March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

THRDC YATOA SALAMU ZA POLE KUFUATIA VIFO VYA ASKARI, WASHAURI UCHUNGUZI HURU UFANYIKE HARAKA

Na: Anthony Rwekaza

Mratibu Kitaifa wa Matandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Nchini Tanzania (THRDC) Onesmo Olengurumwa, kwa niaba ya wanachama wa mtandao huo ametoa salamu za pole kwa Viongozi wa Serikali, Jeshi la Polisi na Watanzania wote walioguswa na tukio lililotokea Jumatano Augosti 25, 2021 lililosababisha vifo vya watu wanne Jijini Dar es salaam.

Akizungumzia sakata hilo wakati akiongea na vyombo habari Mratibu huyo Onesmo Olengurumwa amesema Mtandao huo unatoa pole kwa familia ambazo zimepoteza ndugu zao, Jeshi la Polisi ambalo pia limepoteza wafanyakazi wake na pole kwa Watanzania wote walioguswa na tukio hilo .

“Mtandao Watetezi wa Haki za Binadamu ambao una wanachama zaidi ya 200 Nchi nzima, kwa niaba ya wanachama wetu tunapenda kutoa pole kwa familia ambazo zimepoteza ndugu zao, tunafahamu kabsa tukio la jana limechukua maisha ya watu wanne, askari wetu pamoja na majeruhi kadhaa, tunatoa pole kwa familia zote lakini pia tunapenda kutoa pole kwa Jeshi la Polisi na tunatoa pole kwa Watanzania wote walioguswa”amesema Mratibu THRDC, Onesmo Olengurumwa

Pia Onesmo Olengurumwa amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kujitaidi kuwai sehemu lilipotendeka tukio ilo na kufanikiwa kuliweka eneo hilo shwari kwa kumthibiti mtu huyo ambaye nia yake bado haijajulikana, pia amelipongeza Jeshi hilo kwa kuifanya Tanzania iwe shwari muda wote.

“Tupongeze Jeshi la Polisi kujitaidi kuweza kuwai kwenye tukio pamoja kwamba muda ulipita kidogo na kuweza kumthibiti yule kijana ambaye mpaka sasa haikujulikana nia yake ilikuwa nini!,kuweza kumthibiti na atimaye kufanya eneo hilo likaendelea kuwa shwari na usalama wa Tanzania kuendelea kuwa salama kwa muda wote” amesema Mratibu THRDC, Onesmo Olengurumwa

Aidha Onesmo Olengurumwa amesema Mtandao huo unapendekeza kuwa matukio kama hayo yanapotokea ni vyema wananchi wakapewa taarifa kwa uharaka wakajua nini kimetokea, baada ya kufanya uchunguzi huru ambao utawekwa wazi.

” Sisi kama mtandao wa Haki za Binadamu ombi letu kwa matukio kama hata yanapojitokeza ni vyema wananchi wakapewa taarifa kwa harka wakajua nini nini kimetokea na lengo la kutokea,… sisi tunapendekeza kuwepo kwa uchunguzi ambao ni wa huru zaidi” amesema Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa

Katika tukio hilo Mratibu huyo wa THRDC amesema kwa kuwa tukio hilo limetokea mikononi mwa Jeshi la Polisi wanapendekeza Rais Samia Suluhu Hassan au IGP na Waziri wa Mambo ya Ndani kuunda tume ndogo ambayo itaweza kufuatiria kwa undani tukio hilo.

“Tunasema uchunguzi kuwa huru kwa sababu matukio hayo yametokea mikononi mwa Polisi ili kupata taarifa zaidi ya nini kimetokea vyombo vyetu vipo vingi vinaweza, Rais Samia, IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi) au Waziri wa Mambo ya Ndani wakaunda tume ndogo ambayo itaweza kufuatilia tukio kwa undani nakuja kutupa majibu watanzania nini kilitokea ” amesema Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa

Kufuatia mtu huyo kuawa baada ya kusababisha vifo vya watu wanne Mratibu huyo amesema Polisi hawajakiuka sheria yoyote kwa kuwa endapo mtu huyo angeachwa ingewezekana angesababisha madhara makubwa zaidi, amedai labda kungekuwepo na teknolojia za kisasa zaidi labda ndizo zingeweza kufanikisha mazingira ya kumtia mbaroni akiwa hai kama inavyofanyika kwenye Mataifa mengine makubwa.

Ikumbukwe Mapema jana (Jumatano) Augosti, 25, 2021, Jeshi la Polisi kupitia Kamishina wa Oparesheni na Mafunzo (CP), Liberatus Sabas alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililosababisha vifo vya watu wanne wakiwemo askali wa Jeshi la Polisi.

“Leo August 25 mwaka 2021 tumepatwa na tukio baya la kihalifu ambalo limepoteza maisha ya watu wanne. Watatu kati yao ni Askari polisi na mmoja ni askari wa kampuni binafsi ya ulinzi, Askari wetu walikua kazini eneo la makutano ya barabara ya Ally Hassan Mwinyi na Kinondoni, akatokea Mtu na kuwashambulia kwa Bastola. Walipoanguka akachukua bunduki za Askari hao na kuanza kurusha risasi hovyo kuelekea Ubalozi wa Ufaransa”Kamishna wa Oparesheni na mafunzo (CP), Polisi Makao makuu, Liberatus Sabas