February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

THRDC YAANZA NA WAANDISHI WA HABARI ZA MTANDAONI

Mtandao wa Watetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC) ikishirikiana na Taasisi ya International Center for Not-For-Profit Law (ICNL) wameanza kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari wa mitandaoni juu ya umuhimu wa kuzingatia sheria zinazosimamia tasnia ya habari na kuripoti matukio ya haki za binadamu nchini Tanzania.

Katika ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku tatu yaliyoanza hii leo Mei 10 mjini Morogoro,Mratibu wa Kitaifa wa THRDC,Onesmo Olengurumwa amesema kuwa uhuru wa kujieleza unabeba dhana nzima ya vyombo vya habari na kuna ulazima wa kuwepo kwa uhuru wa kujieleza si kwa wanahabari pekee bali kwa wananchi wote.

“Mafunzo yetu haya yanalenga kuwajengea ninyi uwezo ili muweze kufanya kazi vizuri kuhabarisha watanzania kwani sasa watanzania wengi wanahamia kwenye mitandao kwa sababu ndio vitu vinapatikana kwa urahisi na wakati mwingine kwa gharama ndogo,” ameeleza Olengurumwa.

Olengurumwa ameongeza kuwa baada ya vyombo vya habari mitandaoni kuanza kufanya kazi zaidi ya kuhabarisha umma ndio ulikuwa mwanzo wa kutungiwa kwa sheria na kanuni zisizo rafiki ili kudhibiti uhuru wa mawazo ya watu kupitia mitandao mbalimbali ya Kijamii.
“Tumeendelea na tutaendelea kulalamikia sheria na kanuni kandamizi zilizoundwa na mamlaka kwa ajili ya kudhoofisha uhuru wa Habari nchini Tanzania” ameeleza Olengurumwa

Nae Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Deudatus Balile amewataka wanahabari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mabadiliko ya sheria unaofanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na kufuata weledi na maadili ya taaluma.

“Sheria inaendeleakuwa sheria mpaka hapo itakapobadilishwa tusije tukafika mahala tukasema sheria mbaya tuvunje,tukiivunja inaweza ikatufunga.Kama wanahabari tuoneshe weledi kidogo tuwe tofauti na wale wanaochukua taarifa na kuipost tu mtandaoni,” Amesema Balile na kuwasisitiza waandishi wa habari kuchagua kwenda darasani na kupata kiwango cha elimu kilichowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.

“Kanuni haijabadilika,tukifika Disemba 31 ule tuliopewa wa miaka mitanokujiendeleza unakwisha kwa hiyo tujiandae”

Naye Mkurugenzi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT),Kajubi Mukajanga amesema kuna umuhimu wa kutazama mazingira ya ufanyaji kazi wa vyombo vya habari kwa undani zaidi na kutoa wito wa kufutwa kwa sheria zinazotajwa kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari.

“Tunadhani bila kushughulikia sheria zinazosimamia,zinazoongoza,zinazodhibiti kazi zetu tatizo halitaweza kuisha.Kwa nia njema kwa kiongozi anaweza akaamua kama hivyo akasema vifungulieni vyombo fulani lakini nidhamu ya sheria bado haipo,maana yake ni kwamba kesho anaweza akapata tatizo mtu kwa kutokana na sheria ile ile au huyo huyo aliefunguliwa anaweza akapata tatizo kutokana na sheria ile ile”ameeleza Kajubi Mukajanga.

Kwa upande wake Rais wa UTPC Deogratius Nsokolo,ameeleza kuwa vyombo vya habari nchini vinekuwa katika maumivu kwa muda mrefu na ndiyo yalivyochagiza vyombo vya habari mtandaoni kupata nguvu na vimetoa chachu kwenye maendeleo ya wananchi na uhuru wa kujieleza huku mwandishi wa Habari kutoka Zanzibar Salma Said akikumbushia kuwa tangu mwaka 2012,wandishi wa Habari Zanzibar wanalalamikia kuhusu sheria kandamizi dhidi ya uhuru wa habari visiwani humo.