March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

THRDC-ZANZIBAR,MAHAKAMA, KUFANYA KAZI PAMOJA ENEO LA HAKI ZA BINADAMU

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania tawi la Zanzibar,ukishirikiana  Mahakama Kuu Zanzibar,wameandaa mafunzo ya siku mbili,yaliyoanza leo Novemba 27,yanayowakutanisha Majaji mbalimbali,na mahakimu wanaofanya kazi Zanzibar, kujadili masuala mbali mbali yanayohusu utekelezaji wa haki za binadamu visiwani humo,kwa kuzingatia kuwa,makundi hayo mawili (Majaji na Mahakimu) ndiyo yanahusika na utoaji wa haki mbalimbali, baada ya kusikiliza kesi ama malalamiko na kuyatolea maamuzi kwa mujibu wa sheria.

Mafunzo hayo yanayofanyika katika Hotel ya Golden Tulip iliyopo Kiembe Samaki,yamehudhuriwa pia Majaji wastaafu,akiwemo Jaji Mstaafu Joaquine De Mello,ambae amestaafu Rasmi hapo jana Novemba 26 kama Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Wengine waliohudhuria mafunzo hayo ni Chuo cha Mafunzo Zanzibar (Jeshi la Magereza),Polisi,ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa serikali (DPP) upande wa Zanzibar,pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Mafunzo hayo yamefunguliwa na Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar, Hamis Ramadhan,ambae pamoja na mambo mengine,amewataka Majaji na Mahakimu kutoa haki kwa kuzingatia weledi,uwazi,uwajibikaji na muda.

Jaji Ramadhani pia amekemea vitendo mbalimbali vinavyolalamikiwa na wananchi juu ya mfumo wa mahakama ikiwemo rushwa,uchelewashwaji kesi,pamoja na kutopatikana kwa nakala za hukumu baada ya kesi mbali mbali kumalizika.

Haya ni Mafunzo ya kwanza kuratibiwa na THRDC tawi la Zanzibar,ambapo Mratibu wa Mtandao huo Abdallah Abeid amezitaka mahakama visiwani humo, kushirikiana na Mtandao huo, uliosogeza Zaidi huduma zake visiwani humo,huku Mratibu wa Kitaifa Wakili Onesmo Olengurumwa,akisisitiza umuhimu kwa wadau wa sheria na utoaji wa haki zikiwemo mahakama, kushirikiana  kwa pamoja katika utekelezaji wa Haki za Binadamu visiwani Zanzibar.