kampuni ya
uwindaji ya OBC mwaka 2010, kwa lengo la kulinda maslahi yake ya uwindaji katika eneo
hilo. Baada ya wananchi kugundua nia ya Kampuni ya OBC kumegewa ardhi ya Vijiji,
mgogoro mpya uliibuka ambapo Kijiji cha Soitsambu mwaka 2010 kilitoa Notisi ya kusudio
la kumuondoa OBC kwenye ardhi ya Kijiji kwa barua yenye kumbukumbu namba
AR/KJ/55/402/4/1331, kwamba ifikapo mwezi Desemba Kijiji hicho kitakuwa huru kupangia
matumizi mengine katika ardhi hiyo ya Kijiji.
Matokeo ya Mabadiliko ya Sheria ya mwaka 2009 kwa pori tengefu la Loliondo Sheria
iliyokuwa imetambua mapori tengefu ndani ya ardhi za wananchi ilibadili hadhi ya mapori
tengefu na kuondoa shughuli zote za kibinadamu bila kutambua eneo lote la Loliondo na
sehemu ya Sale yalikuwa ni ardhi za vjijiji vilivyokuwa na mapori haya tengefu. Wilaya
zingine za kifugaji ambazo zimekuwa na mapori tengefu ndani ya ardhi ya vijiji ni Pamoja na
Longido, Monduli na Simanjiro na vijjiji vingi katika wilaya hizi vimepatiwa hati za umiliki.
Sheria hii kwa kutambua kuwa maeneo mengi yaliyokuwa na mapori tengefu ni ardhi halali za
vijiji iliweka utaratibu katika kifungu cha 16 (4) hadi 16 (5) kwa waziri kutambua maeneo yote
yenye mapori tengefu yaliyoko katika ardhi za vijiji na kutangaza ndani ya mwaka mmoja toka
baada ya kuanza kutumika kwa sheria hii kuwa yamekosa hadhi ya kuwa mapori tengefu. “
For the purpose of sub-section 4 , The Minister shall ensure that no land falling under the
village land is included under the game controlled areas’ Section 16 (5)”.
Tafsiri yake ni kuwa , kwa kutambua kuwa maeneo mengi karibu asilimia 60 ya mapori tengefu
hapa nchini yalikuwa katika ardhi za vijiji, watunzi wa sheria hii waliona ni muhimu kuondoa
mapori tengefu katika maeneo ambayo yalikuwa ni ardhi za vijiji kama ilivyokuwa kilometa
za mraba 4000 za Loliondo na Sale. Bahati mbaya zoezi hili kwa upande wa Loliondo
halikufanyika kama sheria ilivyoagiza, badala yake pamekuwepo na maneno mengi kuwa bado
Loliondo nzima ni GCA kinyume na utaratibu wa sasa wa kisheria ambao hauruhusu mapori
tengefu kuchangamana na shughuli za kibadamu. Matokeo yake ni kwamba kwa mujibu wa
sheria ya Wanyamapori ya sasa Loliondo hakuna tena pori tengefu linalotambulika kisheria.
Nafasi ya Taratibu za Kimila
Pamoja na kwamba sheria za kikoloni na hata za Tanzania baada ya Uhuru zilitungwa ili
kuweza kusimamia sekta ya ardhi na uhifadhi, ni muhimu kwa wadau wote kufahamu kwamba
Mila, utamaduni na elimu ya asili zimekuwa nguzo kuu na muhimu katika kuendeleza ardhi na
maliasili katika tarafa za Loliondo na Sale. Jamii ya wafugaji wa Kimaasai inategemea mfumo
wa asili wa matumizi ya ardhi unaotegemea misingi ya maarifa, desturi na mila za jadi.
Ardhi inatumiwa kulingana na mahitaji ya pamoja ikiwepo ufugaji, makazi na matambiko.
Kwa utaratibu wa maarifa ya jadi, nyanda za malisho zinasimamiwa kwa aina ya matumizi
kulingana na msimu (kiangazi, masika na kipupwe). Matumizi ya ardhi yanasimamiwa kwa
kutumia mifumo ya asili ya mila na desturi chini ya uratibu na miongozo ya viongozi wa mila
(Ilaigwanak). Mila na desturi ya jamii huzingatia uhifadhi wa mazingira, matumizi ya nyanda
za malisho (maji na malisho) kwa ajili ya matumizi ya mifugo na wanyamapori. Mfumo huu
ulijenga mahusiano mazuri ya asili baina ya wanyamapori, mifugo na watu tangu enzi na enzi.
Mahusiano baina ya mifugo na wanyamapori; mila na desturi ni nguzo kuu katika kuendeleza
wanyamapori na rasilimali za asili katika tarafa ya Loliondo na Sale. Licha ya uendelevu wa
utaratibu huu, mfumo wake wa usimamizi wa ardhi kwa mifumo ya asili ya nyanda za malisho
umekumbwa na migongano mingi ya kisheria na kisera ya uhifadhi wa wanyamapori.
Misimamo ya Baadhi ya Viongozi kuhusu ardhi ya Vijiji Loliondo
Zimekuwepo jitihada hasa zilizoonyesha kwa namna fulani serikali ilikuwa inaashiria kitu gani
pamoja na kwamba ni baada ya makele yaliyopigwa na wananchi wa Loliondo na Sale na
watetezi wa Haki za Binadamu ndani na nje ya nchi. Mfano mojawapo ni andiko la Rais wa
Awamu ya Nne, Mhe Kikwete katika mtandao wa Kijamii wa Twitter akisema kwa kunukuu.
