February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

THRDC YATOA MAPENDEKEZO MATANO KWA SERIKALI YA TANZANIA UN; IKIWEMO LA KUTOWAONDOA WANANCHI NGORONGORO

Onesmo olengurumwa akiwa katika Mkutano wa 49 wa UPR,jijini Geniva nchini Uswizi

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),kupitia Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao huo, Onesmo Olengurumwa umeshiriki katika Mkutano wa 49 wa Mchakato wa Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu (Universla Periodic Review) katika jiji la Geniva nchini Uswizi ambapo Tanzania imepokea ripoti yake ya mwisho ya mapendekezo ya hali ya haki za binadamu kutoka katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (OHCHR).

Akizungumza katika Mkutano huo Olengurumwa ameipongeza serikali ya Tanzania kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato huo wa UPR pamoja na kutoa ushirikiano mkubwa kwa Asasi za Kiraia na Watetezi wa Haki za Binadamu kabla na wakati wa mapitio ya tatu ya hali ya haki za binadamu nchini.

“Tuko tayari kuendelea kufanya kazi pamoja katika ufuatiliaji wa mapendekezo 187 yaliyokubaliwa (ikiwemo 20 yaliyokubaliwa kwa sehemu). Tunaisihi Serikali yetu iangalie upya msimamo wake kuhusu mapendekezo 67 ambayo hayakukubaliwa hadi sasa,”amesema Olengurumwa.

Pia Olengurumwa ameishukuru serikali kwa kuendelea kutambua maendeleo ya haki za binadamu nchini katika kipindi cha mwaka mmoja tangu Rais Samia Suluhu aingie madarakani na kutoa rai ya kuendeleza ushirikiano huo ili kutanua wigo wa dhamira hiyo njema katika maeneo mengine yahusuyo haki za binadamu.

“Tunashukuru na kutambua maendeleo ya haki za binadamu tunayoendelea kuyapata tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani mwaka mmoja uliopita, pamoja na dhamira yake njema na ya Rais wa Zanzibar, Mhe. Hussein Mwinyi, katika kukuza, kuendeleza na kulinda haki za binadamu na demokrasia Tanzania Bara na Visiwani. Tunatoa wito kwao kuendeleza mapenzi hayo na kupanua dhamira hii njema katika maeneo mengine yahusuyo haki za binadamu na utawala wa kisheria,”ameongeza.

Aidha Olengurumwa akiwa katika Mkutano huo wa UPR amesema wao kama wadau wa Haki za Binadamu wanatambua umuhimu na kupongeza ushiriki wa Serikali ya Tanzania kwenye mchakato wa UPR na kutoa ushirikiano mkubwa kwa asasi za kiraia na Watetezi wa haki za binadamu kabla na wakati wa mapitio ya tatu, na kuwa wako tayari kuendelea kufanya kazi kwa pamoja katika ufatiliaji wa mapendekezo 187 ambayo yamekubaliwa na kupitishwa ikiwemo mapendekezo 20 yaliyokubaliwa kwa sehemu, licha ya hivyo ameisihi Serikali kutafakari upya msimamo wake kuhusu mapendekezo 67 ambayo hayajakubaliwa.

“Tumepokea nia njema ya hivi karibuni ya Tanzania kuhusu uwezekano wa kubadili uamuzi wake wa kuondoa tamko lake chini ya Kifungu cha 34(6) cha Itifaki ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu. Tunatoa wito kwa Serikali kuharakisha mchakato huo ili kuruhusu wananchi na Watetezi wa haki za binadamu kuifikia Mahakama hiyo iliyopo hapa nchini,”

Olengurumwa ametoa wito kwa serikali kufanya maboresho ya mifumo ya sheria ikiwemo kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya pamoja na mabadiliko ya vifungu vya sheria vinavyoathiri shughuli za Asasi za Kiraia na Watetezi wa haki za binadamu nchini hususan Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, Sheria ya Takwimu, Sheria ya Uhalifu wa Kimtandao, Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa, Sheria ya Vyama vya Siasa, Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (kuhusu Maudhui ya Mtandaoni), Mabadiliko ya Sheria ya Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali, pamoja na Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu na Haki za Msingi za Binadamu (BRADEA).

“Tunatoa wito wa mabadiliko ya haraka ya Kifungu cha 4 cha BRADEA ambacho kinazuia asasi za kiraia. Watetezi wa haki za binadamu, na watu wenye nia njema kufungua mashauri ya kikatiba kwa lengo la kulinda katiba na kwa niaba ya wahanga wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo makundi maalumu. Kifungu hiki kinazuia wajibu wao wa kutetea na kulinda katiba na haki za binadamu kupitia mahakama. Vilevile, pawepo na jitihada zaidi katika kuhakikisha ongezeko la makosa yanayostahili dhamana na kuacha maamuzi kuhusu dhamana yabaki kwa mahakama,”amesema Olengurumwa

Pia Olengurumwa ametumia fursa hiyo kuiomba serikali kuridhia mikataba mingine ya kimataifa ikiwemo Mkataba dhidi ya Vitendo vya Utesaji na kutoa penndekezo la kuundwa kwa chombo huru kitakachofuatilia mwenendo wa Jeshi la Polisi ili kuhakikisha na kukuza uwajibikaji katika vyombo vya sheria hususan Jeshi la Polisi Tanzania.

Vilevile Olengurumwa kupitia Mkutano huo ameishauri Serikali ya Tanzania kusitisha mpango uliopo wa kuwaondoa wananchi jamii ya kimasai takribani 70,000 wanaoishi ndani ya Tarafa ya Ngorongoro pamoja na kusitisha mpango wa kumega ardhi ya vijiji ya Pori Tengefu la Loliondo lenye ukubwa wa Kilomita za Mraba 1,500.
“Tunaishauri serikali kwa msisitizo mkubwa isitishe mpango uliopo wa kuwaondoa jamii asili ya wamaasai 70,000 kwenye ardhi yao ya asili iliyoko Tarafa ya Ngorongoro, pamoja na mpango wa kumega ardhi ya vijiji vya Loliondo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,500 Wilayani Ngorongoro. Tunasisitiza uwepo wa ushirikishwaji mpana wa jamii unaozingatia misingi ya haki za binadamu katika mipango yote ya serikali ihusuyo maeneo hayo yenye mgogoro Wilayani Ngorongoro.” Ameongeza Olengurumwa.

Ikumbukwe kuwa mchakato huu wa UPR ulianza mapema mnamo mwezi Novemba mwaka 2021 ambapo Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zilizofanyiwa mapitio ya tathmini ya hali ya haki za binadamu na kupokea jumla ya mapendekezo ya awali 252. Katika mkutano wa leo, Tanzania imepokea jumla ya mapendekezo 269 kutoka Baraka la Haki za Binadamu Umoja wa Mataifa.Huku serikali ya Tanzania ikiwakilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria,George Simbachawene.

Miongoni mwa mapendekezo hayo 269 ambayo Tanzania imeyapokea hii leo 187 yamekubaliwa,20 yaliyokubaliwa kwa sehemu na mengine 67 hayajakubaliwa hadi sasa.