Mstahiki Meya jimbo la Zanzibar Mjini,Mahmoud Musa ameupongeza Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu tawi la Zaznibar kwa juhudi inazoonyesha katika utoaji wa elimu kuhusu masuala ya utetezi wa haki za binadamu.
Pongezi hizo zimetolewa hii leo wakati akifungua semina ya siku mbili iliyoandaliwa na THRD-Zanzibar,ambapo wadau takribani wa 50 mashirika ya Asasi za Kiraia kutoka Unguja na Pemba wanajengewa uwezo kuhusu namna ya kufuatilia, kuripoti matukio ya haki za binadamu na utunzaji wa kumbukumbu wa taarifa hizo.Mafunzo haya yameanza hii leo Machi 15,2022 na yatahitimishwa hapo kesho yanafanyika katika Hoteli ya Golden Tulip,Zanzibar.
Mahmoud amesema Serikali ya Zanzibar inatambua umuhimu wa mchango wa Asasi za Kiraia (AZAKI), mashirika ya haki za binadamu na sekta binafsi kwa ujumla katika kutetea na kukuza haki za binadamu,hasa kwenye ukusanyaji wa taarifa pamoja na utoaji wa huduma kwa jamii pindi haki hizozinapovunjwa.
“Tunaunga mkono juhudi za Mtandao wenu na Asasi za Kiraia kwa ujumla katika kuwapatia mafunzo haya. Vilevile kuwajengea uwezo wa namna bora ya kuendesha shughuli za utetezi wa haki za binadamu kwa kushirikiana na serikali,”amesema Mahmoud akiongeza THRDC-Zanzibar imekuwa ikishirikiana na serikali katika utekelezaji wa kazi zake kwa maslahi ya jamii.
Mahmoud amesema anaamini utolewaji wa mafunzo hayo utaendelea kuimarisha ushirikiano baina ya watetezi wa haki za binadamu na serikali hususan katika kulinda na kukuza haki za binadamu visiwani humo na kutoa wito kwa wadau wa AZAKI kutumia elimu watakayoipata kutoka katika mafunzo hayo.
“Natoa wito kwenu nyote, muendelee kuchukua na jitihada hizi, na sisi kama serikali tutaendelea kuwapa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa kazi zenu,”
Kwa upande wake Mratibu wa THRDC tawi la Zanzibar,Abdallah Abeid amesema tangu kusajiliwa kwa Mtandao huo visiwani humo mnamo mwezi Septemba mwaka jana wamekuwa wakifanya kazi kubwa na wamekuwa wakishirikiana na serikali katika utekelezaji wa shuguli zao.
“Leo mtapata fursa ya kupata wale wataalam wanaofanya mapitio ya changamoto za kimahakama na mtapata fursa ya kutoa maoni yenu kuhusiana na changamoto mbalimbali za kimahakama na bahati nzuri tupo pamoja na serikali katika kuhakikisha kwamba mikakati yenu yote kama wanachama wa mtandao hapa Zanzibar inapata ushirikishwaji mkubwa wa serikali,” amesema.
Aidha amewaasa washiriki wa mafunzo hayo kutumia fursa ya kukaa karibu na kushirikiana na serikali katika kupeleka taarifa za matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
“Katika kuunga mkono kazi za taasisi mbalimbali zinazohusiana na maswala ya haki basi, tuliunga mkono pia ile sheria mpya ya rushwa na uhujumu uchumi kwa kufanya ‘validation’ tulileta wadau mbalimbali kujadili kutoa maoni yao ambayo sasa hivi ipo kwenye Tume ya mabadiliko ya sheria hapa Zanzibar ambayo pia tunafanya nao kazi kwa karibu sana na kwa bahati nzuri tumebahatika pia kusaini Mkataba wa Makubaliano maalum yaani ‘MoU’na mahakama kuu ya Zanzibar katika kufanya kazi zetu”ameongeza Abdallah.
Naye Mratibu wa Kitaifa wa THRDC,Onesmo Olengurumwa ameeleza kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya AZAKI kuhusu namna ya kufuatilia na kutoa taarifa zinazohusu haki za binadamu ili kuweza kutatua changamoto mbalimbali za haki za binadamu visiwani humo ikiwemo maswala ya udhalilishaji, madawa ya kulevya na maswala yote yanayohusu haki za wanawake na watoto.
“Bahati nzuri tupo pamoja na serikali katika kuhakikisha kwamba mikakati yenu yote kama wanachama wa mtandao hapa Zanzibar inapata ushirikishwaji mkubwa wa serikali kwasababu kila mnachokifanya mwisho wa siku anayetakiwa kukitekeleza na kubadilisha sera au sheria ni serikali, tuendelee kutumia fursa ya kukaa karibu na kushirikisha serikali na kupeleka taarifa za ukwikwaji wa haki za binadamu na wakati huo huo kukosoa pale ambao kuna changamoto zinazojitokeza kuhusu haki za binadamu”amesema Olengurumwa.
Pia ameongeza kuwa anatumai mafunzo haya yatawajengea uwezo kuhusu namna ya kufuatilia,kuhifadhi na kusambaza taarifa za haki za binadamu kwani wao ni jeshi kubwa linalofuatilia na kulinda haki za binadamu kwa niaba ya serikali kwa mujibu wa katiba na mitandao ya kimataifa au (standard)
“Tunashukuru kwamba maeneo ya udhalilishaji mmekuwa mkifanyia kazi muda mrefu na Mh. Rais Mwinyi amefanya kazi vizuri sana tumeanza kuona matokeo, kwahiyo nadhani kazi yenu mkifanya vizuri viongozi wanasikia na kufanyia kazi,”amesema Olengurumwa.
Aidha Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania,Jaji Joacquine De mello amewasa watetezi wa haki za binadamu kusemea haki za wengine pale zinapovunjwa na kueleza kuwa anaamini taasisi ambazo zinapatiwa mafunzo zitakwenda kuwafundisha wengine ili kuongeza uelewa Zaidi kuhusu masuala ya ufuatiliaji na uandishi wa ripoti za haki za binadamu.
Habari Zaidi
DCI KINGAI ASISITIZA WAZAZI KUZINGATIA MALEZI BORA KWA WATOTO WAO ILI KUPUNGUZA UKATILI
THRDC,C-SEMA YAENDESHA MAFUNZO KWA POLISI NA WAENDESHA MASHITAKA