February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

THRDC YAWAONGEZEA UWEZO MAWAKILI WANAWAKE KUHUSU NAMNA YA KUENDESHA MASHAURI YENYE MASLAHI YA UMMA

Mwenyekiti wa Cha cha Majaji  Wanawake Tanzania (TAJWA) ,Jaji Joaquine De mello amesema ushiriki wa mawakili wanawake katika kuendesha mashauri yenye maslahi kwa umma ni mdogo ukilinganisha na idadi ya wanaume wanaoshiriki katika kuendesha mashauri hayo huku akitaja mitazamo hasi kwa jamii kuhusu mwanamke ni mojawapo ya sababu inayopelekea hali hiyo.

Jaji De mello amesema hayo hii leo jijini Dar es salaam  wakati akifungua warsha ya siku mbili ya kuwaongezea uwezo wanawake mawakili wa haki za binadamu juu ya namna ya kuendesha mashauri yenye maslahi ya umma, warsha ambayo imeandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).

Jaji Joaquine De mello wakati akifungua warsha ya siku mbili iliyoandaliwa na THRDC hii leo

“Sote tunatambua umuhimu wa mwanamke na uwezo mkubwa alionao katika ujenzi wa jamii bora. Tena katika kada yetu ya sheria kazi nzuri za sisi mawakili na mahakimu wanawake zenye matokeo chanya katika jamii zinajionyesha zenyewe. Sio tu katika ushiriki wa moja kwa moja katika kesi za maslahi ya umma bali pia katika kuongoza taasisi zinazosimamia kesi za aina hii. Mawakili wanawake wanaoshiriki katika kesi za maslahi ya umma kwa uchache wao, wameonyesha kiwango cha juu cha ujuzi na uwezo pamoja na changamoto zote zinazowakabili. Hivyo basi nitoe wito kwa mawakili wengine kufuata nyayo zao,” amesema.

Aidha ameongeza kuwa Kesi zenye maslahi ya umma zimekua moja ya njia nzuri ya kuhamasisha kukomesha ukiukwaji wa haki za binadamu unaoathiri umma kiujumla na kuwataka mawakili wanawake kujitokeza na kushiriki katika undeshaji wa kesi hizo.

“Mpaka kufikia mwezi Machi mwaka huu, jumla ya mawakili wanawake 3055 walisajiliwa nchini, lakini wanoshiriki katika kesi za maslahi ya umma bado ni wachache. Hali hii imeonekana kujitokeza pia katika Mahakama ya Afrika Mashariki, mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu, pamoja na Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (ACHPR),”

Kwa upande wake Meneja Programu kutoka THRDC,Remmy Lema amesema wanawake mawakili wanatakiwa kujengewa uwezo ili waweze kushiriki katika kuendesha kesi zenye maslahi ya umma.

Meneja Program kutoka THRDC,Remmy leo akitoa hotuba ya ufunguzi katika warsha ya kuwaongezea uwezo mawakili wanawake kuhusu namna ya kuendesha mashauri yenye maslahi ya umma

“Lengo kuu la mafunzo haya ni kuona kweli kuna mawakili wanawake wanashiriki katika kuendesha kesi hizi na zinafanikiwa,pia tutapata nafasi ya kuweza kutafakari ni kesi zipi zipo ‘pending’ na kwa namna gani ambavyo mawakili wanawake tunaweza tukajiengage katika hizo kesi kuhakikisha kwamba tunakuwa sehemu ya usimamizi wa hizo kesi,” ameeleza Lema.

Naye Afisa kutoka THRDC, Wakili Leopold Mosha (Protection Officer) amesema THRDC inatoa mafunzo hayo ili kupunguza changamoto ya ushiriki wa mawakili wanawake katika kuendesha kesi zenye maslahi ya umma.

“changamoto kubwa ni mawakili wanawake wanaoshiriki katika kesi zenye maslahi ya umma wamekuwa ni wachache zaidi kuliko wanaume, sasa ili kujaribu kupata ufumbuzi wa tatizo hilo tumeanza sasa kufanya mafunzo kwa mawakili wanawake ambao watakuwa wanashiriki katika kesi hizo,” ameeleza Wakili Mosha.

Aidha Jaji De mello ameupongeza Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania kwa kuandaa mafunzo hayo pamoja na kutoa juhudi inyoonyesha katika utoaji wa elimu  kusimamia dira na maono yake katika utetezi bora wa haki za binadamu nchini. “niseme tu kwamba nawapongeza wadau wa haki za binadamu ikiwemo THRDC na wengine wengi kwa juhudi za kuhamasisha ushiriki wa mawakili wanawake kwenye kesi za maslahi ya umma na ninaamini kwamba warsha hii italeta matokeo,”amesema Jaji De mello