“There has never been, or will there ever be any plan by the Government of Tanzania to evict
the Maasai people from their ancestral land”. Kwa Kiswahili “Hakujawahi kuwa na wala
hakutakuwa na mpango wowote wa serikali wa kuwafukuza watu wa jamii ya Kimaasai kutoka
katika ardhi ya mababu zao.”
Wakati huo huo Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoa msimamo wa Serikali ya Awamu ya nne
kuhusu Loliondo Mei 2013 kwa kuandika barua iliyotambua kuwa pamoja na kwamba nia ya
serikali ni nzuri ukweli unabaki kuwa hii ni ardhi ya Vijiji na ni lazima kujipanga upya kama
serikali kuona ni kwa njia gani maeneo haya yatahifadhiwa bila kuathiri haki za wanavijiji wa
eneo hilo. Barua hii ilisitisha zoezi la kutwaa eneo la kilometa za mraba 1,500 kama ilivyo
tangazwa na waziri wa Maliasili wa wakati huo , Balozi Hamisi Kagasheki. Hi inaonyesha
kuwa serikali ya awamu ya sita inapingana hata na serikali ya awamu iliyopita kuhusu ardhi ya
Loliondo.
Hitimisho
Sio tu viongozi wa awamu zote zilizopita kuanzia Marais, Mawaziri wakuu wameendelea
kutambua kuwa ardhi yenye mgogoro ni ardhi ya vijiji lakini yenye rasilimali za umma
(Wanyama) , lakini hata wananchi wenyewe wanatambua hilo na wamebakia na msimamo huo
kuwa ardhi ni yao. Tunazungumzia kilometa za mraba 4000 maana yake ni ardhi yote ya Tarafa
ya Loliondo ikiwemo mji mdogo wa Loliondo ambapo ndipo kuna makao makuu ya Wilaya.
Sasa sote tujiulize , inawezekanaje kuwa tarafa nzima na sehemu ya tarafa ya Sale kuwa sio
ardhi za vijiji wakati humo humo pamekuwepo na vjiji halali vilivyoanzishwa na kusajiliwa na
serikali na vyenye hati za umiliki wa ardhi?
Kabla ya uhuru wananchi walikuwa wanakalia na kutumia maeneo hayo kimila ambapo
walipata haki ya kisheria na ndiyo maana wakoloni miaka kati ya 1940-1950 walipokuwa
wanataka kuanzisha hifadhi ya Serengeti walikuwa na majadiliano ya muda mrefu na viongozi
wa mila wawakilishi wa jamii na hatimae kuingia makubaliano ya kuhama mwaka 1958,
ambapo inathibitisha pasipo shaka kuwa hiyo ilikuwa ni ardhi yao na walikuwa wakimiliki
kimila.
Vilevile baada ya uhuru, Vijiji hivi vimeendelea kutambuliwa na Serikali kwa kusajiliwa kwa
mujibu wa Sheria mbalimbali ikiwa ni pamoja na Sheria ya Serikali za Mitaa [Mamlaka za
Wilaya] Na.7 ya mwaka 1982, kupimwa na kupatiwa hati/vyeti kwa mujibu wa Sheria za ardhi
ya mwaka 1923, na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na.5 ya mwaka 1999. Soma zaidi sura ya pili ya
taarifa hii. Ni muhimu serikali na jamii ya watanzania kuelewa kuwa kihistoria eneo hili
halikuwahi kuwa wazi tangu enzi za mababu, wakati wa Ukoloni, baada ya Uhuru hadi sasa.
Kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuwa eneo la Loliondo sio ardhi ya vijiji inapotosha na
huenda amepotoshwa pia kuhusu uhalali wa ardhi ya vijiji vya Loliondo na Sale.
Serikali itangaze rasmi kuwa ardhi za vijiji vilivyokuwa na mapori tengefu kabla ya sheria ya
mwaka 2009 kwa sasa havina hadhi tena ya mapori tengefu ili kuondoa usumbufu unaondelea
kwa sasa . Vilevile sheria hii inatarajiwa kuibua migogoro katika maeneo mengi nchini kwa
kuwa mapori tengefu yalianzishwa katika ardhi za Vijiji vilivyosajiliwa, kupimwa kupata hati
za ardhi/Vyeti vya ardhi za Vijiji na kufanya Mipango ya matumizi ya ardhi. Aidha kwa tafsiri
ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na.5 ya mwaka 2009 katika kifungu cha 16(5), hakuna
pori tengefu lolote Loliondo kwa kuwa haikuwahi kutangazwa kwenye Gazeti lolote la Serikali
(GN) tangu kuanza kutumika kwa Sheria hiyo.
Kinachoonekana kwa sasa ni kuwa serikali inakwepa kuanzisha mchakato wowote wa kisheria
na kushirikisha wananchi endapo wanahitaji hizo kilometa za mraba 1,500. Wanatambua kuwa
kuchukua hilo eneo la vijiji kwa utaratibu wanaotumia sasa wa kusema tunawagawia ardhi
kilometa za mraba 2,500 kutoka kwenye kilometa za mraba 4000 hakutakuwa na gharama
zozote za fidia. Wananchosisitiza wananchi wa Loliondo ni uwepo wa meza ya majadiliano ili
kutoa nafasi ya kutatua mgogoro huu. Nashauri Serikali chini ya Uongozi wa Mama Samia
waondoe vikosi Loliondo na kurudi kwenye meza ya majadiliano na jamii kuhusu namna ya
kuhifadhi maaeneo ya Loliondo. Michakato hii izingatie haki za binadamu na ushirikishwaji
mpana wa wananchi ambao ni wakazi wa maeneo hayo.

Wakili Onesmo Kasale Olengurumwa, Mwanaloliondo- 8/6/202