February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

TOZO ZA MIAMALA “Serikali ni sikivu kama kuna ugumu itaona namna bora”Dk Saada Mkuya

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar, Dkt Saada Salum Mkuya amsema serikali kabla ya kuweka tozo za miamala ya simu iliangalia sehemu ambayo inaweza kupata kodi nyingine kutokana na changamoto za uchumi wa nchi na mwananchi mmoja mmoja ambazo huenda imesababishwa na covid-19 au uchumi wa dunia na tozo hizo ni kwa nia njema ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Kwakuwa serikali inataka kuweka maendeleo zaidi propably tungeangalia hiki kiasi tungeweza kupima effect yake kwa wananchi lakini serikali ni sikivu ikiona kama kuna ugumu fulani na pengine kuna mzigo itazingatia namna bora ya kufanya,”ameeleza Dk Saada.

Dkt Saada amesema hayo hapo jana Katika kipindi cha Mizani ya Wiki kinachorushwa na Azam TV kilicholenga kujadili Faida na Athari za makato mapya ya kodi za miamala ya simu mjadala ambao umewakutanisha pamoja na Mratibu THRDC,Wakili Onesmo Olengurumwa na Mtaalamu wa Masuala ya Fedha kutoka Chuo cha CBE, Dkt Nasibu Mramba.

Katika mjadala huo Dkt Saada amesema wabunge ni wawakilishi wa wananchi hivyo yale ambayo yamezungumzwa na kujadiliwa bungeni kuhusu sheria hiyo ni mawazo ya wananchi wanaowawakilisha.

“Wabunge wanapoingia bungeni wanaingia kuwawakilisha wananchi manake anachotakiwa akizungumze anakuwa ni kwa niaba ya wananchi na kama hilo jambo limetolewa na halikuwa ‘communicated’ manake isije kuwa wananchi hawajashirikihwa kwasababu tunayempa pale ni wawakilishi wa wananchi…ina maana wale ambao wamelileta wamejadili manake ni kwamba wamechukua mawazo ya wananchi,”amesema.

Kwa upande wake Mratibu wa THRDC,Onesmo Olengurumwa ameeleza kuwa uandaaji wa sheria ambazo zinawagusa watanzania wote moja kwa moja unahitaji kuwashirikisha wananchi Zaidi ya Bunge.

“Tuangalie tunapotunga sheria zetu,tozo hizi unapotuma na kutoa pesa ongezeko ni kubwa limekuwa ni maradufu lakini ushirikishwaji wa watanzania umekuwa mdogo,”amesema Olengurumwa na kuishauri serikali kupunguza kiwango cha makato ya tozo hizo kwani ni biashara ambayo imegeuka huduma.

Naye Mtaalamu wa Masuala ya Fedha kutoka Chuo cha CBE,Dkt Nasibu Mramba amesema kuwa kulihitajika elimu kubwa kwa wananchi kuhusu tozo hizo ili kuwaaandaa kisaikolojia isingekuwa kwa ghafla kama ilivyokuja.

“hili suala lina pande mbili tunafahamu nchi zetu haziwezi kuendelea kutoka kwa wengine kwahiyo serikali ikaona ije na tozo hii ili hela itakayopatikana iende kulipia shughuli za maendeleo,lakini upande mwingine watu wamepunguziwa kile walichokuwa nacho kwahiyo watu lazima walalamike,waumie sio kwamba kimechukuliwa kidogo kimechukuliwa kikubwa kwelikweli,” ameeleza Dkt Mramba.

Pia amesema tozo hizo zinaweza kupelekea kupungua kwa ajira kwa mawakala wenye mitaji midogo na pia itapunguza kiasi cha fedha kwa wananchi hali itakayopelekea kupungua kwa uwezo wa kufanya manunuzi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar, Dkt Saada amesema Bunge la Tanzania linaendeshwa kwa demokrasia na iwapo suala hilo halipo sawasawa wanaweza wakalipinga na kutoa namna bora ya jinsi ya kufanya.

“Katika hali ya kawaida hakuna mtu anapenda kulipa kodi lakini tuangalie ile kodi ambayo itakuwa mtu hawezi kuifeel … kodi ambayo pengine haitokuwa sasa uongeze mzigo…. tuangalie both ways ….Kuona kwamba hili jambo linakuwa kwa urahisi Zaidi,”amesema.