March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA YATEMBELEA OFISI ZA THRDC, YASISITIZA KUENDELEZA USHIRIKIANO

Na: Anthony Rwekaza

Tume ya Haki za Binadamu na utawala bora, imetembelea ofisi ya Mtandao Kitaifa wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania(THRDC), na kufanya mazungumzo na Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao huo Onesmo Olengurumwa kabla ya kutembelea vitengo mbalimbali kwenye Ofisi hiyo kuona wanavyotekeleza majukumu ya kutetea haki za binadamu.

Matembezi hayo yameongozwa na Kamishina wa Haki za Binadamu Nyanda Shuli pamoja na watendaji wengiine wa tume hiyo ambao wamepata pia fursa ya kuelezwa mtandao huo unavyofanya kazi, ukiwa na wanachama zaidi ya 200 Nchini Tanzania.

Akizungumza na vyombo vya habari baada ya matembezi hayo Kamishina Nyanda Shuli amesema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imekuwa ikifanya kazi na Mtandao wa THRDC na wadau wengine ambao ni Watetezi wa Haki za Binadamu.

“Tumetembelea mtandao wa THRDC Leo ambavyo imekuwa kawaida yetu kutembelea wadau ambao tunafanya nao kazi kwa karibu sana , tukili kwamba sisi Haki za Binadamu na Utawala Bora tunafanya kazi kwa ushirikiano na wadau wote ambao pia ni Watetezi wanatetea Haki za Binadamu kwahiyo kwetu ni wadau tunaofanya kazi na tunapenda kuendelea kufanya nao kazi.” Amesema Kamishina wa Haki za Binadamu na Utawala Bora, Nyanda Shali

Pia Kamishina Nyanda Shuli akiwa Ofisini hapo, amepata kugusia juu ya kauli za Rais Samia Suluhu Hassan alizozitoa jana akizitika mamlaka za dola kutenda haki kwa watuhumiwa wote bila kuvunja sheria, amepongeza amempongeza na kudai kuwa watayafanyia kazi maelekezo hayo kwa kushirikiana na mamlaka nyingine ambazo Rais amezitaja kwenye hotuba yake kwa kushirikiana na wadau wengine ili kukuongeza nguvu ya upatikanaji wa haki kwa kila mtu.

“Maelekezo ya Mh. Rais Samia Suluhu Hassan kwa upande wetu ni mambo ambayo ni ya muhimu kufanyia kazi tutakaa chini kuangalia maeneo mengine ambayo tunaweza tukaongeza nguvu na kuongeza namna ambayo tutashirikiana na wadau wengine ambao amewataja moja kwa moja ili kwa pamoja tukiunganisha nguvu tuweze kusaidia Nchi yetu kufikia hatua ya haki ambayo Kila mtu atatenda wajibu wake” amesema Kamishina wa Haki za Binadamu, Nyanda Shuli