March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

”TUSITOZE KODI KUBWA BIASHARA ILIYOGEUKA KUWA HUDUMA YA JAMII,”OLENGURUMWA

Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa ameipongeza nia ya serikali katika kubuni njia za mapato kwa taifa ili kuboresha huduma za kijamii na kama watetezi wa haki za binadamu wanaunga mkono jitihada zote zinazolenga kumfikia mtanzania kwa huduma za msingi na maendeleo.

Olengurumwa amesema hayo hapo jana wakati alipokuwa akichangia mjadala kuhusu faida na Athari za makato mapya ya kodi ya miamala ya simu katika kipindi cha Mizani ya Wiki kinachorushwa na Kituo cha runinga cha Azam TV.

Amesema pamoja na kuwa nia ya serikali ya kuweka tozo hiyo ni nzuri na ya kwenda kuboresha huduma za kijamii lakini ushirikishwaji wa watanzania katika mchakato wa upatikanaji wa sheria hiyo ulikuwa ni mdogo.

“Changamoto naona hasa ni pale wananchi wanapojikuta hawakushirikishwa katika kufikia maamuzi haya na hawakuandaliwa kwa hili,” amesema na kuongeza kuwa mjadala kuhusu gharama za tozo hizo uliopo ungefanyika walau mwezi mmoja kabla ya kupitisha sheria huenda sheria hiyo ingepitishwa katika jicho lingine.

Katika mjadala huo Olengurumwa ameishauri serikali kuwa kuwa miamala ya simu kwa sasa imekuwa ni huduma muhimu kwa watanzania na haipaswi kuongezewa kodi na tozo hizo pengine zingeozeka kwa kiwango kidogo tofauti na ilivyo sasa.

“Uhusishwaji wa kifedha kwa watanzania (Financial inclusion) katika mfumo wa kifedha umeendelea kukua toka mwaka 2006.Target ya BOT ilikuwa ni kufikia asilimia 80 lakini sasa hivi tunapozungumza karibu asilimia 90 watanzania wengi wameingia kwenye mfumo rasmi wa kifedha,” ameeleza Olengurumwa.

Aidha Olengurumwa amesema serikali ingeweka Kiwango cha fedha cha kuanza kukatwa tozo angalau kianzie miamala ya laki tano ili kutowatoa watanzania wa chini kwenye mzunguko rasmi wa kifedha na kuishauri serikali kupunguza kiwango cha kodi kilichopo kwani makato yaliyowekwa ni makubwa.

“Benki zina watanzania hata asilimia 5 hawafiki lakini baada ya kuja mfumo wa simu wengi wameingia katika mfumo rasmi wa kifedha,”ameongeza.

Ameongeza kuwa athari za ongezeko la tozo hizo linaweza kupelekea madhara ya kikodi na kupelekea watu wapunguze kutumia miamala ya simu na kuanza kubeba fedha taslimu na kupelekea wizi na ujambazi suala ambalo serikali lilifanikiwa kulidhibiti huko nyuma.