February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

TIGRAY YAKUMBWA NA BAA LA NJAA

Baadhi ya maeneo yaliyofikiwa na misaada

Watu 350,000 katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia wanakabiliwa moja kwa moja  na baa la njaa huku mamilioni wengine wakiwa katika hatari ya kukubwa na kadhia hiyo kutokana na mgogoro uliodumu kwa muda mrefu katika eneo hilo.

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa mataifa inasema kuwa janga hilo ni baya zaidi kuwahi  kutokea baada ya lile lililoikumba Somalia mwaka 2010 hadi 2012 na kuua karibu watu milioni moja, wengi wao wakiwa Watoto.

Mkuu wa kitengo kinachoshughulikia masuala kibinadamu katika Umoja wa mataifa Mark Lowcock  amewaambia wawakilishi kutoka umoja wa nchi za G7 kuwa hali ni tete katika jimbo hilo na msaada wa haraka unahitajika kabla ya hali kuwa mbaya zaidi,jambo ambalo ameongeza kuwa linaweza kuzuilika kwa maamuzi ya haraka.

Shirika la kilimo na chakula la umoja wa mataifa,Mpango wa chakula duniani,Pamoja na  UNICEF wamesema watu milioni mbili wanaweza kupoteza Maisha kwa kukosa chakula endapo hawatasaidiwa haraka huku mashirika mengi chini ya umoja huo yakikabiliwa na ukata wa fedha.

Hata hivyo mkuu wa Mpango wa Chakula Duniani David Beaslay amelalamika kuwa kuna baadhi ya maeneo ya Tigray hayatafikiwa na misaada kutokana na uwepo wa vikundi vya wapiganaji vyenye silaha vinavyozuia watu kufika maeneo hayo.

Serikali ya Ethiopia ilianzisha mashambulizi ya kijeshi katika eneo la Tigray dhidi ya wafuasi wa Chama cha Ukombozi wa Tigray  (TPLF) eneo la Kaskazini mwa nchi hiyo katika mgogoro iliohusisha  pia nchi Jirani ya Eritrea.