March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

THRDC:”KAULI YA SAMIA KUHUSU MAHABUSU NI DHAMANA YA BUNGE”.

Na Leonard Mapuli.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umepongeza hatua  na misimamo anayoonesha Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan dhidi utekelezaji wa haki za Binadamu,hatua inayotokana na kauli ya Rais aliyoitoa wakati wa Uzinduzi wa Semina ya wakuu mbalimbali wa Polisi nchini mnamo Agosti 25 jijini Dar es Salaam, kuhusu mlundikano wa Mahabusu katika magereza na vituo vya polisi kwa upelelezi kutokamilika,ambapo jeshi hilo ndilo lenye dhamana ya upelelezi wa madai yote ya jinai.

“Naomba mkae na wadau wengine muangalie uwezekano wa kurekebisha sheria ya kuweka mtu mahabusu, kwenye nchi za wengine za wenzetu, mtu hakamatwi mpaka upelelezi ukamilike”,ni kauli ya Rais Samia aliyitoa kwa maafisa wa polisi,ambayo inaungwa mkono na Mtandao huo wa Watetezi wa Haki za Binadamu ambao kwa nyakati tofauti umekuwa mstari wa mbele katika kupigia Haki kwa wafungwa,na Mahabusu kupewa dhamana.

Katika mazungumzo yake na wandishi wa Habari ofisi za Makao Makuu ya Mtandao huo,Mratibu wa kitaifa Onesmo Olengurumwa,amesema kitendo cha Rais kusikika zaidi ya mara moja akizungumzia masuala ya watu kubabmbikwa kesi,kuchelewesha kwa upelelezi,na utendaji haki kutoka kwa mahakama,kunatoa mwanga wa Haki za Binadamu kutamalaki.

“Sasa ni zaidi ya mara nne, Rais amezungumza masuala ya kuwepo kwa haki jinai Tanzania,amezungumzia kuhusu kuwepo kwa mifumo  ambayo haitawaumiza watanzania ambao wanatuhumiwa kwa makosa mbalimbali na wapo mahabusu”,amesema Olengurumwa.

Aidha kwa mujibu wa Taarifa ambazo Mtandao huo umekiri kuzikusanya kutoka vyanzo mbali mbali, asilimia 90% ya watu waliopo Magerezani ni mahabusu,na kesi zao bado zinaendelea,huku idadi iliyobaki ndio wanaotumikia vifungo mbalimbali.

“Tulishasema miaka mingi na tumekwenda hadi mahakamani ambako kesi mbalimbali zilifunguliwa,mfano kesi ya Wakili Sanga iliyokuwa inataka kuwepo  dhamana kwa makosa yote,na mahakama kuu ikaridhia maombi yale,lakini mahakama ya rufaa ikaenda kutengua,kuna kesi ambayo mimi na wadau wengine tumefungua tukitaka ule utaratibu wa kupeleka watu kwenye mahakama ambazo hazina uwezo wa kusikiliza kesi zao,mfano pale Kisutu,ni sababu inayopelekea kesi nyingi kuchukua muda mrefu”,ameongeza Olengurumwa ambae pia ni wakili wa mahakama kuu ya Tanzania.

Tamko la Rais limezitaka mamlaka mbali mbali za kisheria kuona namna ya bora ya kufanya watu kutokaa mahabusu kwa muda mrefu wakisubiri uchunguziwa kesi zao kukamilika,hali inayolalamikiwa sana na wadau wa masuala ya Haki za binadamu hasa pale watuhumiwa wanapokuja kuachiwa huru baada ya miaka mingi ya kusota mahabusu bila hata Mahakama kuwafidia,huku wengine wakihukumiwa kutumikia vifungo vya muda mchache jela,kuliko muda waliokaa wakiwa mahabusu.

Aidha mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu,una matarajio makubwa kuwa kauli ya Rais itazifikia mamlaka za mabadiliko ya sheria za jinai likiwemo  bunge, na endapo yatafanyiwa kazi vilivyo,itasaidia kupunguza  makosa yasiyokuwa na dhamana,ili magereza zibaki na wafungwa pekee.Mtandao pia umezitaka Mamlaka za Mabadiliko ya sheria kuweka bayana kuwa watu wanaokwa mahabusu muda mrefu na baadae kuthibitika kuwa hawana hatia,kuwe na utaratibu wa fidia kwa sababu ya mtu kupotezewa muda wake mwingi na kukatisha shughuli zake mbalimbali za uzalishaji.