February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

THRDC,MPC YAWANOA WANAHABARI KUHUSU KURIPOTI TAARIFA ZA CHANJO YA UVIKO-19

Na Hilder Ngatunga

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Dkt  Thomas Rutachunzibwa amewataka wananchi watoe hofu kuhusu chanjo za uviko-19 kwani chanjo hizo ni salama.Dkt Rutachunzigwa amezungumza hayo katika mjadala ulioandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania THRDC na Klabu ya waandishi wa Habari Mwanza (MPC) uliofanyika hii leo kwa njia ya mtandao ukiwa na lengo la kuwaongezea ujuzi wanahabari namna ya kuripoti kuhusu chanjo ya uviko-19.

PICHA : Dkt Thomas Rutachunzibwa,Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza

Dkt Rutachunzibwa amesema Tanzania inao wataalamu waliobobea katika masuala ya afya na wamefanya mapitio ya chanjo hizona kuidhinisha chanjo za aina tano kutumika nchini ikiwemo ya AstraZeneca, Pfizer, Johnson and Johnson na zingine na kusema kwasasa chanjo hizo bado wanaendelea kuzitafiti kama zitafaa kutumika kwa wajawazito ikibainika hazitakuwa na madhara kwa kiumbe aliyeko tumboni ila kwa wamam wanaonyonyesha wanaruhusiwa kupata chanjo.

“Chanjo zote zinapokuja huwa kuna kuwa na ‘doubt’, wananchi kudoubt  sio tatizo ila sisi tunatoa taarifa sahihi.Dawa zote tunazotumia hakuna dawa ambayo haina maudhi madogomadogo,faida za dawa hiyo zinakuwa ni kubwa kuliko side effects mfano dawa inayokusababishia kizunguzungu ina faida kubwa sana ya kukutibu” amesema Dkt Rutachunzibwa

Kwa upande wake Dkt Derrick Nyasebwa ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Uhuru  amesema kwamba lengo kubwa la chanjo ni kupunguza vifo na madhara ya muda mrefu na kueleza kuwa kupata chanjo ya uviko-19 haimaanishi kwamba mtu hatopata maambukizi lakini hutapata ugonjwa mkali tofauti na yule ambaye hajapatiwa chanjo kabisa

“Watu wengi wanadhani kuganda kwa damu inatokana na chanjo, lakini madhara mengine ya covid-19  ni kuganda kwa damu ambapo unaweza ukapata stroke na matatizo mengine,tuwe makini tunapojaribu kutupia mizigo kwenye chanjo na hakuna ripoti ya moja kwa moja watu hao walifariki kutokana na kuganda kwa damu,” ameeleza

Aidha ameongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizofanyika zinaonyeshakuwa kati ya watu Milioni moja watu 7 walikutwa na matatizo ya kuganda kwa damu ambapo ni sawa na asilimia 0.0006 ambacho ni kiwango kidogo na kuongeza kuwa chanjo zinasaidia katika kupunguza hatari ya kifo kwa asilimia 85.

Kwa pamoja wataalamu hao wa afya wamewataka wananchi kuepuka taarifa zisizo sahihi kuhusu ugonjwa wa uviko-19 na kuongeza kuwa hakuna uthibitisho wa kisayansi unaaonyesha kuwa kitu cha chuma kama kijiko kinaweza kunaswa katika eneo ambalo mtu amechanjwa chanjo hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkpoani Mwanza (MPC),Edwin Soko amewaasa waandishi wa habari nchini Tanzania kuhusisha vyanzo sahihi katika taarifa zao kwa kuwatumia wataalamu wa afya watakao toa taarifa sahihi kuhusu chanjo yauviko-19 pamoja na kuongeza thamani za taarifa zao.

“Msingi wa chombo cha hbari ni kujenga, zinapokuja taarifa zenye kutia hofu si jambo jema kwa jamii. Yawezekana chanjo ina madhara labda kwa kiasi gani mfano usipochomwa chanjo madhara ni asilimia Fulani na ukichomwa madhara ni asilimia hii. je hizi data tulikuwa tunaziona kwenye vyombo vya habari?Je tunawapa watu gani madaktari wenye taaluma au tunawapa wanasiasa wazungumze kisiasa kuhusu ugonjwa huu,”amesema Soko.

Aidha  Mkurugenzi wa Baraza la Vyombo vya habari nchini Kenya,Victor Bwrie amesema nchini Kenya waandishi wa habari wamefanikiwa pakubwa kutoa elimu kuhusu chanjo ya ugonjwa huo kwa kushirikiana na serikali na wananchi wengi wapo tayari kupatiwa chanjo hiyo na kama Baraza waliandaa jarida la maelekezo kwa waandishi wa habari juu ya kuripoti kuhusu janga hilo.

“waandishi wa habari wengi tuliwapa maelekezo kwamba wawasikilize sana wataalamu ambao wanajua nini kinafanyika kwasababu huu ugonjwa ni mpya na sisi hatujui chochote na pindi covid-19 ilipoanza tulikuwa tunafanya na serikali moja kwa moja na kamati au waziri wa afya kwamba habari za covid zilikuwa zinatolewa kila siku na rais au waziri wa afya,”amesema Bwire

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi THRDC, Vicky Ntetema wakati akifungua rasmi mafunzo hayo amesema mafunzo hayo kwa wanahabari kuhusu chanjo ya uviko-19 ni muhimu sana katika kupata taarifa sahihi kuhusu chanjo hizo.

“Huu ni ugonjwa mpya na kwasababu ni janga lakini pia watu wengi wanapoteza maisha sasa tusipokuwa na taarifa sahihi watu wataendelea kupoteza maisha sasa tufahamishwe chanjo zitatusaidiaje.”amesema Ntetema akisisitiza kuwa waandishi wa habari wanapaswa kuwa na taarifa sahihi kuhusu chanjo ya uviko-19 ili waweze kuisaidia jamii.

Vicky Ntetema,Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi THRDC